Kauli ya Mbowe yaibua mjadala

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe akitaka chanjo ya Covid 19 kuwa ya lazima kwa wananchi wote, baadhi ya wasomi na wanasiasa wamekuwa na mtazamo tofauti.

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe akitaka chanjo ya Covid 19 kuwa ya lazima kwa wananchi wote, baadhi ya wasomi na wanasiasa wamekuwa na mtazamo tofauti.

Kwa nyakati tofauti Rais, Samia Suluhu amekuwa akisisitiza suala la wananchi kupata chanjo litakuwa ni hiari na sio lazima.

Mei 14, mwaka huu akiwa katika baraza la Idd, Rais Samia alisema ili kukabiliana na ugonjwa huo ni lazima kushirikiana na mataifa mengine, lakini Serikali itaendelea kuchukua tahadhari mbalimbali, ikiwemo matumizi ya chanjo ya ugonjwa huo ambapo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) walitaka chanjo hiyo kutolewa kwa hiari.

Hata hivyo, juzi Mbowe akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa mkoani Mwanza alisema utolewaji wa chanjo kwa hiari ni kinyume na utaratibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata hivyo, baadhi ya wasomi na viongozi wa vyama vya siasa wamepinga kauli ya mwenyekiti huyo na kusisitiza kuwa msimamo wao katika suala la chanjo zitolewe kwa hiari.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Addo Shaibu alisema kwa kuzingatia hali ya tafiti zinazoendelea inapaswa suala hili libaki kuwa la hiari.

“Napendekeza chanjo ipatikane kwa wingi, pia nakubaliana na Mbowe chanjo igharamiwe na Serikali, lakini nadhani bado tuache iwe huru kwa watu kupata chanjo au kutopata chanjo,” alisema Shaibu.

Naye Mwenyekiti wa NCCR, Mageuzi, James Mbatia alitaka Mbowe aulizwe vizuri ili kufafanua kauli yake kwani inawezekana aliteleza ulimi.

Mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano kwa umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa alisema chanjo zinazofanywa katika maeneo mbalimbali duniani bado kwenye nchi za Afrika zinakuja kwa ajili ya majaribio hivyo ni vema jambo hilo liwe la hiari.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema suala la chanjo bado ni changamoto kwa kuwa wengi hawajui kama ni hiari au lazima.

Alibainisha kuwa chanjo hiyo inapaswa kuwa hiari mfano wa chanjo ya homa ya njano, kwa kuwa bado kuna sintofahamu, wengine wakisema ina madhara na wengine wakisema haina.

“Wananchi wana haki ya kujua hata kama itakuja kuwa lazima, wana haki ya kujua madhara ya hiyo kitu na ili watu wengi waweze kupenda taarifa zaidi zitolewe,” alisema Henga.

Dk Richard Mbunda, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema suala la Serikali kugharamia matibabu kwa wagonjwa na chanjo analiunga mkono kwa kuwa wananchi wanakumbana na janga hilo wakiwa kwenye majukumu yao.

“Suala la chanjo kuwa la lazima hilo siliungi mkono, wananchi wanapaswa kuelimishwa kwanza ili kujua umuhimu wa chanjo” alisema.