Kesi ya uhaini 1985: Konstebo akana kufundishwa jinsi ya kutoa ushahidi-49

Muktasari:

  • Machi 5, 1985, akimalizia kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhaini iliyowakabili Watanzania 19, wakiwamo wanajeshi 14, shahidi wa 48, Konstebo Mpelelezi Thobias, alikanusha mahakamani madai ya Wakili Murtaza Lakha kwamba alifundishwa jinsi ya kutoa ushahidi.

Machi 5, 1985, akimalizia kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhaini iliyowakabili Watanzania 19, wakiwamo wanajeshi 14, shahidi wa 48, Konstebo Mpelelezi Thobias, alikanusha mahakamani madai ya Wakili Murtaza Lakha kwamba alifundishwa jinsi ya kutoa ushahidi.

Konstebo Thobias alisema hakuna aliyemfundisha kutoa ushahidi isipokuwa alijikumbusha juu ya taarifa iliyoandikishwa polisi.

Lakha: Ulijikumbusha lini?

Thobias: Juzi.

Lakha: Wapi?

Thobias: Kwenye nyumba moja Mtaa wa Bagamoyo, Oysterbay.

Lakha: Ulikumbushwa na nani?

Thobias: Hawa unaowaona mbele yako isipokuwa wa katikati hakuwapo. (Hapo mbele walikuwa wamekaa Mkurugenzi wa Mashtaka, William Sekule; Wakili Mwandamizi wa Serikali, Johnson Mwanyika ambaye alikuwa katikati na Kulwa Sato Massaba).

Lakha: Una maana mkurugenzi wa mashtaka na ndugu Massaba?

Thobias: Ndiyo.

Lakha: Alikuwapo mtu mwingine?

Thobias: Alikuwapo ndugu Kumalilwa.

Lakha: Ulikuwapo humo ndani na nani mwingine?

Thobias: Nilikuwa peke yangu.

Lakha: Walikuwapo mashahidi wengine nje?

Thobias: Alikuwapo Konstebo Mshindo na wengine ambao siwajui.

Lakha: Hiyo nyumba ni ya nani?

Thobias: Sijui.

Lakha: Ni nyumba ya kuishi au ni ofisi?

Wakati Lakha alipoendelea kumhoji shahidi iwapo walikuwapo polisi na watu wa usalama kumfundisha jinsi ya kutoa ushahidi, Mkurugenzi wa Mashtaka, William Sekule, aliingilia kati.

Sekule alilalamika madai ya Lakha kuwa shahidi alikuwa amefundishwa jinsi ya kutoa ushahidi yalikuwa yameelekezwa kwake na msaidizi wake, jambo ambalo si sawa kwa kuwa walichofanya si kumfundisha shahidi bali ni kumkumbusha taarifa yake.

Mkurugenzi wa mashtaka aliendelea kuieleza Mahakama kwamba, utaratibu wa kumkumbusha shahidi taarifa yake unaruhusiwa, hivyo ndivyo alivyofanya pamoja na wasaidizi wake.

Kuhusu nyumba alikokumbushiwa shahidi, Sekule alisema inaeleweka kuwa iko chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwa alikuwa amekwishawasiliana na baadhi ya mawakili wa washtakiwa juu ya kuwapo kwa nyumba hiyo na utaratibu wa kuwakumbusha taarifa zao.

Alisema alichukua hatua ya kuwasiliana na baadhi ya mawakili kwa kuamini watawaeleza wenzao kutokana na suala la madai ya mashahidi kufundishwa kujitokeza mara kwa mara mahakamani.

Wakili Lakha aliiambia Mahakama kuwa, hakuwa na nia ya kuyalenga madai yoyote kwa mkurugenzi wa mashtaka na wasaidizi wake, isipokuwa ilibidi ashikilie suala hilo kutokana na taarifa alizokuwanazo kwamba polisi na maofisa wa usalama wamekuwa wakishiriki katika kuwahoji mashahidi.

Hata hivyo, Wakili Lakha aliomba upande wa mashtaka na Mahakama isimwelewe vibaya kwa kuuliza kuhusu ufundishaji wa mashahidi.

Alisema binafsi alikuwa hana taarifa ya Sekule kuwasiliana na mawakili wenzake juu ya taratibu za kuwakumbusha mashahidi na sehemu wanapokumbushiwa na kuongeza kuwa, angekuwa na taarifa hiyo asingeuliza juu ya suala hilo.

Akiendelea kujibu maswali ya Wakili Lakha, Konstebo Thobias aliiambia Mahakama kwamba alimkamata Sajini Michael kwa sababu alikuwa amevaa suruali ya polisi wakati yeye si polisi na kwa sababu hakuridhishwa na majibu yake wakati alipokuwa akimhoji kabla ya kumkamata.

