Kelele janga jipya mitaani

Muktasari:
- Wakati Taifa likihitaji msaada mkubwa wa huduma za kiroho kwa ajili ya kuponya maradhi ya wananchi yanayosababisha kujikita katika matukio kama ya uhalifu, mauaji na mengineyo, huduma hizo katika baadhi ya maeneo zimegeuka kuwa adha kubwa kwa wakazi.
Dar/Mikoani. Wakati Taifa likihitaji msaada mkubwa wa huduma za kiroho kwa ajili ya kuponya maradhi ya wananchi yanayosababisha kujikita katika matukio kama ya uhalifu, mauaji na mengineyo, huduma hizo katika baadhi ya maeneo zimegeuka kuwa adha kubwa kwa wakazi.
Baadhi ya nyumba za ibada ambazo kimsingi zinahitajika kwa ajili ya huduma za kiroho kwa Watanzania, zimeamua kukiuka sheria za nchi na kuwa chanzo cha kelele kufuatia matumizi makubwa ya vyombo vinavyotoa sauti.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwapo kwa makanisa ambayo mengi ni yale ya uamsho, yakitumia ‘flash’ zenye mahubiri na nyimbo, na kuzichezesha kwa sauti kubwa kuanzia asubuhi hadi usiku hata katika mazingira ambayo hakuna waumini kanisani.
Vivyo hivyo kwa baadhi ya misikiti, inayolalamikiwa kwa kutoa mahubiri kuhamasisha waumini kuamka kwa ajili ya swala ya alfajiri.
Usajili wa makanisa unasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya sheria ya Society Act ya 2002 na maboresho yake ya mwaka 2019.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa dini na wananchi, wanadai hali hiyo inachangiwa na ulegevu wa usimamizi wa sheria za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na halmashauri za miji, manispaa na majiji nchini.
Uchunguzi unaonyesha baadhi ya nyumba za ibada zipo karibu kabisa na shule za watoto wadogo na NEMC inasema huo ni uvunjifu wa sheria na kwamba kama ni eneo la makazi, haipaswi kujenga nyumba ya ibada kwenye eneo la makazi mpaka matumizi ya ardhi yabadilishwe.
Kanuni ya Udhibiti wa Sauti na Mitetemo ya NEMC ya mwaka 2015 inatoa maelekezo ya viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika makazi ni inatakiwa isizidi decibels 35, lakini kwenye makazi na biashara ni decibels 45 kuanzia saa 6 mchana.
Pamoja na kanuni hiyo, lakini imebainika kuwa kelele hupigwa hadi kufikia kati ya decibels 78 hadi 100 na kuleta adha na usumbufu kwa majirani.
Alipoulizwa kuhusu kero hiyo juzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema kwa kifupi; “Ni kweli juu ya hilo. Nimewaagiza wataalamu wangu wa NEMC kuanza kulifanyia kazi.”
Mkurugenzi mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alisema kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoa onyo kwa wanaozalisha kelele hizo na wengine wamekuwa wakipigwa faini, kuchukuliwa vyombo na kufunguliwa mashitaka.
Ingawa Dk Gwamaka hakuingia kwa undani, lakini miezi mitatu iliyopita alikaririwa akisema NEMC imepata ongezeko kubwa la malalamiko dhidi ya kelele kutoka nyumba za ibada, nyumba za starehe na baa akisema kelele zimevuka viwango.
Mkurugenzi huyo mkuu alisema kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita wamekuwa wakielimisha jamii na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, watendaji wa kata na hata wamiliki wa nyumba za starehe, lakini bado hali ni mbaya.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kati ya saa 12 jioni mpaka saa 4 usiku kuna viwango vya kelele ambavyo vinapaswa kuzingatiwa na vivyo hivyo kuanzia saa 4 mpaka asubuhi viwango vyake ni vya chini na vipo kisheria na havipaswi kuvuka.
