Kenya na ulimwengu wao wa siasa nje ya kilichozoeleka Afrika
Mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga akiwa na mgombea mwenza, Martha Karua wakiangalia nyaraka baada ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya urais yaliyompa ushindi William Ruto. Picha na maktaba
Muktasari:
- Taswira ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022 imeifanya nchi hiyo kuwa tofauti ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika, hasa kwa namna siasa zilivyofanywa na zinavyoendelea kufanywa kwa namna ya kipekee.
Taswira ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022 imeifanya nchi hiyo kuwa tofauti ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika, hasa kwa namna siasa zilivyofanywa na zinavyoendelea kufanywa kwa namna ya kipekee.
Tofauti ya kwanza ni pale Rais aliyepo madarakani, Uhuru Kenyatta alipopishana mitazamo na Naibu Rais wake ambaye baadaye alikuwa mgombea wa urais, William Ruto lakini bado huduma zote za kiserikali, ikiwemo ulinzi, malazi na malipo Ruto aliendelea kupatiwa.
Pengine jambo hili linaipa Kenya sura tofauti kwenye siasa ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika ambapo ikitokea kiongozi au kiongozi mstaafu amehama kutoka chama tawala mara nyingi baadhi ya huduma anasitishiwa, kinyume na utaratibu.
Wakati bado ni Naibu Rais wa Kenya, Ruto alikuwa mstari wa mbele kupinga mchakato wa mabadiliko ya katiba, maarufu kama BBI uliokuwa unapendekeza kuongezwa kwa baadhi ya nafasi serikalini, ikiwemo ya Waziri Mkuu, japokuwa mchakato huo ulikuwa unapigiwa chapuo na Rais Uhuru Kenyatta.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alitafsiri vitendo hivyo vya Naibu wake kama harakati za kuutaka urais, huku akimhakikishia hatopata, kwani Wakenya watachagua mtu atakayewaletea maendeleo na sio ufisadi.
“Ni juu yako kuamua ikiwa unataka kwenda kwenye nyumba iliyojaa wezi na waongo kwa sababu ya maneno matamu na senti chache au nyumba ya haki ambayo itahakikisha haki kwa wote na mustakabali mzuri kwa watoto wetu,” alisema Rais Kenyatta akiwa kwenye ziara ya kikazi katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a.
Jambo la pili linaloitofautisha nchi hiyo kwenye ulimwengu wa siasa ni pale ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya iligawanyika kutokana na kutofautiana kimtazamo kati ya Mwenyekiti wake, Wafula Chebukati na Makamu Mwenyekiti Juliana Cherera, lakini bado kila upande unatoa matamko na wamebaki na vyeo vyao.
Si rahisi kwa nchi nyingi za Afrika kuendelea kubaki na cheo chako kwenye Tume ya Uchaguzi endapo utapishana kauli na mkuu wako, kitu ambacho kwa Kenya wameonyesha tofauti, huku sababu za kugombana kwao ni madai ya Juliana Cherera na makamishna wengine watatu wa IEBC kumtuhumu mwenyekiti Chebukati kupanga matokeo yake bila kuwashirikisha.
Hata hivyo, kwa upande wa Chebukati ameendelea kushikilia msimamo wake wa kuwa matokeo hayo ni ya haki na mchakato wote wa uchaguzi ulifuatwa vizuri, huku na yeye akiwashutumu baadhi ya viongozi wa juu wa usalama wa serikali na viongozi wa Azimio la Umoja kumrubuni atangaze matokeo tofauti na uhalisia.
