Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya Rais Samia wanaoidai Tanzania inakiuka haki za binadamu

Muktasari:

  • Novemba mwaka jana, Bunge la Ulaya liliituhumu Tanzania kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na mauaji yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.



Dar/Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina historia na misingi imara ya kuheshimu haki za binadamu, akisisitiza wanaodai nchi inakiuka haki hizo wanafanya kile alichokiita kumpa mbwa jina baya ili kumuua.

Amesema mabadiliko ya siasa za ulimwengu yamesababisha vijana, hasa wa mataifa ya Afrika, kujazwa sumu na kuaminishwa kuwa nchi zao zinakiuka haki za binadamu.

Samia amekuja na kauli hiyo katika kipindi ambacho Tanzania imetolewa matamko kadhaa na jumuiya ya kimataifa ambayo, pamoja na mambo mengine, yanaituhumu kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Novemba mwaka jana, Bunge la Ulaya liliituhumu Tanzania kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na mauaji yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea nakala ya kitabu Falsafa ya Sheria ya Mama Samia (Mama Samia Doctrine of Law) kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Julai 13, 2026. Kitabu hicho kinaelezea historia, falsafa na mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia. Picha na Ikulu.

Julai 10 mwaka huu, Jumuiya ya Madola nayo ilitoa tamko la kuitaka Tanzania kutafuta suluhu ya kisheria na kisiasa na kuruhusu uhuru wa kujieleza na kukusanyika, ikisema vitendo vya kuzuia haki hizo vinakiuka haki za binadamu.

Ukiacha matamko ya jumuiya za kimataifa, baadhi ya wanaharakati pia wamekuwa wakiituhumu Serikali ya Tanzania kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Rais Samia amesema hayo leo, Jumatatu, Julai 13, 2026, alipohutubia ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali na kusema kumekuwa na wimbi la kuwaaminisha vijana kuwa Serikali zao, hasa za Afrika, hazifuati au zinakiuka haki za binadamu.

“Hapa nataka tuukumbushe ulimwengu, na watu wetu wajue kwamba, kwa upande wa Tanzania, sisi ni wafuasi wazuri sana wa haki za binadamu. Mtakumbuka sisi Tanzania tuliweka kwa mara ya kwanza kwenye Katiba yetu ule mtiririko wa haki za binadamu tulipobadilisha sheria mwaka 1984,” amesema.

Amesema Tanzania imetanua wigo wa haki hizo na imetunga sheria nyingine zinazoweka nguvu ya utekelezaji wa haki hizo, huku wananchi wakipewa nafasi ya kudai haki mahakamani.

Pamoja na hayo, amesema kwa sababu Tanzania ipo ndani ya Afrika, imesaini Tamko la Haki za Binadamu la bara hilo.

“Sasa hayo yanayosemwa na yatakayoendelea kusemwa, sisi tunajua kwa jinsi gani tuko vizuri, lakini hata ulimwengu unajua sisi tuko vizuri kiasi gani katika kuangalia haki za binadamu. Ila wanasema, ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya. Basi jamii yote itamzongea imuue,” amesema.

Amesema hakuna aliye juu ya sheria na kwamba yeyote anayevunja sheria atashughulikiwa. Amesisitiza kuwa, pamoja na wanaodai Tanzania inakiuka haki za binadamu, hakuna aliye juu ya sheria.

Mkuu huyo wa nchi amesisitiza kuwa mabadiliko ya sera za kiuchumi, matamko na mwelekeo wa kisiasa duniani vinaziweka nchi zinazoendelea katika hali ngumu ya ushindani na, pengine, kupigwa vita.

“Nilishamsikia mtu mmoja mkubwa tu wa nchi moja akisema, ‘Sisi, yeyote anayeendelea kimaendeleo kwa kasi, huyo ni adui yetu,’” amesema.

Ameeleza kuwa, kadiri nchi zinazoendelea zinavyosonga mbele kimaendeleo, wapo wanaozirudisha nyuma ili zisiende kwa kasi inayokusudiwa.

“Tunashuhudia mataifa yakihujumiana, tunashuhudia vijana kulaghaiwa na kumezeshwa sumu dhidi ya mataifa yao na kushawishiwa kuhujumu uchumi wao uliojengwa kwa nguvu kubwa,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Bavoo Anatoly Junus, kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), leo Julai 13, 2026. Picha na Ikulu.


Katika hali hiyo, amesema nchi inahitaji kujihami na kulinda raia wake katika nyanja zote, ikiwemo kiuchumi, na kwamba mawakili wa Serikali ni walinzi muhimu wenye ujuzi wa sheria za ndani na kimataifa.

Kwa hali iliyopo sasa, amesema lazima mawakili wawe na weledi kuhusu matamko na itifaki za kimataifa zinazotolewa ili ziangaliwe haraka, zitafsiriwe kwa kuzingatia hali ya nchi na kutoa majibu kwa wakati ili kuhami uhuru wa Taifa.

