Katibu Bakwata Kagera akatwa mkono, mkataji auawa kwa kipigo

Katibu wa Bakwata Mkoa wa Kagera, Hamza Zacharia akiwa kitandani katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba alikolazwa akitibiwa majeraha baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kushoto na Mkazi wa Muleba mkoani humo, Abdulmalick Yahya, ambaye naye aliuwawa kwa kipigo na wananchi wenye hasira kali. Picha na Mpiga Picha wetu

Muktasari:

  • Polisi yasema mtuhumiwa alikuwa akilipa kisasi baada ya kufukuzwa kazi.

Mwanza. Mkazi wa Muleba mkoani Kagera, Abdulmalick Yahya (42) ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi, baada ya kuonekana akimshambulia kwa panga Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kagera, Hamza Zacharia (43).

 Kutokana na tukio hilo, Zacharia anauguza majeraha katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba. Shambulio hilo limesababisha apoteze kiganja cha mkono wa kushoto.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Februari 6, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amethibitisha tukio hilo lililotokea Ijumaa Februari mosi, mwaka huu.

Chatanda amesema uchunguzi wa awali umebaini Abdulmalick kabla ya kutekeleza tukio hilo, alikuwa mtunza stoo ya vifaa katika mradi wa ujenzi wa jengo la Bakwata Complex linalojengwa katika Manispaa ya Bukoba.

“Februari mosi, 2024 alifukuzwa kazi ya kutunza ghala (stoo) la vifaa vya ujenzi wa Complex hiyo na kamati ya ujenzi, akamtuhumu Katibu wa Bakwata kwamba ndiye chanzo cha hayo yote. Kwa hiyo akaplan (akapanga) kulipa kisasi,” amesema Kamanda Chatanda.

Amesema, “Kitendo hicho kilisababisha mashuhuda waliokuwepo kujaribu kumzuia asiendelee kumjeruhi na walipoona anageuka na kutaka kuwadhuru, walimshambulia hadi pale alipookolewa na polisi na kuwahishwa hospitalini. Hata hivyo, alifariki dunia akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Bukoba.”

Kamanda Chatanda amesema uchunguzi kuwabaini waliohusika kumshambulia na kusababisha kifo cha mtuhumiwa huyo unaendelea.

Amesema watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Tunawaomba wananchi kumrudia muumba wao, hilo litawaongeza hofu na kuthamini maisha ya wenzao. Pia jamii iepuke kujichukulia sheria mkononi, ndiyo maana mtu akikosea tunatakiwa kumkamata au kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali, ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.

Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta alipotafutwa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Amesema mamlaka zinazoshughulikia makosa ya jinai ndiyo zenye mamlaka ya kulizungumzia.

“Unajua hizo taarifa unazosema ni jinai ziko polisi na mimi sipo niko safarini nje ya mkoa. Nami nasoma habari kama wanavyozisoma wengine, pengine nikifika nitafahamu na kulizungumzia,” amesema Sheikh Kichwabuta.

Shuhuda wa tukio hilo, Said Fabian amesema; “Alimkatakata panga kidogo mgongoni yule bwana (Zacharia) akadondoka katika hali ya kujitetea akaweka mkono kichwani, ili asikatwe panga kichwani, kwa hiyo yule bwana (Abdulmalick) alichofanya alikata palepale mkono ulipokuwa mpaka akautoa."

Majeruhi afunguka

Majeruhi wa tukio hilo, Zacharia amesema alilazimika kuigiza kwamba amefariki ili asiendelee kushambuliwa maeneo mengine ya mwili.

“Wakati anakata mimi na-guard (najikinga) na mkono, kwa hiyo kila akitupa panga mimi naweka mkono, hali ilivyoendelea hivyo ilibidi nijifanye nimefariki kwa hiyo akakata mara ya mwisho akaona mimi sijitingishi ndiyo akaondoka," amesema.