Kete 96 za heroini zinavyomtesa raia wa Liberia kwa miaka 12

Muktasari:

  • Mchakato wa kusikiliza kesi yake ulinza kupitia kesi ya jinai namba 27 ya 2016 iliyosikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Juliana Masabo na Oktoba 20, 2021 alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo jela miaka 20 na kulipa faini.

Dar es Salaam. Kama ni kupigania kuwa huru, basi raia wa wa Liberia, Edwin Cheleh Swen amepambana kwa miaka 12 sasa akijaribu bila mafanikio kujinasua na kifungo cha miaka 20 jela na faini ya Sh203 milioni, adhabu aliyohukumiwa na Mahakama nchini Tanzania.

Swen alikamatwa Mei 28, 2012 saa 9:45 alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akisafirisha gramu 1,509.35 za dawa za kulevya aina ya heroini zenye thamani ya Sh67.9 milioni, akijiandaa kusafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya Airways.

Dawa hizo zilikuwa katika mfumo wa kete na baada ya kukamatwa na maofisa wa Polisi uwanjani hapo na kupekuliwa, hakukutwa na kitu, kumbe alikuwa amezimeza.

Polisi walimweka chini ya uangalizi maalumu, ambapo alitoa jumla ya kete 96 kwa njia ya haja kubwa katika siku tofauti.

Mchakato wa kusikiliza kesi yake ulinza kupitia kesi ya jinai namba 27 ya 2016 iliyosikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Juliana Masabo na Oktoba 20, 2021 alitiwa hatiani na kuhukumiwa miaka 20 na kulipa faini.

Tangu alipokamatwa alikuwa akikanusha kukutwa na dawa hizo hadi alipotiwa hatiani na Mahakama Kuu na ameendelea kupigania kujinasua na adhabu hiyo, alikata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, lakini nako ameshindwa.

Aprili 17, 2024, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Winne Korosso, Sam Rumanyika na Leila Mgonya waliitupa rufaa yake wakisisitiza kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa wa kuaminika na mashtaka yalitibitishwa bila kuacha mashaka.

Hukumu hii ya jopo la majaji watatu inafanya safari ya kupigania kutokuwa na hatia ya kosa la jinai kufikia mwisho kwa kuwa kwa mfumo wa Mahakama Tanzania, Mahakama ya Rufani ndio ya juu, hivyo pengine kama atapewa msamaha na Rais.


Hivi ndivyo alivyonaswa JNIA

Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, Mei 28, 2012 saa 9:45 alfajiri katika uwanja wa JNIA, Makole Bulugu ambaye baadaye alikuwa shahidi wa nane, alimkamata raia huyo wa Liberia baada ya kupokea taarifa fiche kuwa mgeni huyo anajihusisha na usafirishaji dawa za kulevya.

Ufuatiliaji wa taarifa hizo fiche ulihusisha ukaguzi wa majina kwa kila hati ya kusafiria ya mgeni aliyekuwa akipita eneo la ukaguzi na baada ya kuona hati ya raia huyo wa Liberia, alimkamata na kumjulisha anashukiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Alipelekwa Kituo cha Polisi Uwanja wa Ndege ambako alipekuliwa na kukaguliwa lakini hakukutwa na kitu. Matokeo ya ukaguzi huo yalimfikia Kamishina Alfred Nzowa ambaye aliagiza mgeni huyo awekwe chini ya uangalizi na safari yake ikasitishwa.

Kutokana na maelekezo hayo, alihamishiwa Ofisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU-JNIA) na kuwekwa chini ya uangalizi, ambapo kati ya siku hiyo hadi Juni mosi, 2012, mtuhumiwa huyo ambaye sasa ni mfungwa, alitoa jumla ya kete 96 za dawa hizo.

Dawa hizo zilipelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambayo baada ya kuzipima katika maabara, ilithibitisha ni dawa za kulevya aina ya heroini na baadaye vyombo vingine vilitoa thamani ya dawa hizo kuwa ni Sh67, 920, 750.


Alivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, mtuhumiwa alikanusha mashtaka hayo na kutoa utetezi wa Alibi, kwamba hakuwepo kabisa eneo hilo la JNIA siku na saa inayotajwa, bali alikuwa eneo lingine kabisa mbali na uwanja huo.

Akijitetea mbele ya Jaji Masabo ili kujinasua kosa hilo, alisema Mei 25, 2012 hakukamatwa JNIA kwa kuwa aliingia Tanzania Mei 22, 2012 kwa ajili ya mapumziko na alifikia na kukaa katika Hoteli ya Joe iliyoko eneo la Sinza Jijini Dar es Salaam.

Aliiambia Mahakama kuwa Mei 25, 2012 alikamatwa na maofisa watatu wa polisi akiwa katika eneo la Sinza na baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Akiwa kituoni hapo, alidai alipekuliwa na baadaye hati yake ya kusafiria, tiketi ya ndege ya Kenya Airways, kitambulisho na risiti za hoteli vilichukuliwa na hapo ndipo aliwekwa mahabusu bila kuelezwa sababu za kukamatwa kwake na maofisa wa Polisi.

Baadaye, alidai alipelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama iliukataa utetezi wake na kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na kumhukumu kifungo cha miaka 20 na kulipa faini ya Sh203 milioni, mara tatu ya thamani za dawa.


Akakata rufaa

Raia huyo wa Liberia hakuridhishwa na hukumu hiyo ya Jaji Masabo na kupitia kwa wakili wake, Kung’e Wabeya alikata rufani Mahakama ya Rufaa na kuwasilisha sababu za rufaa 10 Machi 21, 2022.

Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Jaji hakupima vyema mizania ya ushahidi na hivyo kufikia hitimisho la kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 20 na kulipa faini ya zaidi ya Sh200 milioni kwa kuegemea ushahidi dhaifu na unaojikanganya.

Sababu nyingine ni kuwa Jaji alishindwa kuwa huru katika mwenendo wa kesi na hukumu, na kusababisha kuupa uzito ushahidi usiounganika, usioaminika, unaojikanganya wa shahidi wa 2 na kielelezo cha Jamhuri namba 2.

Pia akaeleza kuwa wakati Jaji anamhukumu, hakuzingatia miaka tisa na miezi mitano ambayo alikuwa ameshakaa mahabusu kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa na hakuzingatia mnyororo wa vielelezo tangu vilipodaiwa kukamatwa JNIA.

Pia alisema Jaji alishindwa kutilia maanani kiwango cha uthibitishokinachotakiwa na upande wa mashtaka ili kuthibitisha kesi, ikizingatiwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka.


Kisa rufaa kutupwa

Katika hukumu yao baada ya upande wa Jamhuri kupinga sababu za rufaa, jopo la majaji hao lilisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, kazi iliyokuwa mbele yao ni kuweka mizania kama sababu za rufaa za mrufani zilikuwa na mashiko.

Hata hivyo, jopo hilo lilichambua sababu moja baada ya nyingine ya rufaa na kuzitupa zote huku likisema hoja kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka dhidi yake, wala isingehitaji kuwapotezea muda kwani ushahidi wa Jamhuri uliaminika.

Mbali na ushahidi uliotolewa kortini kuaminika, walisema vielelezo vyote vya Jamhuri vilipokelewa kwa usahihi na Mahakama na utetezi wake wa Alibi haukutikisa mzizi wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hukumu hiyo ilisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, F.A Mtarania mbele ya Wakili Kubeya aliyemtetea mrufani ambapo mrufani ambaye alikuwa gereza la Ukonga, aliunganishwa kusikiliza hukumu hiyo kwa njia ya mtandao.