Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkude adai fidia Sh1 bilioni METL

Dar es Salaam. Kiungo nyota wa Yanga, Jonas Mkude ameiburuza kortini Kampuni ya Mohamed Enterprises (Tanzania) Limited, akidai fidia ya Sh1 bilioni kwa kutumia picha yake katika matangazo ya biashara ya bidhaa zake bila ruhusa yake.

Mbali na kudai fidia hiyo, Mkude ambaye amewahi kuichezea Simba pia anaiomba mahakama iiamuru kampuni hiyo kumlipa mrahaba unaotokana na manufaa ambayo kampuni hiyo imepata.

Kesi hiyo ya madai namba 192 ya mwaka 2023, imefunguliwa Oktoba 2, 2023 katika  Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Dar es Salaam na Kampuni ya mawakili ya Bridge Attorneys & Consultancy ya Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mchezaji huyo nyota.

Kesi hiyo iko mbele ya Jaji Butoma Philip ambapo jana lilikuja kwa ajili ya kutajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza.

Mkude anailalamikia kampuni hiyo kutumia picha yake kutangaza biashara ya huduma zake na bidhaa kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram, facebook na Twitter sasa ikijulikana kama X bila kupata ridhaa kutoka kwake.

Kulingana na hati ya madai, Mkude anadai  Julai 12, 2023 aliingia mkataba na Klabu ya Yanga na akiwa na timu yake mpya anajiandaa na mechi, alikutana na tangazo la biashara lenye picha yake likiwa katika mitandao hiyo ya kijamii.

“Matangazo hayo yalisambazwa kupitia mitandao rasmi ya Twitter, Instagram na Facebook ya Mohamed Enterprises Limited (METL) ambayo aliweza kuyapiga picha (screenshot), kuyahifadhi na baadaye kuyachapisha," inasema hati hiyo ya madai.

Mkude anadai  siku hiyohiyo alianza kupokea simu nyingi na ujumbe mbalimbali kutoka kwa ndugu, jamaa, mashabiki na mwajiri wake, wakimpongeza kwa kupata bahati ya kupata fursa hiyo ya matangazo na wengine wakihitaji ufafanuzi juu ya suala hilo.

Kiungo huyo aliyedumu Simba kwa miaka 13, katika hati hiyo anadai  machapisho hayo yaliyopelekwa kwa umma, yalipangwa kuandaliwa na kusambazwa bila ruhusa yake wala kuhusishwa kwa namna yoyote ili aweze kutoa idhini au kuruhusu kutumika kwa picha yake.

"Kwa kutumia picha ya mdai (Mkude) kuzipa umaarufu shughuli zake za kibiashara na kuvutia wateja ili watumie bidhaa zake iliizesha METL kupata faida huku akimnyonya mdai na kukiuka haki miliki," inaeleza hati ya madai.

Mkude analalamika kuwa baada ya kutumiwa kwa picha zake bila idhini yake, ameathirika kiuchumi na kisaikolojia ambavyo haviwezi kupata tiba pasipo kulipwa fidia hiyo ya Sh1 bilioni kwa ukiukwaji huo wa matumizi ya picha yake bila idhini.