Katavi wafanya sensa kwa amani

Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko (kulia) akitoa taarifa zake kwa karani wa sensa Aston Kajuba. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema sensa imefanyika kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi ambao hawajafikiwa kuwa wavumilifu.

Katavi. Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ameshiriki sensa ya watu na makazi kwa kuhesabiwa akisema ulinzi umeimarishwa.

Akizungumza na mwananchi leo Agosti 23, 2022 nyumbani kwake mtaa wa Misha Road kata ya Ilembo Manispaa ya Mpanda, amesema wananchi wameonyesha umakini mkubwa kutoa taarifa zao.

"Mimi nimehesabiwa na familia yangu ya watu watano, makarani wameandaliwa vizuri wana nidhamu ya kutosha.

"Niwasihi wananchi wasikate tamaa kwa maeneo ambayo hawajafikiwa na makarani, kwani sensa hii ni endelevu," amesema Mrindoko.

Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Katavi Hassan Rugwa amesema uongozi umejipanga kikamilifu kuhakikisha wote wanahesabiwa.

"Tumeshirikisha makundi yote,tutasimamia usiku na mchana ili adhima ya serikali itimizwe," amesema.

Karani wa eneo la Aston Kajiba amesema changamoto aliyokutana nayo ni Mwenyekiti wa mtaa kutokuwepo kutokana na sababu za kikazi.

"Wananchi wamenipokea vizuri japo Mwenyekiti wa mtaa hayupo wanaonyesha wamepata elimu ya kutosha," amesema.

Edson John mfanyabiashara wa mifugo Mpanda amesema amehesabiwa akiwasihi wengine kutii agizo la serikali na kwamba mahitaji ya huduma yatapatikana kulingana na idadi iliyopo.