Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya Serikali kilichotokea Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imetoa rai kwa wananchi waishio mataifa ya nje kuhakikisha wanafuata sheria zote za kuishi katika mataifa ya nje ili kuipunguzia Serikali mzigo.

Dodoma. Serikali imesema hakuna Mtanzania aliyeathirika nchini Afrika Kusini kutokana na hali ya sasa ya nchi hiyo, huku ikifafanua kuwa video zilizozua taharuki kwenye mitandao ya kijamii ni za zamani na si matukio ya hivi karibuni.

Hayo yameelezwa bungeni leo Jumanne Mei 26, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi aliyeomba ufafanuzi kuhusu hali ya Watanzania wanaoishi Afrika Kusini.

Shangazi ametaka Serikali itoe taarifa rasmi kuhusu usalama wa Watanzania waliopo nchini humo kufuatia taarifa zinazosambaa mitandaoni zinazodai kuwepo kwa hali ya taharuki.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Kombo amesema ubalozi wa Tanzania uliopo Pretoria umefuatilia suala hilo na kubaini kuwa hakuna Mtanzania mwenye kibali cha kazi aliyeathirika.

“Kwa upande wetu Tanzania, walioathirika zaidi ni raia wa Malawi na Zimbabwe ambao wengi hawana vitambulisho halali vya kufanya kazi,” amesema Kombo.

Ameongeza kuwa video zilizokuwa zikisambaa na kusababisha hofu mitandaoni ni za zamani, si za sasa, na zilishughulikiwa kwa mawasiliano kati ya ubalozi na Serikali ya Afrika Kusini.

“Baada ya zile klipu kusambaa tulimwagiza balozi atoe tamko maalum na alifanya mawasiliano na Serikali ya Afrika Kusini na kuthibitisha hakuna Mtanzania aliyeathirika,” amefafanua.

Waziri huyo pia ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya kazi na ukaazi ili kuepuka changamoto na kuirahisishia Serikali kazi ya ufuatiliaji pindi panapotokea hali za kiusalama.

Matukio ya mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni wanaotoka mataifa mbalimbali yalishika kasi Afrika Kusini ambapo picha na video zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonesha makundi ya watu wanaopinga wahamiaji wakiwashambulia kwa vipigo na kuibua mjadala.

Hata hivyo, Serikali ya Afrika Kusini iliahidi kufanya msako dhidi ya wanaohusika na matukio hayo ya mashambulizi ya chuki kwa raia wa kigeni.