Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA UKAHABA: Mahakama yatishia kuifuta, yatoa siku mbili

Baadhi ya wanawake wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba wakitoka katika Mahakama ya Sokoine jijini Dar es Salaam. Picha na Mpiga picha Wetu

Muktasari:

  • Jamhuri (upande wa mashtaka) katika kesi ya ukahaba imeshindwa kutekeleza amri za Mahakama mara tatu mfululizo, imeipewa siku mbili zaidi kutekeleza amri hizo ikitahadharisha kuwa kufikia Alhamisi kama itakuwa haijatekeleza moja hatua itakazozichukua ni kuifuta.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, jijini Dar es Salaam imeipa siku mbili Jamhuri (upande wa mashtaka) katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano, kutekeleza amri zake, huku ikiitahadharisha kama haijatekeleza mpaka Alhamisi ya Julai 11, 2024 itachukua hatua nyingine, ikiwemo kuifuta kesi hiyo.

Msimamo huo umetolewa na Hakimu Mfawidhi, Lugano Kasebele leo Jumatatu Julai 8, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kutoa uamuzi kuhusiana na hatua ya upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri za Mahakama.

Amri hizo ambazo upande wa mashtaka umeshindwa kuzitekeleza ni kuwasilisha taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa shahidi wake wa nne katika kesi hiyo, WP Konstebo (PC) Masadi Kassim Madenge wa kituo cha Polisi Magomeni Usalama.

Amri nyingine ni kuwafikisha mahakamani uthibitisho wa mashahidi wake wengine ambao pia ni maaskari polisi waliodaiwa kuwa wako kwenye kazi maalumu.

Mahakama ilitoa amri hizo baada ya mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi kupinga taarifa za ugonjwa wa shahidi huyo, wakidai Mahakama haiwezi kutambua ugonjwa kwa kuangalia kwa macho tu, hivyo kutaka upande wa mashtaka uwasilishe uthibitisho wa taarifa ya matibabu.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa shahidi aliyekuwa ameandaliwa kutoa ushahidi alipatwa na matatizo ya kiafya, hivyo kesi kuahirishwa.

Hata hivyo, waendesha mashtaka wa kesi hiyo, mawakili--- Tumaini Mafuru na Winfrida Ouko walidai mashahidi wao wengine ambao ni askari polisi walikuwa kwenye kazi maalumu, taarifa ambayo pia ilipingwa na mawakili wa utetezi wakitaka uthibitisho huo.

Mahakama ilikubaliana na hoja za upande wa utetezi ndipo ikatoa amri hizo mbili, kuwasilisha taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa shahidi huyo na uthibitisho wa mashahidi wengine kuwa katika kazi maalumu.

Akitoa uamuzi kuhusiana na mwenendo wa upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri hizo, Hakimu Kasebelea amerejea historia ya mwenendo wa amri zake kwa upande wa mashtaka na jinsi ambavyo umeshindwa kuzitekeleza.

Pia amebainisha msimamo au maelekezo ya Mahakama za juu (Mahakama Kuu) kwa suala kama hilo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Amesema Juni 27, 2024 Mahakama ilitoa amri mbili kwanza kuhusu uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi ambaye alitarajiwa kutoa ushahidi wake siku hiyo.

Amesema hoja hiyo ilizua utata baada ya upande wa utetezi kupinga wakihitaji uthibitisho wa kitabibu na kwamba, ili kuondoa wasiwasi Mahakama ikaamuru iletwe taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa shahidi huyo.

Hakimu Kasebele amesema Juni 28, 2024 shahidi huyo alifika mahakamani, lakini upande wa mashtaka ukaeleza alitakiwa kwenda hospitalini na Mahakama ikaamuru tena kuwa akitoka hospitalini taarifa ya matibabu yake iwasilishwe mahakamani.

“Toka tarehe hiyo mpaka sasa hakuna taarifa iliyoletwa. Kwa hiyo amri ya Mahakama haikutekelezwa,” amesema Hakimu Kasebele.

Amesema kuwa amri ya pili ilikuwa upande wa mashtaka una mashahidi 10, hivyo wawe wanaitwa watatu ili kutokucheleweshwa haki (yaani kama ikitokea dharura kwa shahidi mmoja mashahidi wengine wanaendelea).

Pia Hakimu Kasebele amesema Mahakama ilielekeza kuwa kama kuna tatizo, basi taarifa ya tatizo la kushindwa kuwaita mashahidi wengine itolewe mahakamani.

