Kaya 7,800 kufikiwa utoaji maoni Dira ya Maendeleo

Mwenyekiti wa Dira ya Taifa,  Profesa Lucian Msambichaka akizungungumza kuhusu  mchakato wa maandalizi ya utoaji maoni wa dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Muktasari:

  • Kila kaya itawakilishwa na mwanakaya mmoja mwenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya 2050.

Unguja. Kaya 7,800 zikitarajiwa kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, mamlaka husika zimeshauriwa kuhakikisha zinafanya uchaguzi sahihi ili watakaoshiriki wasiegemee upande mmoja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi Kisiwani Unguja wamesema uzoefu unaonyesha wanapokuwa na utaratibu wa kuchukua maoni walengwa wakuu husahaulika.

“Huu ni utaratibu mzuri kuwaangalia wananchi lakini ni vyema kuwa na namna ya kuratibu watakaohusika wasichaguliwe kwa matakwa ya watu binafsi,” amesema Hassan Haroun, mkazi wa Tomondo.

Kamishna Mipango ya Kitaifa kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Mohamed Masoud Ali amesema dira bila kugusa wananchi haitaweza kusimama imara.

Amesema kila kaya itawakilishwa na mwanakaya mmoja mwenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea.

“Ili kuhakikisha dira inakuwa na tija na kuleta mabadiliko kwenye jamii, lazima iangazie matakwa na mahitaji ya wananchi wenyewe kwani hicho ndiyo kipaumbele chake na si vinginevyo,” amesema.

Mohamed amesema wanapaswa pia kuwashirikisha wadau ili kupata maoni ya kimkakati kufikia lengo kamili.

Amesema kabla ya kuanza mchakato wa maandalizi hayo ni muhimu kutathmini dira iliyopita kwa kujifunza na kuyaendeleza yanayoonekana kuwa muhimu.

Kamishna huyo amesema jumla ya kaya 7,800 zinatarajiwa kufanyiwa mahojiano ya ana kwa ana.

Mwenyekiti wa Timu ya kuandaa Dira ya Taifa, Profesa Lucian Msambichaka amesema maendeleo hayaendeshwi na mtu mmoja wala watu wa ngazi za juu, badala yake watu wa chini ndio waendeshaji wakubwa wa maendeleo nchini.

Kutokana na umuhimu huo, amesema elimu inahitajika zaidi akieleza ikiwa watu hao hawaelewi kitu wataitikia na hawataweza kufanya kile kinachotakiwa, hivyo hao ndio wanaopaswa kumiliki mawazo kamili ya dira.

“Lazima wananchi wenyewe wasema mwaka 2050 wanataka kuwa wapi, sisi tunapokea maoni na kuyachakata kuyaweka katika utaratibu mzuri,” amesema.

Amewataka vijana kuwa sehemu ya maoni maana wao ndio wenye maono makubwa.

“Tunaelewa kuwa uchumi na maendeleo ya nchi yanaendeshwa na vijana, hivyo lazima wachangie,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Othman Maulid alisema dira itasaidia kuimarisha miundombinu ya utalii, kurahisisha kuvutia wageni na wawekezaji.

“Kila jambo lazima liwe na dira ya kukupa mwelekeo wapi unapoelekea, nasi tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa na wanatoa maoni ya kile wanachokitaka," amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed amewataka viongozi kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalamu kuhakikisha wananchi wanaeleza wanayoyataka kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi.

Waziri Masoud amesema ushiriki wa viongozi hao kwa upande wa Zanzibar ni wa kipekee kuhakikisha mchakato huo unawafikia wananchi ili timu ya uandishi iwe na uwanja mpana wa kukusanya, kuchambua na kuandaa dira itakayoakisi matakwa ya jamii.

"Imani yangu kuwa kupitia umahiri na utendaji wenu zoezi la uhamasishaji wa umma na ukusanyaji maoni ya wananchi na wadau wa dira hiyo utatekelezwa kwa mafanikio makubwa," amesema.

Mchakato wa maandalizi ya dira ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 9, 2023 katika mkutano mkuu wa kwanza wa kitaifa uliofanyika jijini Dodoma.

Ukusanyaji wa maoni kwa wananchi katika ngazi ya mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa, utahusisha mbinu na njia ya mahojiano maalumu na kujaza dodoso kwa njia ya mtandao.