Kata ya Kisegese isiyo na zahanati tangu uhuru
Muktasari:
- Kata hiyo yenye vijiji vitatu vya Ngeleka, Kisegese na Kasyabone ina wakazi hao wanaoishi bila kuwa na zahanati wala kituo cha afya jambo linalosababisa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Wakazi takriban 10,000 wa Kata ya Kisegese wilayani Rungwe katika Halmashauri ya Busokelo Mkoa wa Mbeya, wanakosa huduma za afya tangu nchi hii ipate uhuru miaka 56 iliyopita.
Kata hiyo yenye vijiji vitatu vya Ngeleka, Kisegese na Kasyabone ina wakazi hao wanaoishi bila kuwa na zahanati wala kituo cha afya jambo linalosababisa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Wananchi hao wanateseka licha ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 sura ya 26 kuagiza kuwa kila kijiji nchini kinatakiwa kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya ili kutoa huduma kwa ufanisi kwa wananchi.
Wakazi wa kata hiyo wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata matibabu nje ya kata yao na kusababisha kufika katika wilaya jirani ya Kyela kwa ajili ya kupata huduma hiyo.
Waathirika wakubwa wa tatizo hili ni wajawazito ambao baadhi yao hujifungulia njiani pale wanapozidiwa, huku wengine wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma stahiki za haraka.
Wananchi waeleza mateso, changamoto
“Ikitokea nimeumwa hapa inanilazimu nitembee kwa mguu kutoka hapa kijijini kwetu kwenda hospitali ya Matema ambapo tunatumia muda wa saa nne ili kufika hospitalini hapo,” anasema Edna Ijande, mkazi wa kijiji cha Kisegese.
Anasema hali ni mbaya kwa wakazi wa Kisegese hususan wajawazito na watoto wanapopatwa na magonjwa nyakati za usiku.
Kuna nyakati, Edna hulazimika kutembea kwa mguu kutokana na hushindwa kumudu gharama za kukodi pikipiki, kwa kuwa kutoka kijijini hapo mpaka hospitalini inagharimu kiasi cha Sh Sh25,000.
“Mimi nina binti zangu wawili wote wamejifungua kwa upasuaji katika hospitali za Matema na Itete, lakini binti wa kwanza alinusurika kufariki baada ya kuchelewa hospitalini jambo lililosababisa mtoto kufa akiwa tumboni,” anasema.
Kwa mgeni anayeingia katika vijiji hivyo huenda akadhani ni vipya. Lakini mkazi wa kijiji cha Kisegese, Godfrey Mwakalinga anasema vijiji hivyo ni vya muda mrefu na kwa miaka yote tangu uhuru, wakazi wa kata hiyo wanasumbuliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za afya.
Anasema wagonjwa wanalazimika kutembea au kubebwa mgongoni umbali wa kilometa 20 kufuata matibabu katika hospitali za Matema wilayani Kyela ama Itete ambayo ni ya halmashauri yao.
“Wananchi tuna masikitiko zaidi kwani tunakosa huduma za afya kwenye kata yetu licha ya kuwapo sera ya wazi kuhusu uanzishwaji wa zahanati na hata kituo cha afya,” anasema.
Mwakalinga anasema mwaka 2014 walipelekewa Sh50 millioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na wananchi walichimba msingi na kupeleka mawe, mchanga na kokoto, lakini jambo wanaloona ni la ajabu kwani vifaa hivyo vya ujenzi havijulikani vilipo.
Maumivu ya kukosa huduma za afya yanatesa zaidi familia kutokana na kuleta changamoto katika ndoa na malezi ya watoto kama anavyosema, Eston Mwaijuni mkazi wa kijiji hicho.
“Ukosefu wa huduma za afya unachangia vifo vya watoto wachanga na hata wajawazito kutokana na ukweli kwamba wajawazito wengi wanakosa huduma za kliniki na hata huduma za uzazi’’ anasema na kuongeza:
“Mwezi uliopita tumempoteza binti mmoja ambaye alikuwa anasumbuliwa na malaria. Ndugu zake wakiwa kwenye harakati za kumpeleka katika Hospitali ya Itete alipoteza maisha kabla hajafika hospitalini. Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma maana tunazidi kuangamia”.
Utafiti uliyofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza mwaka 2013 unaonyesha zaidi ya asilimia 37 ya wagonjwa wa vijijini wanatembea kwa miguu wakituma zaidi ya muda wa saa moja kufuata huduma za afya.
Moja ya sababu za kero hiyo ni kutokuwapo kwa uwiano wa vituo vya huduma za afya kwa wananchi hususani katika maeneo ya vijijini.
Vituo vya kutoa huduma za afya vipo mbali na watu wengi huku wananchi wengine wakitembea umbali mrefu na kukabiliwa na ubovu wa miundombinu, huku vituo vingine vikiwa na upungufu wa wataalamu wa afya na vifaa tiba.
Magonjwa yaliyopiga kambi Kisegese
Kama ilivyo kawaida kwa sehemu nyingi nchini, magonjwa yanayoshambulia mara kwa mara wakazi wa kata ya Kisegese ni malaria, kuhara na homa za kawaida.
Taarifa ya hali ya afya katika Halmashauri ya Busokelo inaonyesha malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kuwashambulia wananchi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kisegese, Alex Mwakifwamba anasema pamoja na kwamba hawana huduma za afya magonjwa yanayowasumbua zaidi katika kata ni malaria.
“Awali tulikuwa na duka la dawa hapa mbapo wananchi walikuwa wanapata matibabu ya awali kabla ya kwenda hospitali kubwa lakini nalo limefungwa juzi juzi na hatuelewi sababu za kufungwa kwa duka hilo,” anasema.
Kwa nini Kisegese haina zahanati wala kituo cha afya licha ya wananchi kujitolea vifaa vya ujenzi kama mawe na mchanga huku halmashauri nayo ikitoa Sh50 milioni?
Diwani wa kata ya Kisegese, Edson Mbila anakiri kupokea fedha hizo na kusema kuwa hawakuona haja ya kujenga zahanati kwa kipindi kile kwa kuwa tatizo lilopo ni kubwa hivyo viongozi wa kata walikubaliana kuitunza fedha kwa ajili wa kituo cha afya.
“Ni kweli mwaka 2014 tulipokea Sh50 milioni kutoka halmashuri kwa ajili ya kujenga zahanati ya Kijiji cha Kisegese,lakini mimi na viongozi wenzangu pale ofisini tukashauriana kuwa kutokana ukubwa wa tatizo tusijenge kituo cha afya,na tumeshindwa kujenga muda wote huo kutokana na wananchi kutohamasika kufyatua matofali,”anasema Mbila.
Mwanga wa kujenga kituo cha afya waonekana
Mbila anasema Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya alifika katika kata hiyo Julai mwaka huu na kuwawagiza wenyeviti wa vijiji kuhakikisha kila kijiji kinafyatua matofali 10,000 kabla ya Oktoba mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.
‘’Pia tunao mpango mkakati wa kuendelea kujenga zahanati katika Kijiji cha Ngeleka na tayari eneo kwa ajili ya ujenzi huo limetengwa’’ anasema.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eston Ngilangwa anasema halmashauri yake yenye kata 13 na vijiji 52 ina kituo cha afya kimoja tu na zahanati 21.
Kutokana na changamoto hiyo, wamekuwa wakiwahamasisha wananchi kutoa michango kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata.
Ngilangwa anasema Halmashauri imetenga Sh20 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kisegese ambapo nguvu kazi ya wananchi ndiyo utakuwa mtaji mkubwa kulimaliza tatizo hilo.