Kauli ya DC Mapunda yaibua mjadala
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda
Muktasari:
- Ni kuhusu marufuku ya kupiga picha na fedha nyingi wilayani Temeke, wachumi wasema kumiliki fedha nyingi na kufurahia mafanikio si jambo baya, lakini kujionyesha mali bila maelezo ya wazi kuhusu chanzo chake kunaweza kuibua maswali kuhusu uhalali wa mapato.
Dar es Salaam. Mwenendo wa watu kupiga picha na fedha nyingi na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii umezua mjadala kuwa tabia hiyo inaweza kuwa na athari kwa usalama wa watu, mienendo ya vijana na uelewa kuhusu namna sahihi ya kuonyesha mafanikio.
Mjadala huo umekuja kufuatia Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, kuonya dhidi ya tabia ya baadhi ya watu kupiga picha wakiwa na fedha nyingi na kuzisambaza mitandaoni, akisema maonesho hayo yanaweza kuwavutia wahalifu na kuwafanya vijana kuvutiwa na maisha ya mafanikio ya haraka bila kujua chanzo cha mali hizo.
Julai 23, 2026 akiwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Kupinga Dawa za Kulevya Mapunda alipiga marufuku wananchi wa wilaya yake kupiga picha wakiwa wanaonyesha mafungu makubwa ya fedha na kuyasambaza mitandaoni.
Wachumi wanasema kuwa kumiliki fedha nyingi na kufurahia mafanikio si jambo baya, lakini kujionyesha mali bila maelezo ya wazi kuhusu chanzo chake kunaweza kuibua maswali kuhusu uhalali wa mapato, kuchochea tamaa ya kupata fedha kwa njia za mkato na kuathiri mtazamo wa baadhi ya vijana kuhusu mafanikio.
Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa uchumi Felix Masawe amesema suala la msingi si kuzuia watu kufurahia mafanikio yao, bali kuhakikisha kunakuwa na uwazi kuhusu chanzo cha utajiri unaoonyeshwa hadharani.
Amesema maonesho ya fedha nyingi yanaweza kuwa na athari za kijamii kwa kuwa yanaweza kuwafanya baadhi ya vijana kuamini kuwa mafanikio yanapatikana kwa njia za mkato badala ya kufanya kazi na kujenga uwezo.
"Jamii inapaswa kuhamasishwa kuthamini mafanikio yanayotokana na kazi halali. Mtu akiwa na mafanikio ni jambo jema, lakini ni muhimu pia kuwepo kwa uwajibikaji na uwazi kuhusu chanzo cha kipato," amesema Masawe.
Kwa upande wake, mshauri wa masuala ya fedha Gerson Msemo amesema utamaduni wa kuonyesha fedha nyingi mitandaoni unaweza kuongeza pengo la matarajio kwa vijana ambao wanaweza kutaka kufikia maisha hayo kwa haraka bila kuzingatia mchakato wa kujenga uchumi wao.
Amesema baadhi ya maudhui yanayoonesha utajiri mkubwa bila maelezo ya shughuli za kiuchumi yanayouwezesha yanaweza kuleta taswira potofu kuhusu mafanikio.
"Vijana wengi hutazama mitandao ya kijamii kama kioo cha maisha halisi. Wanapoona mtu ana fedha nyingi, magari ya gharama na starehe nyingi bila kuona safari ya mafanikio, wanaweza kudhani njia pekee ya kufanikiwa ni kupata fedha kwa haraka," amesema.
Msemo amesema kinachohitajika ni jamii kuhamasisha utamaduni wa kuonyesha safari ya mafanikio badala ya kuonyesha matokeo pekee.
"Ni muhimu watu waoneshe pia jitihada, ubunifu na kazi iliyowawezesha kufikia walipo. Hilo linaweza kuwa elimu kwa wengine badala ya kuwa kichocheo cha tamaa," amesema Msemo.
Naye mchumi Marietha Nyoni amesema mamlaka zina sababu ya kuangalia mwenendo huo kwa upande wa usalama na masuala ya kodi, ingawa hatua hizo zinapaswa kuzingatia haki za mtu binafsi.
