Kardinali Rugambwa aeleza alivyopokea uteuzi wake
Askofu Protase Rugambwa (kulia) akipongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Muktasari:
- Askofu Mkuu Protase Rugambwa alitangazwa na kiongozi wa Kanisa Katoli Duniani, Papa Francis kuwa Kardinali Julai 9, 2023 ambapo atawekwa wakfu kushika wadhifa wa ukadinali Septemba 30, mwaka huu jijini Vatican.
Tabora. Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa amesema taarifa za uteuzi wake kuwa Kadinali alizipata baada ya kumaliza ibada ya Jumapili na kuonyeshwa kwenye simu jambo ambalo lilimshtua lakini akamshukuru Mungu kwa hatua hiyo.
Askofu Rugambwa aliteuliwa Julai 9, mwaka huu na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisco kuwa Kardinali nchini Tanzania hivyo kuwa kardinali wa tatu nchini akitanguliwa na Laurean Rugambwa aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na Polycarp Pengo aliyestaafu mwaka 2019.
Papa amemteua Rugambwa kuwa kardinali ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu alipomteua kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Tabora.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 10, 2023 kwa mara ya kwanza baada ya kutembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani, Askofu Rugambwa amewashukuru waumini wa kanisa hilo kwa sala zao, wakazi wa Tabora na Watanzania wote.
“Tulikuwa kwenye ibada na wakati tunatoka ndiyo nikaelezwa kuna kitu kinapita kwenye mitandao na nikaoneshwa kwenye simu nami nikashtuka nikasema basi tuyapokee hayo ni mapenzi ya Mungu. Siwezi kusema sana juu ya jambo hili lakini nashukuru kwa mapokezi niliyopata na namna watu wa Tabora walivyoonesha utayari wa kushirikiana nami,”
“Nashukuru kwa sara za waumini wenzangu, wakazi wa Tabora na Watanzania wote, sote ni raia wa Tanzania kabla ya kuwa waumini wa dini au dhehebu fulani na jambo muhimu ni kuwafanya Watanzania wawe na furaha, amani na upendo,” amesema Rugambwa
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian akitoa pongezi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan amemuomba Askofu Rugambwa kusaidia wananchi kuondokana na imani za kishirikina na wamjue Mungu, huku akiahidi Serikali kuendelea kushirikiana na kanisa na kumtakia kila la heri katika majukumu yake.
“Jana (Jumapili) usiku baada ya uteuzi Rais (Samia Suluhu Hassan) alinipigia simu nije kukupa pongezi kwa niaba yake pamoja na kuwa alikuwa ametoa pongezi zake kupitia mitandao ya kijamii akaniambia ni vizuri nije,"amesema na kuongeza
“Kwa uteuzi huu Mkoa wa Tabora umepata heshima kubwa na kupitia kituo cha hijja cha Ifucha mkoa wetu unazidi kupata baraka kubwa ikiwamo viongozi kupandishwa vyeo kwa mfano wakuu wa wilaya wawili walipanda vyeo na kuwa wakuu wa mikoa ndani ya muda mfupi pamoja na Jaji Mfawidhi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa,”
Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka amesema uteuzi huo ni neema kwa mkoa huo kwani Mwenyezi Mungu anazidi kuweka baraka zake tangu kuwasili kwa Askofu Rugambwa miezi mitatu iliyopita.
Siku moja kabla ya uteuzi wake (Julai 8, 2023), Askofu Mkuu Rugambwa alishirikiana na Askofu Mkuu, Paul Ruzoka anayetarajia kustaafu mwezi ujao, kupokea sanamu ya bikra Maria kutoka kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga katika Kanisa Kuu la Theresia wa Mtoto Yesu mjini Tabora.