Dk Gwamaka alisema kelele hizo zinawasababishia wananchi wanaoishi jirani, kupata athari za kiafya na athari za kisaikolojia na kanuni ya kelele na mitetemo ya 2004 inawalinda wananchi hao.
“Haipendezi sisi kama NEMC kuanza kuadhibu viongozi wa dini, kwenda kuadhibu watu wanastarehesha watu. Ni vizuri wote tukazingatia sheria na kila mwananchi akawa na uhuru wake kikatiba ili Taifa letu liweze kuwa na amani,’’ alisema.
Hali ilivyo Dar es Salaam
Katika Jiji la Dar es Salaam, hali ni mbaya kutokana na baadhi ya nyumba za ibada kukithiri kwa kelele za muziki mkubwa, vigelegele, na kelele hizo husikika kuanzia asubuhi hadi jioni na wakati mwingine hudumu usiku kucha.
Agosti 2021, akiwa katika ziara yake ya kupokea kero mbalimbali kwa wananchi wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla alipokea malalamiko hasa kwa wananchi wa Kinondoni, kuhusu suala la kelele wakidai limekuwa sugu.
Kutokana na hali hiyo, akiwa katika viwanja vya Tanganyika Packers, Makalla, aliagiza watendaji wa mitaa mbalimbali pamoja na watu wa mazingira, kudhibiti changamoto hiyo, akisema Kinondoni ndio inaongoza kwa kelele japo alitoa mfano wa baa zikiwa zinaongoza kwa kupiga kelele.
Anna Nnkinda, mkazi wa jijini Dar es Salaam alishangaa kukuta kanisa limeanzishwa jirani na nyumba ya bibi mmoja huko Mbagala Zakhem.
“Kuna bibi alikuwa anakaa Mbagala Zakhem sasa hivi ni marehemu, siku moja nilienda kwake kumsalimia anapokaa kuna kanisa limefunguliwa linapiga muziki muda wote. Nakumbuka alipata presha kwa sababu ya zile kelele,”alisema.
Kilimanjaro ni shida
Katika eneo lenye ukubwa wa kilometa moja ya mraba la KDC Kiborloni Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kuna makanisa zaidi ya 10, huku baadhi yakiwa yamefunga spika zenye sauti kubwa na kuwa kero kwa wananchi.
John Bennett anayemiliki mgahawa wa The Golden Shower, alisema katika eneo hilo amezungukwa na makanisa matano kila upande, na baadhi yamefunga vifaa vya muziki ambavyo vikifunguliwa hakuna kusikilizana hadi usiku.
“Kuna kipindi tulilalamika kwa Waziri Makamba (Januari) akiwa Waziri wa Mazingira na alitupa msaada sana, maana alituma watu wa NEMC na walithibitisha hili na haya makanisa yakapunguza sauti mwezi mmoja tu yakarudia,” alisema.
Hali ikiwa hivyo katika wilaya ya Moshi, ndivyo ilivyo katika wilaya ya Hai ambapo wananchi wa kata ya Muungano, wamelalamikia uwepo wa utitiri makanisa katika kata hiyo na baadhi yameweka spika zenye kelele kupitiliza.
Hellen Mushi ambaye ni mkazi wa eneo la Shabaha, alisema katika mtaa huo, kuna makanisa zaidi ya 10 ambayo kila kanisa linafunga spika kubwa na kuhubiri kwa sauti hatua inayosababisha usumbufu kwenye makazi ya watu.
Alichokisema Askofu Shoo
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alipoulizwa ana maoni gani juu ya hilo, alisema Serikali inahitaji kuweka sheria, taratibu na kuzisimamia kuhusu nyumba zinazostahili kuwa nyumba za ibada.
“Wengi wanaotoa hayo mafundisho ukiwatazama kwa jicho la rohoni, hawana nia njema ya kuhubiri injili ya kweli ya Kristo wala watu wapate ukombozi wa kweli wa kiroho na kifikra, bali wao wanaongozwa na tamaa za madaraka na fedha,” alisema.