Amesema fedha zinazoonyeshwa hadharani zinaweza kuwa ishara inayohitaji uchunguzi zaidi pale zinapokuwa hazilingani na shughuli au kipato kinachojulikana cha mhusika.
“Si kila mtu anayeonyesha fedha nyingi amefanya kosa, lakini pale ambapo kuna tofauti kubwa kati ya maisha yanayoonyeshwa na shughuli inayojulikana, mamlaka zinaweza kutaka kujiridhisha kuhusu chanzo cha mapato hayo," amesema Marietha.
Amesema pamoja na hatua za udhibiti, elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na usalama binafsi inapaswa kupewa kipaumbele.
"Mitandao ni sehemu ya maisha yetu sasa, lakini matumizi yake yanahitaji busara. Kuonyesha kila kitu ulicho nacho kunaweza kuwaweka watu kwenye hatari," amesema Marietha.
Akizungumzia hilo mkazi wa Temeke, Amina Salum, amesema maonesho ya fedha kwenye mitandao yamekuwa yakichochea baadhi ya vijana kutamani maisha yasiyoendana na uwezo wao.
"Wengine wanaona picha za watu wakiwa na pesa nyingi na magari ya kifahari, wanaanza kutafuta njia za haraka za kupata fedha bila kujali madhara yake. Tahadhari kama hizi zinaweza kusaidia," amesema.
Mkazi wa Buza Richard Mussa, amesema mamlaka zinapaswa kuhakikisha hatua hizo hazionekani kama zinazuia watu kuonyesha mafanikio yao yanayotokana na kazi halali.
"Kama mtu amefanya biashara, amelipa kodi na amepata mafanikio, ni muhimu pia tuheshimu hilo. Kinachotakiwa ni kufuatilia wale ambao chanzo cha mali zao hakieleweki," amesema Mussa.
Alichokisema DC huyo
Amesema mtu anayepata fedha kwa njia halali mara nyingi hana sababu ya kuzifanya kuwa maonesho kwa sababu hata watu wenye mishahara mikubwa hawatangazi kiasi wanachopata.
"Wewe umefanya kazi, mshahara umeingia tarehe 20 au 22, mbona hujapiga picha na mshahara wako na kutuambia leo umepata mshahara? Kwa nini mshahara wote mnaweka siri?" amesema.
Mapunda amesema maonesho hayo yanaweza kuhatarisha usalama wa wahusika kwa kuwavutia wahalifu.
"Temeke marufuku kupiga picha na fedha nyingi kama huamini jaribu uone kesho yake kitachotokea, nitakachofanya ni kumwambia OCD kamkamate, muweke ndani kwa sababu anatamanisha majambazi wakamvamie ili usalama wa eneo letu uwe mbaya. Mbali na hilo nitawaelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waje kuchukua kodi yao maana huyu umepata faida iliyopitiliza," amesema Mapunda.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema hana tatizo na watu kuwa na maisha mazuri, magari ya kifahari au kufurahia mafanikio yao, lakini ni muhimu jamii kujiuliza kuhusu chanzo cha mali zinazoonekana kutokuwa na maelezo.
"Mimi ni muumini wa watu kuwa na maisha mazuri. Napenda watu wawe na magari mazuri, waishi vizuri. Sina roho ya husuda. Ila tunapopata maswali kuhusu namna gani kafika pale ni vyema tukaulizana kwa ustaarabu," amesema.
Amesema mamlaka zimebaini kuwa moja ya sababu zinazowasukuma baadhi ya vijana kuingia katika biashara ya dawa za kulevya ni kuvutiwa na maisha ya kifahari wanayoona kwa wenzao bila kufahamu chanzo cha kipato chao.
"Tumethibitisha moja ya sababu zilizowaingiza vijana kwenye usafirishaji wa dawa za kulevya na uuzaji wa dawa za kulevya ni maisha mepesi ambayo wanaona vijana wenzao wanaishi tofauti na kipato," amesema Mapunda.