Suala la waliopata ulemavu vita ya Kagera laibukia bungeni

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameomba Serikali kuwatazama wapiganaji ambao hawakupata ajira baada ya vita kwa kuwa ni wachache ione namna inavyoweza kuwasaidia kwa chochote nao wakafurahi.

Dodoma. Serikali imesema Tanzania ina wapiganaji 272 ambao wanalipwa pensheni ya ulemavu waliupata wakati wakiitetea nchi baada ya uvamizi wa Nduli Adi Amin Dada.

Mbali na malipo hayo, wazee wenye ulemavu ambao waliupata katika vita hiyo, wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za jeshi na kwamba malipo ya pensheni za ulemavu yapo kwa mujibu wa kanuni za Pensheni na Viinua Mgongo za mwaka 1966.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Novemba 9, 2023 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fakharia Shomar Khamis ambaye ameuliza Serikali inatoa kauli gani kuhusu kuwasaidia wazee waliopata ulemavu wakati wa kupigana Vita ya Kagera mwaka 1979.

Kwenye swali la nyongeza Mbunge huyo ameuliza ni kwa nini Serikali isiwachukue baadhi ya wazee ambao hawana familia ili kuwaweka eneo moja na kuwatunza na akaomba ikibidi walipwe pesheni kama wastaafu wengine.

Naibu Waziri amesema wazee waliokosa kabisa malezi ya familia wawasiliane na halmashauri zao ili waweze kuona namna ya kuwatunza ingawa ameeleza kuwa serikali inapendekeza watunzwe na vijana na watu wa familia.

Ameomba wazee ambao hawako kwenye orodha hiyo wawasiliane na vikosi vya Jeshi la Ulinzi vilivyopo karibu na maeneo yao ili wasaidie namna bora ikiwemo kuingizwa kwenye mfumo kama wengine.

Kuhusu ajira kwa wapiganaji hao, amesema wengi kati ya wapiganaji hao walipewa ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama hususani Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza ingawa wapo walioshindwa kuajiriwa kutokana na sababu mbalimbali.

Sagini amesema wizara inaendelea kufuatilia hali halisi za wazee waliopigana vita ili kuchukua hatua stahiki na kuhusu fidia kama wanavyolipwa watumishi wastaafu amesema ni suala kisera ambalo linapaswa kutazamwa upya.

Kwa upande mwingine Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amemwomba Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupeleka pendekezo kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili aone namna bora ya kuwasaidia wapiganaji wa Vita ya Uganda ambao hawakupata ajira lakini bado wako hai kwa kuwa ni wachache angalau wafikiriwe kwa chochote.