Kesi dhidi ya Chavda kuanza kusikilizwa Mei 14

Mshtakiwa, Pravinchandra Chavda ( kulia) anayekabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kutoa taarifa za uongo Polisi kwa lengo la kupewa ripoti ya upotevu wa hati za tano za viwanja, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  leo Aprili 16, 2024 baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Anakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kutoa taarifa za uongo polisi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Mei 14, 2024 kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kutoa taarifa za uongo Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inayomkabili mfanyabiashara,  Pravinchandra Chavda.

 Kuanza kusikilizwa kesi hiyo kunatokana na jalada la shauri hilo kurudishwa mahakamani kutoka kwa Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa wa Dar es Salaam (RPO) lilipokwenda kupitiwa.

Chavda (73), mkazi wa Upanga anakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kutoa taarifa za uongo polisi kwa lengo la kujipatia ripoti ya upotevu wa hati za viwanja vitano na kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga leo Aprili 16, 2024 amedai kesi iliitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi,  lakini mara ya mwisho jalada  lilipelekwa kwa RPO kupitiwa upya.

Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mshtakiwa kuwasilisha malalamiko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) yakiwemo ya kuomba kesi ifutwe.

DPP alimwelekeza RPO kupitia upya jalada hilo, kabla ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Aaron Lyamuya, alidai baada ya kupitiwa jalada hilo limerudishwa mahakamani kuendelea na usikilizwaji kama ilivyokuwa imepangwa awali.

"Jalada limesharudishwa  mahakamani kutoka kwa RPO, kinachofuata ni kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe  kwa ajili ya kuanza kusikilizwa," amedai.

Hakimu Lyamuya alimuuliza mshtakiwa kupitia wakili wake, Majura Magafu kama yupo tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Wakili Magafu amesema mteja wake yupo tayari kuendele na shauri hilo.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14, 2024 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Tangu upelelezi ukamilike na mshtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi katika usikilizaji wa awali (PH), Desemba 19, 2023, kesi ilipangwa kuanza Januari 27, 2024, lakini haikuendelea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mshtakiwa kuwa nje ya nchini kwa ajili ya matibabu.

Sababu nyingine ya kesi kutokuendelea na usikilizwaji ni mshtakiwa kuwasilisha malalamiko kwa DPP.

12 kutoa ushahdi

Aliposomewa maelezo ya mashahidi Desemba 19, 2023 upande wa mashtaka ulidai unatarajia kuwa na mashahidi 12 na vielelezo mbalimbali.

Upande wamashtaka unadai Chavda anakabiliwa na mashtaka manne ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma, kugushi na kuwasilisha nyaraka za kugushi.

Anadaiwa Januari 10, 2022 jijini Dar es Salaam alijipatia kiwanja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwasilisha kwa msajili wa hati nyaraka ya uhamisho wa kiwanja hicho akijifanya Mkurugenzi Mtendaji wa Sole, kampuni ya uwekezaji ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua si kweli.

Oktoba 7, 2019 katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, mshtakiwa anadaiwa alitoa taarifa za uongo kuhusu upotevu wa hati tano za viwanja kwa lengo la kujipatia hati za upotevu wa mali hizo wakati akijua si kweli.

Chavda anadaiwa akiwa jijini Dar es Salaam, akijua na kwa lengo la kudanganya alighushi nyaraka inayoitwa maazimio ya bodi akijaribu kuonyesha nyaraka hiyo ni halisi na imetolewa na Mkurugenzi wa Point Investment Limited, ambayo ni mmiliki wa kiwanja hicho wakati akijua si kweli.

Chavda anadaiwa Januari 10, 2022 mkoani Dar es Salaam aliwasilisha nyaraka ya kugushi kwa msajili wa hati akionyesha kiwanja namba 1814 kilichopo Msasani Peninsula aliuziwa.

Baada ya kusomwa maelezo ya mashahidi, mshtakiwa aliyakana isipokuwa majina yake, anuani yake, siku aliyokamatwa na Polisi, na siku aliyofunguliwa kesi na kufikishwa mahakamani. Kwa mara ya kwanza, alifikishwa mahakamani Oktoba 23, 2023.