Kesi wanaopinga kuhamishwa KIA yapigwa kalenda

Muktasari:
- Wananchi hao wamefungua kesi dhidi ya serikali wakipinga kuhamishwa katika eneo ambalo Serikali inadai ni mali yake.
Moshi. Kesi iliyofunguliwa na wananchi tisa dhidi ya Serikali, wakipinga kuhamishwa katika eneo lenye ukubwa wa hekari 11,000 za vijiji vine, vinavyopakana na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), imeahirishwa hadi Oktoba 5 mwaka huu baada ya wakili wa wajibu maombi kuwa na udhuru.
Akizungumza leo Jumanne Agosti 22, 2023; Jaji wa Mahakama wa Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Adrian Kilimi anayesikiliza kesi hiyo, amesema uamuzi wa maombi hayo ya wananchi wanaopinga kuhamishwa, utatolewa Octoba 5, 2023 ili kuwapa muda wa wajibu maombi ambao ni serikali, kujibu mapingamizi yao kwa maandishi.
Jaji huyo amesema mahakama itatoa uamuzi juu ya mapingamizi yaliyotolewa na waleta maombi kuhusu hoja za wajibu maombi hayo, zilizowasilishwa mahakamani nje ya muda wa kisheria wa kuwasilisha majibu.
Wakili wa Serikali, Hadija Matewele, aliyemwakilisha wakili wa wajibu maombi ambaye alipata udhuru, ameiomba mahakama hiyo, kuahirisha kesi hiyo kutokana na wakili anaeisimamia kusafiri kikazi.
Wakili wa waleta maombi, Jeremia Mjema, amesema shauri hilo limekuwa likipigwa kalenda mara kwa mara kutokana na upande wa Serikali kuleta mapingamizi nje ya muda wa kisheria.
Amesema hana pingamizi kwa ombi la wajibu maombi kuomba shauri hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi.