Kasoro za kiutaratibu zamfungulia njia koplo aliyefukuzwa kazi
Muktasari:
- Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Morogoro, imemruhusu aliyekuwa askari polisi, Koplo Said Omary Pazzi, kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama nje ya muda wa kisheria kupinga uamuzi wa kufukuzwa kazi, baada ya kubaini kuwa hakukabidhiwa binafsi matokeo na uamuzi wa kesi yake ya nidhamu kama sheria inavyotaka.
Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Morogoro, imemruhusu aliyekuwa Koplo wa Jeshi la Polisi, Said Pazzi kuwasilisha maombi ya mapitio ya mahakama nje ya muda, ili kupinga kufukuzwa kwake kazini kufuatia hukumu ya mahakama ya kijeshi iliyomuhusisha na tuhuma za rushwa.
Uamuzi huo umetolewa Juni 12, 2026 na Jaji Stephen Magoiga, katika shauri lililowakutanisha Pazzi dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Pazzi alifukuzwa kazi mwaka 2023 baada ya kupatikana na hatia katika shauri la nidhamu lililosikilizwa na mahakama ya kijeshi. Baada ya uamuzi huo, adhabu hiyo ilithibitishwa ndani ya Jeshi la Polisi kufuatia matokeo ya kesi hiyo.
Akiwa hajaridhika, Pazzi alikata rufaa kwa IGP ambaye Machi 14, 2024 alithibitisha uamuzi wa kufukuzwa kwake.
Baadaye alikata rufaa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ambaye Machi 5, 2025 alieleza kuwa uamuzi wa IGP ulikuwa wa mwisho ndani ya mfumo wa rufaa wa Jeshi la Polisi na kumwelekeza kutafuta nafuu katika vyombo vingine vya kisheria.
Kupitia maombi yake Mahakama Kuu, Pazzi aliiomba mahakama imruhusu kufungua maombi ya mapitio ya mahakama nje ya muda, akidai kuwa haki yake ya kusikilizwa ilikiukwa katika mchakato wa nidhamu na rufaa.
Alidai kuwa hakuruhusiwa kuwasilisha baadhi ya vielelezo vya utetezi wake na kwamba, hakukabidhiwa matokeo na uamuzi wa shauri lake kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Pia alidai kuwa IGP aliamua rufaa yake bila kumpa nafasi ya kusikilizwa.
Serikali ilipinga maombi hayo ikieleza kuwa Pazzi alishiriki kikamilifu katika shauri la nidhamu, akiwahoji mashahidi wa upande wa mashtaka na kusaini nyaraka mbalimbali za mwenendo wa kesi.
Ilisema madai ya kunyimwa haki ya kusikilizwa hayana msingi kwa kuwa alipewa nafasi ya kujitetea.
Serikali pia ilisisitiza kuwa mlalamikaji alichelewa kwa muda mrefu kuwasilisha maombi hayo bila kutoa sababu za kuridhisha za ucheleweshaji huo.
Katika uamuzi wake, Jaji Magoiga amesema baada ya kupitia kumbukumbu za mahakama ya kijeshi, viapo vya pande zote na hoja za kisheria, ilibidi Mahakama iamue kama kulikuwa na sababu za msingi za kuongezwa muda wa kuwasilisha maombi ya mapitio ya mahakama.
Mahakama imekubaliana na hoja za Serikali kwamba Pazzi alishiriki kikamilifu katika kesi ya nidhamu, akihudhuria mwenendo wa kesi, akiwahoji mashahidi 11 wa mashtaka na kutoa ushahidi wake mwenyewe.
Kwa msingi huo, Mahakama ilibaini kuwa hakunyimwa haki ya kusikilizwa au kujitetea katika mchakato huo.
Hata hivyo, Mahakama imebaini kuwa Pazzi hakukabidhiwa binafsi matokeo na uamuzi wa kesi yake ya nidhamu kama inavyotakiwa na Kanuni C.7(5) za Kanuni za Huduma za Jeshi la Polisi za mwaka 1995.
Mahakama imesema utaratibu wa kuacha nyaraka hizo katika ofisi ya polisi haukutosheleza matakwa ya sheria, kwa kuwa ni wajibu wa mamlaka husika kumfikishia muhusika uamuzi huo moja kwa moja.
“Mahakama inabaini kuwa hakukabidhiwa binafsi uamuzi wa kesi yake kama sheria inavyotaka,” amesema Jaji Magoiga.
Mahakama imeeleza kuwa kasoro hiyo ya kiutaratibu inaibua hoja ya kisheria inayoweza kuhalalisha kuongezwa kwa muda wa kufungua mapitio ya mahakama.
Kutokana na uamuzi huo, Mahakama Kuu imeruhusu maombi ya Pazzi ya kuwasilisha mapitio ya mahakama nje ya muda, hivyo kumfungulia njia ya kupinga uamuzi wa kufukuzwa kwake kazini.