Kesi ya Mkude, METL kusikilizwa Mahakama Kuu

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga Novemba 27, 2023 kusikiliza usuluhishi katika kesi ya mchezaji wa Yanga, Jonas Mkude ambaye anaidai Kampuni ya Mohamed Enterprises (Tanzania) Limited fidia ya Sh1 bilioni kwa kutumia picha yake kwenye matangazo ya biashara ya bidhaa zake bila idhini yake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajia kusikiliza usuluhishi katika kesi ya kiungo wa Yanga, Jonas Mkude ambaye anaidai Kampuni ya Mohamed Enterprises (T) Limited (METL) fidia ya Sh1 bilioni kwa kutumia picha yake katika matangazo ya biashara ya bidhaa zake bila idhini yake.

 Kesi hiyo ya madai namba 192 ya mwaka 2023 imetajwa leo Novemba 20, 2023 mbele ya Jaji Butamo Philip na imepangwa kusikilizwa kwa hatua ya usuluhishi Novemba 27, 2023.

Mbali ya kudai fidia hiyo, Mkude ameiomba mahakama hiyo iamuru kampuni hiyo kumlipa mrabaha unaotokana na manufaa ambayo kampuni hiyo imeyapata.

Katika madai hayo, Mkude anadai kampuni hiyo ilitumia picha yake kutangaza biashara ya huduma zake na bidhaa kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram, Facebook na X (Twitter) bila ya kupata ridhaa kutoka kwake.

Mkude anadai Julai 12, 2023 aliingia katika mkataba na klabu ya Yanga na akiwa na timu yake mpya anajiandaa na mechi alikutana na tangazo la biashara lenye picha yake likiwa katika mitandao hiyo ya kijamii.

Matangazo hayo yalisambazwa kupitia mitandao rasmi ya METL na aliyapiga picha na baadaye kuzichapisha.

Anadai siku hiyohiyo alianza kupokea simu nyingi na ujumbe kutoka kwa ndugu, jamaa, mashabiki na mwajiri wake wakimpongeza kwa kupata fursa hiyo ya matangazo na wengine wakihitaji ufafanuzi juu ya suala hilo.

Katika hati hiyo inadai machapisho hayo yaliyopelekwa kwa umma yalipangwa, kuandaliwa na kusambazwa bila ruhusa yake wala kuhusishwa kwa namna yeyote ili aweze kutoa idhini au kuruhusu kutumikia kwa picha yake.

Anadai kwa kutumia picha yake kampuni hiyo ilipata umaarufu kwenye shughuli za kibiashara na kuvutia wateja ili watumie bidhaa zake na kupata faida huku ikimyonya yeye mdai na kukiuka hakimiliki.

Mkude anadai baada ya kutumiwa kwa picha zake bila idhini yake ameathirika kiuchumi na kisaikolojia, mambo ambayo hayawezi kupata tiba pasipo kulipwa fidia ya Sh1 bilioni kwa ukiukwaji huo wa haki zake.