Kesi za ubakaji, ulawiti kila kona

Muktasari:

  • Mshtakiwa adai mtoto wa jirani aliingia kwake kuomba chai wakambambikia kuwa alitaka kubaka

Serengeti. Licha ya uwapo wa sheria kali kuhusu ubakaji, vitendo hivyo vimeendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali nchini.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, washtakiwa watatu wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za makosa tofauti mmoja kwa kosa la ubakaji na mwingine jaribio la kumbaka mtoto wa miaka (3).

Katika kesi ya jinai namba 248/2018 mwendesha mashtaka wa Polisi, Renatus Zakeo mbele ya hakimu Ismael Ngaile, alidai Sonda Chemele (18) anadaiwa kutaka kumbaka mtoto wa miaka mitatu.

Zakeo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 14 kijiji cha Nyiberekera, baada ya kujaribu kumbaka mtoto huyo.

Mshtakiwa alikana shtaka huku akidai kuwa mtoto huyo ni wa jirani yake na aliingia nyumbani kwake kuomba chai wakati anaingia ndani akakutana na kaka yake mlangoni ambaye hapo hapo alimkamata Sonda kwa madai kuwa alitaka kumbaka mtoto huyo.

Hakimu Ngaile aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5 huku mshtakiwa akirudishwa mahabusu.

Katika shauri jingine, Zakeo alimtaja Hezron Kenedy (32) mkazi wa kijiji cha Bwitengi anayedaiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye miaka 18 wa Sekondari ya Ikoma.

Alidai Agosti 31 majira ya usiku kijiji cha Bwitengi, mshtakiwa alimuingilia kimapenzi binti huyo bila ridhaa yake.

Mshtakiwa alikana mashtaka na kesi iliahirishwa hadi Oktoba 27, yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika

Wakati huohuo, kesi ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye miaka 17 wa Sekondari ya Machochwe inayomkabili mwalimu wa shule hiyo, Peter Manko (28) iliahirishwa hadi Oktoba 5. Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la ubakaji, alifikishwa mahakamani mara ya kwanza Agosti 8, alikana na alipata dhamana.