Watatu walioshitakiwa kwa ugaidi Mtwara waachiwa huru


Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imewaachia kwa dhamana watu watatu walioshitakiwa mwaka 2017 kwa madai ya kujiunga na kikundi Hisbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kujiunga nacho na kuanzisha dola ya kiislamu nchini.

Mtwara. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara imewaachia kwa dhamana watu watatu walioshitakiwa mwaka 2017 kwa madai ya kujiunga na kikundi Hisbu Tahir kinachodaiwa kushawishi watu kujiunga nacho na kuanzisha dola ya kiislamu nchini.

Ramadhani Moshi Kasoko, Waziri Selemani Mkalianganda na Omar Salum Bumbo wamekaa mahabusu tangu Desemba 5, 2017 baada ya kukamatwa kwa tuhuma hizo za ugaidi.

Watu hao wameachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuleta ombi maalumu mahakamani hapo kutaka waachiwe kwa dhamana huku upelelezi wa kesi dhidi yao ukiendelea.

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi hizo mbele ya mahakimu wawili tofauti.

Mbele ya Hakimu huyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Mwahija Ahmed amesema kuwa Jamhuri haina nia ya kuwashtaki washitakiwa hao katika kesi yao ya ugaidi.

Washitakiwa hao walikamatwa mwaka 2017 katika maeneo tofauti tofauti ya mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara, kisha kushitakiwa katika kesi namba 09/2017. Hadi wanaachiwa, upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa haujakamilika.

Hakimu Mkazi, Musa Esanju amesema jana Februari 23, 2022 kuwa washitakiwa hao wameachiwa kwa baada ya kutimiza vigezo vya dhamana ambayo ni pamoja na kila mmoja wao kuwa na wadhamini wawili wenye kiasi cha Sh20 milioni  kila mdhamini.

Hakimu Esanju amewaambia waandishi wa habari kuwa baada ya Jamhuri kujiridhisha kuwa wametimiza vigezo vya kupewa dhamana   washtakiwa hao wameachiwa.

Miongoni mwa masharti ya dhamana yao ni kutoa ahadi ya kutunza amani na kuonesha tabia njema kwa muda wa miaka mitatu wakiwa chini ya uangalizi.

Vile vile wametakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) mkoa wa Mtwara Kila ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa miaka mitatu.

Washtakiwa hao watakuwa chini ya uchunguzi na uangalizi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakifatiliwa nyendo zao. Iwapo watavunja makubaliano hayo, kesi dhidi yao itahuishwa.