Kata ya Mshewa kujengwa kituo cha afya, mabweni ya wanafunzi

Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk David Mathayo

Muktasari:

Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk David Mathayo amesema wameanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mshewa akibainisha kuwa kikikamilika kitasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Same. Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk David Mathayo amesema wameanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mshewa akibainisha kuwa kikikamilika kitasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 5, 2021 katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi kwa kumchagua na kukabidhi gari la wagonjwa.

"Natambua katika kata hii hakuna kituo cha afya, ipo zahanati lakini nimekubaliana na diwani wa hii kata tumeanza mchakato tutajenga kituo cha afya eneo la kliniki ya zamani na kituo hiki kitasaidia wajawazito kujifungulia hapa karibu badala ya kupelekwa hospitali ya Wilaya Same.”

"Natambua wajawazito wanapata shida pindi wanapokosa huduma katika zahanati na hulazimika kwenda vituo vya afya katika kata nyingine au hospitali ya Wilaya ambako ni mbali, sasa hapa lazima pawe na kituo cha afya,” amesema mbunge huyo.

Amesema wamejipanga kujenga mabweni mawili katika shule ya sekondari Kwizu iliyopo katika kata hiyo, hatua ambayo itawapa wanafunzi fursa ya kujisomea kwa bidii na kufaulu vizuri masomo yao.

"Katika shule ya sekondari Kwizu yatajengwa mabweni mawili, kila bweni litaingia wanafunzi 80 na kufanya jumla ya wanafunzi 160,hatua hii itakuwa chachu kwa wanafunzi kusoma kwa bidii, na kuinua taaluma maana hawatatembea tena umbali mrefu na wanafunzi wa kike wataondokana na vishawishi njiani,” amesisitiza.

Rehema Jumanne, mkazi wa kata hiyo amesema kupatikana kwa kituo cha afya kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.