Kauli ya Dk Mwigulu ya vidumu shuleni yawaibua wadau
Muktasari:
- Ripoti ya SWASH inaonesha pengo la huduma za maji shuleni. Wadau wamesisitiza umuhimu wa mipango mbadala, uwajibikaji wa utekelezaji na usawa wa kijinsia.
Dar/Arusha. Wakati Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba akipiga marufuku wanafunzi wa sekondari na msingi kubeba vyombo vya maji maarufu vidumu shuleni maarufu vidumu, wadau wa elimu wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya uamuzi huo.
Wamesema Serikali inapaswa kufanya tathmini ya kijiografia na kutenga rasilimali fedha za kutosha ili kumaliza tatizo hilo kwa shule nyingine, hususan za maeneo ya pembezoni.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Maji, Usafi wa Mazingira na Tathmini ya Usafi Mashuleni (SWASH) ya mwaka 2018, inaonesha angalau shule tatu kati ya tano za msingi nchini zina huduma ya maji inayotokana na vyanzo vya maji vilivyoboreshwa, wakati shule moja vyanzo vyake havijaboreshwa na moja haina chanzo chochote cha maji.
Ripoti hiyo imebainisha zaidi kuwa angalau shule nne kati ya tano zilizopo mjini zina huduma ya maji yenye vyanzo vilivyoboreshwa, ukilinganisha na shule tatu kati ya tano kwa maeneo ya vijijini.
Chanzo kikuu cha maji ya vyanzo vilivyoboreshwa ni maji ya bomba kwa asilimia 29.5, ikifuatiwa na visima kwa asilimia 12.1.
Wakati ripoti hiyo ikionesha hivyo, leo Jumanne, Februari 24, 2026, Dk Mwigulu akifungua kikao cha Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira jijini Arusha, pamoja na mambo mengine aliyoagiza, amesema wanafunzi wa sekondari na shule za msingi kubeba maji shuleni ni mambo ya zamani.
Amesema wamekubaliana Taifa linapoelekea, taasisi zote zinazokusanya watu ziwe na maji, na kuwa kila shule ya msingi, sekondari, vituo vya afya na zahanati vipate huduma hiyo muhimu.
“Kwa kuwa wote mko hapa wakurugenzi na watendaji wakuu, tunapotoka sasa hivi, tunaposema tupate maji vijiji vilivyosalia, wekeni pia kwenye daftari zenu, sitaki kusikia wanafunzi wanaenda na vidumu vya maji shuleni.
“Kila shule ya msingi na sekondari iwe na maji, wanafunzi wapate maji palepale. Haya mambo ya kila mwanafunzi kufunga kigudulia pembeni ni mambo ya zamani,” amesema Dk Mwigulu na kuongeza;
“Kwa hiyo, mipango yetu tuliyosema imebaki vijiji zaidi ya 1,500, wekeni ramani hiyo. Kila shule hapa nchini, zahanati, kituo cha afya na hospitali viwe na maji, inaweza ikawa mradi au kisima.”
Waziri Mkuu huyo amesema: “Kwa hiyo twendeni tukalifanye hilo. Tukijipa mwaka mmoja inatosha kuwa tumeshamaliza shule zote ziwe na maji. Wakati mwingine maisha ni shule nzuri kuliko shule yenyewe, uzoefu wa tatizo ni shule nzuri kuliko shule yenyewe. Wale waliosoma shule za bweni nadhani mmenielewa mkipangwa shule ambayo haina maji, eeeh, tulimalize hilo tatizo katika shule zetu.”
Baada ya Dk Mwigulu kueleza hayo, Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali juu ya uwezekano wa hilo kutekelezeka. Mdau wa elimu, Ochola Wayoga, amesema wazo la kila shule kuwa na chanzo chake cha maji linawezekana endapo Serikali itaweka dhamira ya dhati na kutenga rasilimali za kutosha.
