Kesi ya uhaini 1985: Ubishi wa kisheria wazuka mahakamani, kesi yaahirishwa -50

Kesi ya uhaini 1985: Ubishi wa kisheria wazuka mahakamani, kesi yaahirishwa -50

Muktasari:

  • Ufumbuzi wa ubishi wa kisheria kati ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi uliilazimisha mahakama kuiahirisha kesi hiyo kabla ya muda wa kawaida.

Ufumbuzi wa ubishi wa kisheria kati ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi uliilazimisha mahakama kuiahirisha kesi hiyo kabla ya muda wa kawaida.

Ubishi huo ulizuka baada ya aliyekuwa meneja wa duka la Ramsons Ltd au B. Choitram katika Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, Banarsi L. Chohan au Ramesh, ambaye ni shahidi wa 50 upande wa mashtaka kuiambia mahakama kwamba Pius Lugangira, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, alifika kwenye duka hilo mwishoni mwa Desemba 1982.

Mkurugenzi wa Mashtaka, William Sekule, alimtaka shahidi huyo aeleze alichoambiwa na Lugangira siku hiyo aliyokwenda dukani kwao ambayo ilikuwa ni Desemba 27 mwakaa 1982. Baada ya kusikia maombi hayo ya mwendesha mashtaka, Wakili Hussen Muccadam alipinga kwa kusema isingewezekana kwa shahidi huyo kuieleza mahakama alichoambiwa na Lugangira kwa sababu huo ungekuwa ni ushahidi wa kusikia na ambao kisheria haukubaliki.

“Kama Lugangira hawezi kuitwa na kufika hapa mahakamani kama shahidi, basi napinga kwa shahidi huyu kusema kile alichoambiwa na Lugangira kwa vile ushahidi wake utakuwa ni wa kusikia ambao chini ya sheria za ushahidi mahakamani hauwezi kuzingatiwa na kukubaliwa,” alisema wakili Muccadam.

Hata hivyo, Sekule bado alitaka shahidi huyo aruhusiwe kusema kile alichoambiwa na huyo Lugangira. Alisema: “Katika mazingira ya kesi hii, naona shahidi huyo anaweza kabisa kueleza kile alichoambiwa na Lugangira kwa sababu yeye (Lugangira) pamoja na marehemu Tamimu daima wamekuwa wakitajwa walikuwa washiriki katika huo mpango wa uhaini.”

Akizidi kupinga kwa shahidi huyo kuruhusiwa kufanya hivyo, wakili Muccadam alisema: “Lakini, pamoja na kutajwa kama mshiriki, Lugangira bado hajashtakiwa. Hivyo kutajwa si sababu.”

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, Jaji Kiongozi alisema: “Nalazimika kuahirisha kesi hii mpaka kesho ili kuupa upande wa mashtaka fursa ya kufanya utafiti juu ya kifungu cha sheria ambacho kinaweza kunifanya mimi nimruhusu shahidi huyu kusema kile ambacho aliambiwa na Lugangira bila kuvuruga sheria za ushahidi mahakamani.”

Chohan, akiongozwa na Sekule, alisema kuwa kati ya Oktoba 1982 na Januari 1983 alipokuwa bado akifanya kazi kwenye duka hilo kabla ya kuanza biashara yake yeye mwenyewe, aliwahi kumtambua mtu mmoja kwa jina la Pius Lugangira.

Alisema alipata kumtambua Lugangira wakati alipofika kwenye duka lake Desemba 27 mwaka 1982 na kwa kipindi hicho mkurugenzi wa duka lenyewe, V. R. Choitram, alikuwa safarini Uingereza.

Shahidi wa 49 katika kesi hiyo, Shindo Mwaruka, konstebo mpelelezi kutoka Kituo cha Polisi cha Oysterbay naye aliieleza mahakama jinsi alivyotumwa kwenda kuichunga nyumba ya Drive In, asubuhi ya Januari 8 mwaka 1983 na kuona ni nani alikuwa akiingia na kutoka kwenye nyumba hiyo.

“Nilikwenda kwenye hilo lindo mimi pamoja na konstebo mwenzangu mpelelezi, Hariri Lowoo. Tulikuwa na maagizo ya kumkamata yeyote ambaye tulimwona akiingia au kutoka kwenye hiyo nyumba,” alisema shahidi huyo na kuongeza: “Tulianza kazi yetu saa 12.30 za asubuhi na ilipofika saa tatu, mtu mmoja mwenye makamo ya kutosha, mnene na mweusi, alifika na kutaka kuingia kwenye hiyo nyumba akidai kuwa alikuwa anakwenda kuwasabahi wapwa zake.”

Sekule: Ulifahamu vipi kuwa alikuwa akienda kuwasabahi wapwa zake?