Akizungumzia kero hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin alikiri kuwapo kwa malalamiko mengi ya makanisa na baa kuanzishwa katikati ya makazi ya watu ambazo zinapiga muziki kwa sauti kubwa na kuwa kero kwa majirani.
“Nimemwelekeza DC (mkuu wa wilaya) wa Moshi apitie maeneo yote ambayo hayastahiki kufanyia mambo niliyoyataja wafuate kanuni na taratibu,” alisema RC Babu
Kanda ya Ziwa
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa walirusha lawama kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo kupitia Msajili wa Vyama vya Kijamii husajili makanisa.
“Mtaa wa Nyaruhama ninakoishi, kuna makanisa matatu likiwamo la Anglikana ambalo hatuna tatizo nalo kwa sababu ibada zao hufanyika kwa utulivu bila vipaza sauti,” alisema Naomi Masanja.
Kero ya kelele kutoka kwenye nyumba za ibada zilizoko katikatikati ya makazi, pia ilishuhudiwa mkoani Mara, ambapo Neema John, mkazi wa Bweri Manispaa ya Musoma alisema mtaa huo una makanisa zaidi ya matatu yanayotumia spika.
“Kipindi cha nyuma, ibada zote zilikuwa zinafanyika mchana na usiku huku kila kanisa likitumia vyombo vya muziki vinavyofunguliwa kwa sauti ya juu; tunashukuru hivi sasa wanafanya ibada siku za Jumapili pekee,” alisema Neema.
Arusha, Morogoro, Tanga
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa majiji ya Arusha na Tanga walitaka uwepo wa udhibiti wa kelele zinazozalishwa na baadhi ya makanisa.
Mchungaji Joel Nnko alisema ni muhimu kuwepo na udhibiti wa nyumba za ibada, kwani kila jambo linapaswa kuwa na utaratibu wake akisema tatizo analiona lipo kwa wanaosimamia sheria na taratibu za uanzishaji wa makanisa nchini.
“Mimi naona shida ipo kwa wanaosimamia sheria kwa sababu siku hizi kiongozi wa dini akigombana na mwenzake tu utasikia na yeye ameanzisha kanisa lake sasa haya mambo sio vizuri,”alisema Mchungaji Nnko.
Hata hivyo, Mchungaji wa kanisa la Assemblies of God lililopo eneo la Madizini Manispaa ya Morogoro, Stephen Msigala, alisema kuanzishwa kwa makanisa kwenye makazi ya watu sio usumbufu bali ni kusogeza karibu huduma za kiroho.
Mchungaji Msigala alisema kwa kiasi kikubwa makanisa hayo yamesaidia kufikisha huduma za kiroho kwa wananchi na pia yamesaidia tabia na mienendo ya wanadamu ambayo imekatazwa na Mungu na sheria za nchi.
Jijini Tanga, Sheikh wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Tanga, Sheikh Juma Luwuchu alisema wanaojadili kelele hizo wasichanganye na mawaidha, adhana na hotuba ya Ijumaa kwani kwao ni sehemu ya ibada.
Meya wa Jiji la Tanga, Abdurahman Shiloow, alisema tatizo la kuibuka kwa nyumba za ibada kwa jiji hilo siyo kubwa kama ilivyo kwa miji mingine, lakini tahadhari imewekwa ya kudhibiti kelele katika shughuli za harusi na vigodoro.
Mbeya, Iringa hali si shwari
Mbeya, mkoa ambao unatajwa kuwa na makanisa mengi zaidi nchini, wananchi wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kutotoa usajili holela wa makanisa ili kupunguza utitiri usiofuata utaratibu wa nyumba za ibada wakati wa kusifu na kuabudu hususan nyakati za usiku katika maeneo yasiyo rasmi.
Stella Amos, mkazi wa Mabatini alisema ifike wakati sasa Serikali kabla ya kutoa vibali, kufanyike utafiti wa maeneo ambayo yameelezwa kuombwa vibali vya kuendeshea ibada na hata kumbi za starehe.