Hata hivyo, tuhuma hizo ambazo Chebukati amezitoa zimepingwa vikali na Mkurugenzi mtendaji wa Azimio la Umoja, Raphael Tuju aliyesema:
“Nilipata taarifa za kijasusi kutoka kwa ofisa mmoja wa IEBC kuwa baadhi ya fomu 34A zilikuwa zinabadilishwa na nilijaribu kumtafuta mwenyekiti lakini aliwaita polisi kunizuia kukutana naye,” alisema Tuju, ambaye baadaye alikiri kukutana na Chebukati kwenye makazi yake Kareni kwa maongezi ya kawaida
Licha ya tuhuma hizo ambazo zinaendelea kurindima nchini Kenya zikiwahusisha vigogo wa IEBC, bado uchaguzi mdogo wa kaunti ya Kakamega pamoja na Mombasa na baadhi ya majimbo mengine manne umesimamiwa na tume hiyo chini ya Mwenyekiti Wafula Chebukati, japokuwa kambi ya Raila Odinga ikionyesha kutoridhishwa na usimamizi huo.
“Wafula Chebukati aliwafanyia vitendo visivyo vya kiungwana makamishna wake waliokataa kusimama upande usio wa kweli, alipewa rushwa. Inatakiwa ajitoe kusimamia uchaguzi wa hapa Mombasa kwa sababu amekosa sifa na imani ya watu,” Raila alimtuhumu Chebukati wakati akimnadi mgombea ugavana wa Mombasa kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Abdulswamad Nassir.
Wakati hayo yakiendelea, utofauti mwingine wa siasa za nchi hiyo iliyopata Uhuru mwaka 1962 ni pale ambapo kwa mara ya kwanza Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajitoa kusimamia kesi inayomhusisha mtu wa serikali.
Turudi nyuma kidogo baada ya Chebukati kumtangaza Ruto ambaye pia ni Naibu Rais kuwa mshindi, timu ya Azimio la Umoja ikiongozwa na Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua ilipeleka mahakamani kesi ya kupinga ushindi huo.
Kiutaratibu Mwanasheria Mkuu wa serikali alitakiwa kusimama na Ruto ambaye ni Naibu Rais na kuutetea ushindi wake, kitu ambacho kilishawahi kufanywa na aliyekuwa kwenye nafasi hiyo mwaka 2017, Profesa Githu Muigai ambaye kwa kipindi hicho alimtetea Rais Uhuru Kenyatta. Hali imekuwa tofauti kwa Mwanasheria mkuu wa sasa wa serikali, Paul Kariuki aliyesema hatapinga kesi yoyote inayohusu ushindi wa Ruto.
Huku pilikapilika za Uchaguzi zikichukua sura mpya kila kukicha, Jukwaa la Majaji na Wanasheria Afrika limetuma jopo la majaji nchini Kenya kwenda kutazama jinsi kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Kenya zitakavyokuwa.
Jopo hilo limewasili nchini humo Agosti 29, 2022 likiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman huku majaji wengine waliombatana naye ni pamoja na: Lilian Tibatemwa-Ekirikubinza kutoka Mahakama ya Juu ya Uganda, Ivy Kamanga kutoka Mahakama ya juu ya Rufaa ya Malawi, Moses Chinhengo kutoka mahakama ya juu ya rufaa ya Lesotho na Rais wa mahakama ya uchaguzi ya Afrika Kusini, Henry Mbha.
Jambo lingine la kitofauti kwenye siasa za Kenya, mahakama ya juu ya nchi hiyo imetoa ruhusa kwa jopo hilo la majaji mashuhuri wa Afrika kuchukua nakala zinazohusiana na kesi hizo kulingana na sheria za kimataifa za haki za binadamu na usawa.
Kwa aina hiyo ya siasa ambayo Kenya imetuonyesha kwenye Uchaguzi Mkuu wake huu, tunaweza kusema kuwa ulimwengu wa siasa wa Kenya ni tofauti na wa nchi nyingi za Afrika ambazo siasa zake ni sawasawa na hesabu ya darasa la kwanza ya moja kuongeza moja na jibu lazima litakuwa mbili (siasa za kukariri na kuiga), hongereni Kenya, endeleeni kutuonyesha aina yenu ya siasa yenye utofauti ndani yake.