Mwaruka: Alituambia mara baada ya kumsimamisha na kuanza kumhoji ni kwa nini alikuwa akitaka kuingia humo.

Sekule: Je, mtu huyo aliwaambia kitu chochote kuhusu wapwa zake?

Mwaruka: Hakutuambia, nasi tulimzuia asiingie kwenye hiyo nyumba baada ya kujitambulisha mbele yake kuwa sisi tulikuwa ni nani.

Sekule: Na hayo mazungumzo kati ya huyo mtu na wewe yalichukua muda gani?

Mwaruka: Kiasi cha dakika 15.

Sekule: Je, kuna mtu mwingine ambaye alikuja hapo baada ya huyo mtu?

Mwaruka: Hakuna mtu mwingine aliyekuja, isipokuwa wasichana wadogo walifika na kusema kuwa walikuwa wakimhitaji msichana mwenzao aliyeitwa Hope.

Konstebo Mwaruka aliongeza kuwa baada ya kutoka kwenye lindo hilo majira ya saa tisa mchana, walimkuta yule mtu ambaye walimhoji alipokuwa akitaka kuingia kwenye ile nyumba ya Drive In akiwa chini ya ulinzi kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

“Mimi nilimwarifu konstebo mwenzangu, James (shahidi mwingine) kuwa mtu huyo alifika kwenye lindo letu Drive In. Basi Konstebo James pamoja na Thobias walimchukua na kumpeleka kwa mkuu wa upelelezi wa kituo hicho, Mrakibu Msaidizi wa Polisi kwa wakati huo, Daudi Mfalingundi,” alisema Konstebo Mwaruka.

Alipoanza kuhojiwa na Wakili Thobias Mkude, shahidi huyo alitakuwa kusema ikiwa yeye alipata kwenda shule na alisema kuwa alikuwa amesoma hadi kidato cha nne kwenye Shule ya Sekondari ya Bagamoyo.

Mkude: Baaada ya kumaliza masomo yako, ulifanya nini na ulimaliza mwaka gani?

Mwaruka: Niliajiriwa na kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers.

Mkude: Ulikuwa ukifanya kazi gani? Karani au nani?

Mwaruka: Nilikuwa napiga chapa kwenye makopo ya nyama.

Mkude: Hujanieleza bado, ni lini ulimaliza kidato cha nne?

Mwaruka: Mwaka 1980.

Mkude: Na ni vipi ulijiunga na Jeshi la Polisi?

Mwaruka: Niliona jina langu limetangazwa kwenye magazeti kuwa nilikuwa nimechaguliwa kwenda Moshi kwenye Chuo cha Polisi kuchukua mafunzo ya kozi hiyo na ndipo nikaenda.

Mkude: Na ni nani hasa aliyekupa amri ya kwenda kwenye hiyo nyumba ya Drive In?

Mwaruka: Mkuu wangu wa kazi, Sajini Jeremiah.

Mkude: Na amri uliyopewa wewe ilikuwa ya nini?

Mwaruka: Kumkamata na kumhoji yeyote aliyejaribu kuingia au kutoka kwenye hiyo nyumba.

Kadhalika, baada ya kueleza kuwa aliandika taarifa polisi kuhusiana na kesi hiyo na hatimaye kuulizwa ni kwa nini ushahidi wake mahakamani ulitofautiana na maelezo yake polisi, shahidi huyo mara kwa mara alilalamika kuwa mwandishi wa taarifa hiyo pengine alikosea na kuandika mambo mengine ambayo yeye (shahidi) hakuwahi kuyasema.

Lakini wakati alipoulizwa kwa nini alitia saini yake baada ya kusomewa, shahidi hakuweza kueleza kinaganaga sababu zilizomsukuma kufanya hivyo isipokuwa alinyamaza kimya.

Mzee wa pili wa Baraza, Lawrence Shekilango Saguti, alimtaka shahidi kueleza ikiwa alikuwa na hakika kabisa kwamba mtu ambaye alikamatwa na akina James kwenye nyumba ya Mkwajuni Kinondoni ndiye yuleyule aliyefika Drive In. Shahidi alijibu kwa kusema: “Nina hakika kabisa.”

Saguti: Je, ulitambua jina lake?

Mwaruka: James aliniambia kuwa alikuwa akiitwa Kapteni Metusela Suleiman Kamando.

Saguti: Na wewe unasema kuwa mtu huyo alikamatwa Januari mosi mwaka 1983. Siyo?

Mwaruka: Ndiyo.

Saguti: Hivyo mtu mwingine akija na kusema kuwa alikamatwa Januari 7 mwaka 1983 atakuwa akisema uongo?

Mwaruka: Ndiyo. Atakuwa akisema uongo.

Nini kiliendelea katika kumbukumbu ya kesi hii ya uhaini, usikose kupata nakala yako ya mwendelezo?

Usikose toleo lijalo