‘’Ibada za usiku kwenye makazi ya watu zimekuwa ni changamoto. Ufike wakati Serikali ifanye utafiti wa maeneo ya makanisa mapya na kumbi za starehe ili kuwaondoa wananchi na adha hiyo,” alisema Stella.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua alipohojiwa kuhusiana na idadi ya makanisa kwa Jiji la Mbeya na wilaya yake, alisema kwa sasa hawezi kuwa na takwimu sahihi.
Kinachoendelea Mbeya ni sawa na mkoa jirani wa Songwe ambapo wakazi wa maeneo ya mjini wameiomba Serikali kuyataka madhehebu ya dini kuwa na vifaa vya kudhibiti sauti ili kuondoa usumbufu kwa kuwapigia kelele wengine.
Essay Kayange, mkazi wa Mlowo alisema mara nyingi na hasa nyakati za usiku baadhi ya makanisa yamekuwa yakiendelea na ratiba zao za ibada, huku yakisababisha kelele zinazotokana na kufungulia kwa sauti ya juu ya muziki na kusababisha wakazi kushindwa kupumzika vizuri.
“Hali ya kuendesha maombi usiku huku wakitumia vyombo vinavyotoa sauti, inaleta usumbufu kwa wengine wanaohitaji kupumzika ili kupata nguvu na afya njema,” alisema Kayange.
Mkoani Iringa nako ni kama maeneo mengine, ambapo mkazi wa Frelimo, Prisca Ndelwa, alisema changamoto na ugumu wa maisha vimekuwa sababu ya watu wengi kuhama makanisa na ndio maana mengi yanafunguliwa.
“Kila likifunguliwa linapata wadau kwa sababu watu wanahitaji faraja na tumaini kutokana na ugumu wa maisha,” alisema
Mchungaji wa Kanisa la Kings, Mjini Iringa Leonard Matei alisema sio tu makanisa yanayosababisha kelele.
“Mbona kuna baa zinapiga mziki na nyingine zinakesha, hamjawahi kusikia kelele? ni makanisa peke yake? alihoji.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mchungaji wa Kanisa la Upendo na Uzima lililopo jijini Dodoma, Yohana Hanga aliyesema hakuna kelele mbaya kama watu wanamhubiri na kumtaja Yesu Kristo kwa ajili ya kuwavuta na kuwasaidia watu.
Hanga alisema sheria ya kutaka watu wasipige kelele haiwagusi watu wote ikiwemo wahubiri, bali inatazama kelele zisizokuwa na msingi kama klabu za pombe na kumbi za burudani.
Misikiti nayo yatajwa
Katika baadhi ya maeneo nchini, baadhi ya misikiti hutumia vipaza sauti nyakati za alfajiri kwa ajili ya kuhamasisha waumini kuamka kwa ajili ya Swala ya Alfajiri.
Ubaidillah Bakari, muumini wa dini ya Kiislama anayeishi jijini Dar es Salaam, alisema katika dini hiyo hakuna mafundisho yanayowataka watu waamshwe kwa kutumia vipaza sauti.
‘‘ Ninachojua mwongozo wetu unatutaka tuite watu kuswali na sio alfajiri pekee bali kwa swala zote kupitia wito ambao sisi tunauita kwa jina la adhana. Sasa ukiangalia, adhana kwa kawaida haichukui hata dakika tano, hivyo haiwezi kuwa kero,’’ alisema.
Aliongeza: ‘‘ Vinginevyo kukiwa na watu wanaotumia vipaza sauti kuita watu nje ya adhana, huo sio mwenendo wetu sahihi, kwani hata swala yenyewe tumeelekezwa kuifanya kwa sauti ya chini kadri inavyowezekana.’’
Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Fina Lyimo (Moshi), Baraka Loshilaa na Bakari Kiango (Dar es Salaam), Mussa Juma (Arusha), Hamida Sharif (Morogoro), Saada Amir (Mwanza), Beldina Nyakeke (Musoma) na Burhan Yakub (Tanga), Hawa Mathias (Mbeya), Stephano Simbeye (Songwe), Habeli Chidawali (Dodoma).