Kesi ya kina Mdee kuunguruma Agosti 26, wenzake saba watakiwa mahakamani

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kusikiliza kesi ya waliokuwa wanachama na Chadema, Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho, Agosti 26,2022.



Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kusikiliza kesi ya waliokuwa wanachama na Chadema, Halima Mdee na wenzake 18 wanaopinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho, Agosti 26,2022.

Tarehe hiyo imepangwa na Jaji Cyprian Mkeha, wakti kesi hiyo ilipoitwa leo Ijumaa Julai 29, 2022 kwa ajili maelekezo muhimu.

Vile vile mahakama imewataka Mdee na wenzake saba kufika mahakamani siku hiyo ya usikilizwaji kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano na mawakili wa Chadema.

Jaji Mkeha ametoa amri hiyo dhidi ya kina Mdee kufuatia ombi lililotolewa na kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Peter Kibatala kuomba waitwe ili waweze kuwafanyia mahojiano.

Mbali na Mdee wengine walioitwa ni Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga na Cecila Pareso.

Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama.

Wanapinga uamuzi huo uliotolewa na Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022; kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).

Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya  Wadhamini waliosajiliwa, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama kwa niaba ya Bunge la Tanzania; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Katika shauri hilo namba 36 la mwaka 2022, Mdee na wenzakeo wanaowakilishwa na mawakili  Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu wanaiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza  kisha itoe amri tatu.

Amri hizo ni ya kutengua mchakato na uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama (certiorari order), kukilazimisha Chadema kutimiza wajibu wake kisheria (mandamus), yaani kuwapa haki ya kusikiliza na amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitokana na rufaa walizozikata kina Mdee kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu, Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, bila ridhaa ya chama.