Kasheshe matumizi ya simu katika uhusiano
Muktasari:
- Wakati simu za mkononi zikielezwa kusaidia kurahisisha mawasiliano, matumizi ya kifaa hicho yanatajwa kuwa kichocheo cha migogoro na kuvunja uhusiano wa wenza wengi nchini.
Dar es Salaam. Wakati simu za mkononi zikielezwa kusaidia kurahisisha mawasiliano, matumizi ya kifaa hicho yanatajwa kuwa kichocheo cha migogoro na kuvunja uhusiano wa wenza wengi nchini.
Watu kutumia muda mwingi kwenye simu, kukutwa na meseji zenye utata, kuanzisha uhusiano wa muda mfupi ni miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na wengi dhidi ya wenza wao.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha migogoro isiyokwisha kiasi cha kuvunja uhusiano uliopo ambao ulikusudiwa kuwa wa kudumu au ndoa.
Mshauri wa uhusiano, Degratius Sukambi ametaja namna tatu ambazo simu za mkononi huchangia kuvuruga hatimaye kuvunja uhusiano wa kimapenzi na wakati mwingine ndoa.
Ya kwanza ni kumrahisishia mtu kuvunja uaminifu, kumrahisishia anayesalitiwa kugundua na kusababisha migogoro mingi isitatuliwe.
Sukambi alieleza kuwa tatizo kubwa sio simu ila kifaa hicho kimechochea kwa kiasi kikubwa mifakarakano kwamba ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto unaowaka.
Mshauri huyo alieleza kuwa simu imerahisisha mawasiliano hali inayomuwezesha mtu kuanzisha uhusiano hata na watu ambao hakuwa akitarajia au kujenga ukaribu na watu ambao wanaweza kuwa hatarishi kwenye uhusiano na mwenza aliyenaye.
“Kwenye mapenzi na ndoa simu zimechochea tabia ya watu kutokuwa waaminifu, zimerahisisha mtu kutafuta mbadala na mchakato wa watu kutimiza nia zao za kutokuwa waaminifu umekuwa rahisi mno,” alisema Sukambi.
Kulingana na mshauri huyo, simu pia humwezesha mtu anayesalitiwa kufahamu kwa urahisi juu ya usaliti anaofanyiwa na kupata taarifa za usaliti uliofanywa na mwenzi wake.
“Alikuwa hajui nini kinaendelea lakini kupitia simu anaweza kuona mabadiliko ya mwenzi wake kuanzia kuficha simu, kuweka nywila (password). Hapa lazima mgogoro utaanza itategemea ni namna gani mtautatua ili kunusuru uhusiano wenu,” alisema.
Eneo la tatu ni watu kuacha kuzungumzia tofauti zinapojitokeza na kukimbilia kwenye simu kupunguza msongo wa mawazo matokeo yake kunakuwa na vidonda vingi vinavyoendelea kwenye mioyo ya wahusika.
“Siku hizi wenza wakikwazana badala ya kukaa chini kuzungumza, simu imekuwa mfariji. Mtu anakimbilia Instagram au kwenye magrupu (makundi) ya Whatsapp kuchati badala ya kukabiliana na ukweli kwa kutatua mapungufu yaliyojitokeza.
“Simu zinatumika kama njia ya kuondoa `stress’ (msongo wa mawazo) kwa muda matokeo yake migogoro ndani ya nyumba inarundikana na kuachwa bila kutatuliwa hatimaye inafika wakati watu wanashindwa kuendelea kwa sababu kuna mambo mengi hayazungumzwi,” aliongeza.
Kwa upande wake, Charles Novatus, mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam alieleza kuwa simu zimekuwa zinawatenga wanawake na familia zao kutokana na muda mwingi kutumia kwenye kifaa hicho.
Novatus alisema “utakuta umerudi nyumbani jioni, mkeo hapati muda wa kukaa na wewe mkazungumza masuala ya maisha. Muda wote kainamia simu, anahama tu mitandao ya kijamii, mara Whatsapp, Facebook sijui Instagram wana mambo yao wenyewe.
“Sasa unafikiri niwahi kurudi nyumbani wakati mwenzangu yuko `busy’ na simu hujui kama ni mawasiliano ya kawaida au kuna zaidi ya hayo naona ni heri nipoteze muda huko nje nikirudi nifikie kulala, hapo unatokea ugomvi mwingine, sijui hawa watu wanataka nini,” aliongeza.
Wakati huyo akieleza hivyo Mwajuma Ngeja ambaye ni kungwi alisema amekuwa akiwasisitiza mabinti kuwa makini na matumizi ya simu na kuziogopa simu za waume zao.
“Katika kazi zangu napata kesi nyingi zinazohusu simu, wanawake wanalalamika kukuta meseji za michepuko kwenye simu za wanaume zao, hili ni janga ila ninachosisitiza mwanamke ili uwe na amani na kufurahia ndoa yako kaa mbali na simu ya mumeo.
Wanaume nao wanalalamika wake zao wako mno na simu, siku hizi mitandao ya kijamii inawafanya wanawake wajisahau kutwa nzima ameshika simu, yaani mwanaume yuko naye bado mwanamke anahangaika na simu. Hii haifai ni hatari kwenye ndoa na uhusiano mnaotaka ufike mbali,” alisema Mwajuma.
Mwaka 2020, zaidi ya watu 500 walijitokeza kuomba talaka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) huku zaidi ya 200 zikiombwa jijini Dar es Salaam. Kutetereka kwa mawasiliano baina ya wenza kunachangia hali hiyo.
Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hii tuandikie kupitia 0658376444