Kesi tano za ugaidi zafutwa Kisutu

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta kesi tano za ugaidi na kuwaachia huru kwa masharti washtakiwa 12, waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kujihusiaha na vitendo vya ugaidi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta kesi tano za ugaidi na kuwaachia huru kwa masharti washtakiwa 12, waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kujihusiaha na vitendo vya ugaidi.

Ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Washtakiwa hao  Seif Mwishehe, Yusuph Rajabu, Buheti Buheti, Juma Athuman, Ally Nassoro maarufu kama Omary Swala, Hassan Mnele na wenzao sita.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hizo umetolewa leo Jumanne Machi Mosi, 2022 na Mahakimu watano tofauti, ambao ni Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi, Huruma Shahidi na Yusto Ruboroga, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Jopo la mawakili wanne wa upande wa mashtaka likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Waziri Magumbo akisaidiana na Ramadhani Kalinga, Ashura Mzava na Yusuph Avoid, wameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hizo zimeitwa kwa ajili ya kutajwa na lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Magumbo amedai washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 , iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao Desemba 23, 2015 na mwaka 2016 katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo, Dar es Salaam na eneo la Manyovu mkoani Kigoma.

Watatu walioshitakiwa kwa ugaidi Mtwara waachiwa huru

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imewaachia kwa dhamana watu watatu walioshitakiwa mwaka 2017 kwa madai ya kujiunga na kikundi Hisbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kujiunga nacho na kuanzisha dola ya kiislamu nchini. Soma zaidi