Baba wa kambo ajeruhi mtoto kwa kisu
Muktasari:
- Awali, mtoto aliadhibiwa kwa kuchapwa viboko na mama yake kutokana na madai ya kuiba mayai.
Kibaha. Mkazi wa Kongowe, Abdallah Machupa (49), anashikiliwa polisi akituhumiwa kumkata kwa kisu kichwani mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka mitano akidaiwa kuiba mayai mawili.
Mtoto huyo (jina linahifadhiwa) ni mwanafunzi wa shule ya awali katika Shule ya Msingi Kongowe mjini Kibaha, ambaye amepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna amesema mtuhumiwa anadaiwa kutenda ukatili huo jana Septemba 5 muda mfupi baada ya mama mzazi wa binti huyo kumkanya mwanaye kwa kumchapa viboko na kumuachia.
Amesema wakati mama akimuadhibu mtoto huyo, mtuhumiwa alikuwa mtaani na alipopata taarifa kuwa mtoto ameiba mayai mawili kwa bibi yake alirejea nyumbani.
Kamanda Shanna amesema alipofika nyumbani, mtuhumiwa alichukua panga ili kumuadhibu lakini alidhibitiwa na kaka wa mtoto huyo ndipo alipotoa kisu na kumkata nacho kichwani.
Amesema kutokana na kelele za familia hiyo, baadhi ya majirani walifika na kumdhibiti kwa kumnyang’anya kisu. Kamanda Shanna amesema majirani hao walimshambulia mtuhumiwa kwa ngumi, mateke na fimbo kabla ya askari kufika na kumfikisha kituo cha polisi.