“Katika karne hii, unajenga vipi shule isiyo na maji? Serikali imewezaje kuruhusu shule ianze kufanya kazi bila huduma muhimu kama maji? Hili linahusu pia usalama na afya za watoto,” amesema.
Amesema kupiga marufuku wanafunzi kubeba madumu ni hatua moja, lakini changamoto kubwa ipo kwenye kuruhusu shule kujengwa bila miundombinu muhimu.
“Kama kuna jambo la kupigwa marufuku vikali, basi ni ujenzi wa shule zisizo na maji na huduma za msingi,” ameongeza.
Kwa mtazamo wake, utekelezaji wa agizo hilo unahitaji bajeti mahsusi, akidai uchimbaji wa visima katika shule zote nchini unaweza kugharimu takribani Sh180 bilioni, fedha ambazo amesema zinaweza kupatikana iwapo kipaumbele kitawekwa.
Akizungumzia hilo, mhadhiri wa sera za elimu, Dk Rehema Msuya, amesema agizo hilo linapaswa kuambatana na tathmini ya kina ya kijiografia, akibainisha si kila eneo lina uwezo wa kupata maji ya chini ya ardhi kwa urahisi.
“Zipo shule katika maeneo yenye miamba au ukame mkali, ambapo uchimbaji wa kisima unaweza kuwa ghali au usizae matokeo. Serikali inapaswa kuweka mbinu mbadala kama kuvuna maji ya mvua au kuunganisha shule kwenye miradi ya maji ya jamii,” amesema Dk Msuya.
Meneja mradi wa asasi ya GirlsEdu, Halima Sanga, amesema ukosefu wa maji shuleni unaathiri zaidi wasichana, hasa wakati wa hedhi.
“Maji ni suala la usawa wa kijinsia pia. Msichana akishindwa kupata mazingira salama na maji ya kutosha, anaweza kukosa shule siku kadhaa kila mwezi. Hili ni jambo linalohitaji suluhisho la haraka na la kudumu,” amesema.
Naye mchambuzi wa sera za umma, Benson Kileo, amesema kauli ya Waziri Mkuu inapaswa kuambatana na waraka rasmi wa utekelezaji utakaoainisha vyanzo vya fedha, muda wa utekelezaji na taasisi zitakazowajibika.
“Tumeshuhudia matamko mengi mazuri yakikosa meno ya utekelezaji. Ili safari hii iwe tofauti, lazima kuwe na uwajibikaji wa wazi na tathmini ya mara kwa mara,” amesema.
Aidha, katika kuimarisha mapato na nidhamu, Dk Mwigulu ameagiza kukomeshwa kwa miunganisho haramu inayofanywa na vishoka, akitolea mfano watu wanaojiunganishia maji kwa shughuli za viwandani au kufyatua tofali huku bili zikielekezwa kwa wananchi wa kawaida.
Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema kwa kipindi cha miaka minne ya hivi karibuni, zaidi ya Sh3 trilioni zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji.
“Vijijini tunaendelea na miradi ya maji na tumefikia asilimia 85.2, huku mijini tukifika asilimia 92.5, na tuna miradi 28 inayoendelea,” amesema.
Aweso amesema kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), katika vijiji vyote 12,333 nchini, vijiji 10,758 vimeunganishwa na huduma ya maji huku vikibaki vijiji 1,575 pekee.
Amesema Bodi za Mamlaka za Maji zilizozinduliwa leo zimeundwa ili kusimamia mamlaka za maji zilete ufanisi na kuondoa malalamiko ya wananchi katika huduma hizo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Andilile, amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji kwa lengo la kuimarisha ustawi wa Watanzania, na kuwa wao kama wasimamizi watahakikisha wanasimamia uwekezaji huo ili ulete tija kwa wananchi.
Amesema ni muhimu wajumbe wa bodi hizo kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kufikia malengo ya kumtua mama ndoo kichwani.