Karani wa sensa atakayerekodi video jela miezi 6

Muktasari:
- Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema adhabu anayostahili karani aliyefanya kosa la kupiga picha na kurekodi video wakati sensa ya watu na makazi ni faini ya Sh2 milioni, kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Iringa. Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema adhabu anayostahili karani aliyefanya kosa la kupiga picha na kurekodi video wakati sensa ya watu na makazi ni faini ya Sh2 milioni, kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
Amesema ni kinyume cha sheria kwa karani yeyote kufanya hivyo anapochukua taarifa za wananchi na kwamba waliofanya hivyo, watachukuliwa hatua.
Akizungumza leo Agosti 28, katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya Sensa ya Watu na Makazi Mkoani Iringa, Dk Chuwa amesema taarifa zinazotolewa na wananchi ni siri.
Ameeleza kuwa tayari wameanza kuwachukulia hatua baadhi ya makarani waliofanya hivyo na kwamba, kulingana na sheria, adhabu ya kufanya hivyo ni kifungo cha miezi sita au faini ya Sh2 milioni au vyote kwa pamoja.
“Taarifa za wananchi ni siri, kama mtu anaongea sana mtulize mumkali na tafuta majawabu na namna ya kufanya ili upate taarifa zake.
“Bado nawakumbusha tena ni kosa kurekodi au kujirekodi mnapokuwa huko kuchukua taarifa za wananchi,” amesema Dk Chuwa.
Amewataka wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi kwenye kila ngazi kufanya ziara za kuhakikisha kazi ya ukusanyaji wa taarifa kwenye kila nyumba ambayo imewekewa tiki kwamba, imehesabiwa.
Alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na kwamba, Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuhesabiwa kwa asilimia 80.
“Nimekuja kuangalia hali inaendaje huku, suala hili ni muhimu na Rais Samia Suluhu Hassan alishatuambia kwamba sensa ni muhimu, itasaidia kujua huduma za kijamii zitatufikia kwa wakati gani,” amesema.
Akizungumzia kazi hiyo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ipamba, Richard Kikunga amesema mwanzoni walidhani ni ya siku moja hivyo waliwatangazia watu wote kubaki nyumbani wawasubiri makarani.
Amesema kutokana na idadi kubwa ya kaya zilizo kwenye kitongoji hivyo, karani mmoja alikuwa na uwezo wa kuzifikia kaya 12 hadi 15 jambo ambalo liliwafanya wawasisitize kuacha taarifa nyumbani ili kazi nyingine ziendelee.
“Siku ya mwanzo kila mtu alibaki nyumbani lakini sasa kazi zinaendelea kama kawaida. Wanaendelea kutuhesabia,” amesema Kikunga.
Naye Mratibu wa sensa ya watu na mmakazi wilayani Iringa, Yahaya Kiliwash alisema wamefanikiwa kufikia asilimia 90 na kwamba changamoto kubwa kwao ni suala la mipaka.
“Unawez akuona hawa wanataka kuitikia kitongoji hiki na wale kitongoji kingine lakini zaidi ya hilo kazi inaendelea vizuri kabisa tunatarajia mpaka kesho tuwe tumemaliza zoezi zima,” amesema Kiliwash.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Ipamba wamesema kazi kubwa kwao ni kusisitizana ili kila mmoja wao ahesabiwe.
“Tunajijua na tunataka kila mtu ahesabiwe kwa hiyo kazi hii inaendelea kwa kasi sana,” amesema Godfrey Kapoma.