Kesi ya vipande 660 vya meno kusikilizwa mfululizo

Muktasari:

  • Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 30, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga siku tatu mfululizo kusikiliza kesi ya kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh4.6 bilioni, inayowakabili wafanyabiashara 12.

 Uamuzi huo umetolewa leo, Mei 30, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu Mrio amefikia uamuzi huo kutokana kesi hiyo leo kushindwa kuendelea na ushahidi kutokana na mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo Mussa Ligagabile (59) kuitaarifu Mahakama hiyo kuwa anakwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hemed Halfan alidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji lakini wamepokea barua kutoka kwa mshtakiwa Mussa Ligagabile kuwa hataweza hudhuria kwa sababu anakwenda hospital, hivyo anaomba kesi hiyo iendelee bila ya yeye kuwepo.

Wakili Halfani amedai kuwa licha mshtakiwa huyo kuandika barua ya kwenda leo hospitali, wameshanga kumuona mahakamani hapo akiwa na wenzake

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipoulizwa sababu ya yeye kutokwenda hospitali kama alivyoeleza katika barua yake, alidai kuwa tarehe aliyokuwa amepangiwa kuonana na daktari imesogezwa mbele hadi Juni 27, 2023 ndio maana amekuja mahakamani.

"Kwa kuwa tulikuwa tunafahamu mshtakiwa anakwenda hospitalini na kwakuwa mshtakiwa huyu hana uwakilishi wa wakili na sisi upande wa mashtaka hatukuleta vielelezo ( vipande 660 vya meno ya tembo) kwa sababu hiyo, lakini kwa taarifa tulizopata ndani ya mahakama hii ni kwamba mshtakiwa hakwenda hospitalini baada ya kusogezwa mbele kwa tarehe ya kumuona daktari, kutokana na hali hii, tunaomba Mahakama ipange terehe nyingine kwa ajili ya kuendelea," alidai wakili Halfani.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 13, 14 na Juni 15 itakapoendelea.

"Kesi hii naipanga kwa siku tatu mfululizo kuanzia Juni 13 Hadi Juni 15, 2023 na upande wa mashtaka mlete mashahidi wa kutosha ili kesi hii iweze kusonga mbele," amesema Hakimu Mrio.

Mashtaka yanayowakabili wafanyabiasha hao wanaokabiliwa na mashtaka 51 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupanga na kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh4.6 bilioni.

Pia, washtakiwa wanadaiwa kukutwa pesa taslimu dola za kimarekani 5662 ambazo ni sawa na Sh12, 270,492.

Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka, Wilfred Olomi, ambaye ni Mtunza vielelezo kutoka Wizara ya Maliasili, ameshatoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Ally Sharif (28) raia wa Guinea, mkazi wa Tabata Segerea; Victor Mawalla (29) maarufu kama Daudi Minja, mkazi wa Kimara Korogwe; Haruna Kassa (37) mkazi wa Mwanagati; na Abasi Hassan (40) maarufu kama Jabu, mkazi wa Mwanagati Kitunda.

Wengine ni Solomon Mtenya (46) maarufu kama Kuhembe, mkazi wa Kimara Baruti, Mussa Ligagabile (59) mkazi wa kibonde maji - Mbagala, Khalfani Kahengele (64) mkazi wa Keko; Ismail Kassa (53) mkazi wa Kipunguni B; na Kassim Saidi (50) maarufu kama Bedui mkazi wa Arusha.

Katika orodha hiyo pia wamo Peter Nyanchiwa (46) mkazi wa Isenye ; John Buhanza (60) maarufu kama John Muya au Tariye mkazi wa Gongolamboto pamoja na  Musa Musa (46) maarufu kama Musa Abdallah.