Amewaambia kuwa ni wajibu wao kugundua vihatarishi mapema, kushauri kwa wakati, kwa usahihi na kwa nia njema, na kuhakikisha nchi inalindwa na kusimamiwa katika misingi imara ya kisheria.

Hata sheria zinazotungwa, amesema, zinapaswa kusaidia kulinda uhuru, rasilimali za Taifa na haki za raia, kama ilivyoelezwa kwenye Katiba.

Amezielekeza taasisi zote za Serikali kujenga utaratibu wa kutambua vihatarishi vya kisheria mapema, ikiwemo katika mikataba, utawala wa ardhi, manunuzi, miradi ya maendeleo, ajira, mazingira, Tehama na hata huduma kwa wananchi.

Viongozi wa Serikali, mawakili na wageni mbalimbali wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha, Julai 13, 2026. Picha na Ikulu.

Aidha, ametoa rai kwa chama hicho kuwa chombo cha kujenga weledi, maadili, nidhamu, ubunifu na mustakabali wa sekta ya sheria nchini, ndani na hata nje ya Serikali.

“Nilipokuwa naandika hili nilikuwa najiuliza, hivi kuna misingi ya maadili na utendaji ya taaluma ya sheria? Nikaingia kwenye Google nikakuta ipo,” amesema.

Amesema miongoni mwa misingi hiyo ni kusimamia haki, kutoa maoni bila kuegemea upande wowote, uadilifu, uhuru, usiri na kuzuia matumizi mabaya ya makubaliano ya usuluhishi wa kesi za kiraia.

Amesema chama hicho hakipaswi kuwa chanzo cha migogoro na mifarakano katika Taifa, akisisitiza kuwa wasikubali taaluma hiyo itumike kuhalalisha jambo lenye nia ovu dhidi ya Taifa.

Samia amesema ulimwengu unatumia kila nguvu kutimiza matakwa yake.

“Niwaombe sana ndugu zangu, sisi ni Watanzania, Tanzania ni yetu; si ya mtu mwingine. Ikiendelea na ikiwa vizuri, ni yetu; tukiivuruga na ikaharibika, ni yetu. Tutasaidiwa kuiharibu, lakini hatutasaidiwa kuijenga tena,” amesema.


Sikuwahi kusaini adhabu ya kifo

Katika hotuba yake hiyo, amesema tangu alipoingia madarakani hajawahi kutia saini ya kuruhusu mtuhumiwa aliyehukumiwa adhabu ya kifo kunyongwa.

Kifungu cha 325(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kinampa Rais wa nchi mamlaka ya kuruhusu utekelezaji wa adhabu ya kifo.

Kifungu hicho kinasema: “Rais atatoa hati ya utekelezaji wa adhabu ya kifo (death warrant), au amri ya kubadilisha adhabu hiyo, au msamaha, kwa sahihi yake na muhuri wa Jamhuri ya Muungano ili kutekeleza uamuzi huo.”

Hata hivyo, adhabu hiyo haijawahi kutekelezwa tangu mwaka 1994 kutokana na wakuu wa nchi kutotia saini hati ya utekelezaji wa adhabu ya kifo. Mkuu wa nchi wa mwisho kusaini hati hiyo alikuwa Ali Hassan Mwinyi.

“Kalamu yangu mimi hatari yake ni kusaini mtu anyongwe, na sijawahi kufanya hivyo. Baada ya ninyi kupeleleza, kupeleka kesi na kuisimamia, hakimu akaamua akahukumiwa kunyongwa, Rais asaini anyongwe, sijawahi kufanya,” amesema Rais Samia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera, amesema katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, watashirikiana na wadau kuhakikisha sheria zinazohitaji maboresho zinaboreshwa.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, amesema chama bora cha kitaaluma ni kile kinachoisaidia Serikali kufikia malengo yake, si kukiitikisa wala kukiyumbisha.

Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Bavoo Anatory, amesema Serikali imeokoa Sh969.3 bilioni na Sh1.9 trilioni kutokana na ushindi uliopatikana katika mashauri mbalimbali.

Kati ya mashauri hayo, amesema mashauri 565 ya madai ndani na nje ya nchi pamoja na mashauri 18 ya usuluhishi yalihitimishwa kwa majadiliano nje ya mahakama.

Pia, amesema Serikali imetaifisha mali mbalimbali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu au zilizotumika kutenda uhalifu, ikiwemo fedha taslimu Sh2.9 bilioni.

“Pia, Dola 903,875 za Marekani, hati fungani tatu zilizopo Benki Kuu ya Tanzania zenye thamani ya Sh490 milioni, nyumba na viwanja 46, magari 64, dhahabu na vipande vidogo vyenye uzito wa gramu 103,807.58 na meno manne ya tembo,” amesema.