Kaya 13 zanufaika na mradi bomba la mafuta Kiteto

Muktasari:

  • Kaya 13 wilayani Kiteto mkoani Manyara, zimenufaika kwa kujengewa nyumba za kuishi kupitia mradi wa bomba la mafuta ambao utajengwa kutoka Hoima Uganda kupitia Kiteto hadi Tanga.



Kiteto. Kaya 13 wilayani Kiteto mkoani Manyara, zimejengewa nyumba za kuishi na familia zao kupitia mradi wa bomba la mafuta ambao utajengwa kutokea Hoima Uganda kupitia Kiteto hadi Tanga.

 Wakizungumza kwa furaha, leo Jumatatu Novemba 13, 2023 baada ya kukabidhiwa nyumba hizo zilizojengwa eneo la Olengasho Kijiji cha Kimana wilayani Kiteto, baadhi ya wananchi hao wanasema wangetumia miaka 30 kujenga nyumba hizo kutokana na aina ya maisha wanayoishi.

"Nyumba kama hii ningetumia miaka 30 kuijenga kutokana na aina ya maisha ninayoishi mimi... Hapa kilimo natumia kama njia kuu ya uchumi na sijafanikiwa, leo hii nimekabidhiwa nyumba na bomba la mafuta pamoja na mkuu wa wilaya kwa kweli nashukuru sana," amesema Dinya.

Halima Juma amesema kilimo anacholima kama njia ya kujikimu kimaisha hajawahi kufikiri kuwa na ujenzi wa nyumba hiyo na kushukuru mradi huo wa bomba la mafuta kupitia katika eneo lake na kumpa fidia kwa kumjengea nyumba hiyo

"Nashukuru mradi wa bomba la mafuta pamoja na viongozi wa Serikali ambao sasa wamenifanya kuishi katika mazingira bora mimi na familia yangu…kilimo ninacholima ni kidogo sikuwa na uhakika wa kupata nyumba kama hii," amesema Halima Juma.

Akizungumzia namna walivyofanikisha ujenzi wa nyumba hizo 13 Kiteto, Mhandisi Edler Maro kutoka katika mradi huo anasema wameshirikisha wananchi walioguswa kikamilifu.

"Hizi nyumba ni kwa ajili ya waguswa ambao nyumba zao zimepitiwa na bomba... ujenzi wa nyumba hizi unatokana na eneo la nyumba yake awali kuna ujenzi wa nyumba A, B, C, na D. Pia ujenzi wa nyumba hizo umehusisha makandarasi watatu," amesema Maro.


Mkuu wa Wilaya ya Kiteto akikabidhi wananchi hao 13 nyumba hizo, Mbaraka Batenga amesema hana malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi hao tofauti na miradi mingine

"Kwa bomba la mafuta hapa Kiteto sina malalamiko kwa jinsi hivyo naamini wananchi wote wameshirikishwa kikamilifu na wameridhika kama walengwa wa mradi," amesema DC Batenga.

Amesema maeneo mengine yamekuwa na malalamiko ambayo yanagharimu wananchi muda na fedha kufuatilia haki zao lakini imekuwa tofauti kwa mradi huu wa bomba la mafuta na kuwaasa wananchi hao nyumba hizo walizojengewa isiwe chanzo cha migogoro ya kifamilia.

"Pasitokee ugomvi wa wamilia kugombea nyumba hizi nitashangaa sana kusikia…Tumieni fursa hii kufanya sasa shughuli za maendeleo kikamilifu kwa kuwa sasa mna uhakika wa maisha," amesema DC Batenga.