“Taarifa tuliyopewa na Wakili Tumaini ni kwamba mashahidi wengine walikuwa kwenye kazi maalumu ambayo hatujaambiwa inaishi lini,” amesema Hakimu Kasebele na kuongeza:

“Hili nalo lilizua wasiwasi wa kucheleweshewa kesi kutokana na sababu zisizo za msingi. Mahakama iliendelea kusisitiza waletwe mashahidi zaidi ya watatu na kama kuna changamoto taarifa itolewe, lakini mpaka sasa hizo hazijatekelezwa.”

Hakimu Kasebele amesema kuwa Julai 2, 2024 alipohoji kuhusu taarifa ya uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi huyo, upande wa mashtaka ulijibu kuwa shahidi tayari alikuwa ameshafika mahakamani na kutoa ushahidi wake.

Siku hiyo Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally alijibu hawakuwa na taarifa hiyo na kwamba hawawajibiki, huku akidai kuwa tayari shahidi huyo ameshafika mahakamani na kutoa ushahidi wake, basi yeye ndiye alipaswa kutoa taarifa hiyo.

Hata hivyo Hakimu, Kasebele amesema leo Jumatatu, Julai 8, 2024 kuwa Mahakama katika amri zake hizo haikusema kuwa kama shahidi huyo aliyedaiwa kuwa mgonjwa atafika mahakamani basi amri zake zinakoma.

“Julai 3, 2024 Mahakama iliamua kutoendelea na kesi kutokana na kuona kuna kitisho au wasiwasi wa amri zake kutokuendelea kutekelezwa,” amesema Hakimu Kasebele.

Amesisitiza kuwa licha ya mawakili wa utetezi kuwasilisha kesi rejea kuhusiana na maelekezo au msimamo wa Mahakama kuhusu utekelezaji wa amri za Mahakama, lakini cha kusikitisha upande wa mashtaka umeendelea kutokutekeleza amri hizo.

Hakimu Kasebele amesisitiza kwa mujibu wa hukumu mbalimbali za Mahakama Kuu (ambazo amezibainisha), kama upande wa mashtaka hawakuwa wameelewa amri ilizozitoa Mahakama walipaswa ama kuomba ufafanuzi.

Amesema kuwa hatua ya pili wangekata rufaa dhidi ya uamuzi/amri hizo, au kuiomba Mahakama ya juu ikatoa ufafanuzi wa amri hizo, lakini upande wa mashtaka katika hatua zote hizo hakuna ilichokifanya, badala yake umeendelea kutokutekeleza amri hizo.

Amesema kuwa amri ya Mahakama ni uamuzi rasmi wa Mahakama na kwamba amri hiyo ni agizo au maelekezo kwa upande uhusika, ili kuhakikisha haki inatendeka au sheria inafuatwa.

Amesema Mahakama Kuu imesema kutoheshimu amri ya Mahakama ni jambo baya ambalo halivumiliki na kwamba kuna hukumu mbalimbali zimetoa maelekezo amri za Mahakama zisipotekelezwa na upande husika.

Ameyataja maelekezo hayo kuwa Mahakama husika inaweza kutoa adhabu kali kwa wale wanaokaidi amri zake kama kutoa onyo, kulipa faini, adhabu ya vifungo, kufuta kesi pale itakapoonekana kuna haja ya kufanya hivyo kuwapeleka wahusika wanaokaidi amri hizo kwenye kamati za nidhamu.

Kutokana na maelekezo hayo, Hakimu Kasebele amesema Julai 2, 2024 ametoa onyo kwa upande wa mashtaka na kusisitiza  utekeleze amri hizo.

“Pia tunaelekezwa kutoa muda wa utekelezaji amri hiyo, kufuta kesi kama tatizo la utekelezaji amri halitafanyika. Kwa hiyo ninatoa siku mbili zaidi leo na kesho, Jumatano mtekeleze amri za Mahakama,” amesema Hakimu Kasebele na kusisitiza:

“Alhamisi tunatarajia mtawasilisha vielelezo hivyo (uthibitisho ugonjwa wa shahidi na mashahidi wengine kuwa kwenye kazi maalumu) msipofanya hivyo tutaenda kwenye hatua nyingine kama kufuta kesi kupelekwa kwenye vyombo vya kinidhamu, lakini hatutarajii kufika huko natumaini mmejifunza kitu,” amesema.

Hivyo, Hakimu Kasebele ameahirisha kesi hadi Alhamisi na kusisitiza itaendelea siku hiyo baada ya kutekelezwa kwa amri zake hizo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariam Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.