Thobias alisema Sajini Michael alikuwa na bakora ilimtisha yeye (Thobias) na akahisi Sajini Michael alikuwa na nia ya kumwokoa Kapteni Suleiman Metusela Kamando ambaye tayari alikuwa chini ya ulinzi wake.

Thomas Mkude, ambaye alikuwa ni wakili wa Kapteni Suleiman Metusela Kamando, Kapteni Vitalis Gabriel Mapunda na Kapteni Roderic Rousham Roberts, alipomuuliza shahidi maelezo aliyopewa na Kapteni Kamando juu ya uhusiano wake na mtu aitwaye Joseph Kaijage kabla ya kumkamata, Thobias alisema Kamando alimwambia awali alikuwa akifanya kazi kikosi kimoja.

Mkude: Lakini umeiambia Mahakama alikuambia alikuwa na mtoto wake amelazwa hospitali na alikuwa anakwenda kutafuta msaada kwa Joseph Kaijage.

Thobias: Ndiyo. Na nilimuuliza kwanini hakwenda moja kwa moja kwenye kiwanda cha misumari kumwona. Alibabaika, alinieleza uhusiano wao kabla ya kueleza shida aliyokuwa nayo kwake.

Thobias alisema hakuridhika na maelezo ya Kamando na hivyo alimtuma Konstebo James kufanya uchunguzi kwenye kiwanda cha misumari iwapo kulikuwa na mtu aitwaye Joseph Kaijage na baadaye yeye akafanya uchunguzi mtaani na kugundua kiwanda hakikuwa na mtu huyo wala mtaani hapo hawakumjua mtu huyo.

Mkude: Vitu vyote ulivyomkamata navyo Kamando wakati unampekua vimeletwa mahakamani?

Thobias: Kuna vikaratasi vidogo vingine havikuletwa mahakamani.

Mkude: Kamando alikuwa na Sh3,341. Ziko wapi?

Thobias: Fedha hazituhusu.

Mkude: Uliziona?

Thobias: Sikuziona.

Mkude: Fedha hizo si miongoni mwa vitu ulivyomkabidhi Mfalingundi?

Thobias: Hakuwa na fedha.

Mkude: Hata senti tano?

Thobias: Hakuwa na fedha.

Mkude alimtaka shahidi kuiwasilisha taarifa yake ya polisi mahakamani ili iwe kielelezo cha upande wa utetezi. Mapema alikuwa ameisoma na kuthibitisha kuwa ni yake.

Shahidi ambaye alihojiwa na wakili J. T. Tarimo akisaidiana na Wakili E. Mbuya, baada ya kumalizia ushahidi wake kwa wakili huyo na hatimaye kuhojiwa na wazee wa baraza, Lawrence Saguti na Anne Kirundu pamoja na Jaji Kiongozi, ilibidi aitwe tena kizimbani kwa ombi la Wakili Tarimo.

Wakili Tarimo alitoa ombi hilo lililokubaliwa na Jaji Kiongozi kumuuliza shahidi iwapo anamtambua mtu ambaye alikamatwa na Mfalingundi kwenye nyumba ya Mkwajuni, Kinondoni majira ya saa moja jioni Januari 8, 1983, Shahidi alisema anamtambua na kumwonyesha mshtakiwa wa saba, Kapteni Dietrich Oswald Mbogoro ambaye alikuwa kizimbani.

Tarimo: Mapema umeiambia Mahakama kwamba wakati mtu huyo anakamatwa ulikuwa mbali na kwa vile giza lilikuwa limeanza kuingia usingeweza kumwona vizuri mtu huyo wakati anakamatwa. Sasa umemtambuaje?

Thobias: Kweli giza lilikuwa limeanza kuingia na nilikuwa mbali lakini wakati wa kumkamata, Mfalingundi alitoa amri ya kumtaka asimame iliyokuwa kwa sauti na mimi nikasogea karibu kuangalia.

Tarimo: Kipindi hicho kinatosha kukufanya umtambue hadi sasa?

Thobias: Mimi nilikuwa mmoja wa askari tuliomsindikiza hadi kwenye kituo cha polisi. Niliongea naye kwenye gari.

Tarimo: Kituo cha polisi alichukuliwa na Mfalingundi?

Thobias: Mfalingundi asingeweza kumchukua peke yake.

Mapema shahidi alikanusha madai ya Wakili Tarimo kwamba wakati wanalinda nyumba ya Kinondoni, Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mwongozo alikuja hapo nyumbani na kumwambiwa aondoke haraka la sivyo atakamatwa.

Aliiambia Mahakama kwamba wakati analinda nyumba ya Kinondoni alikuja mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu na kumhoji, mwishowe akamruhusu kuondoka baada ya kuthibitishwa na msichana mmoja kutoka nyumbani humo kwamba alikuwa rafiki yake.


Itaendelea kesho