Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIA yaomba radhi zoezi la utayari la uvamizi kuzua taharuki kwa abiria

Mkurugenzi Mkuu wa KADCO, Christine Mwakatobe akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za uwanja wa ndege KIA leo, Februari 28, 2024. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:


  • Menejimenti ya Uendeshaji na Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO) imesema tukio la kigaidi la uvamizi wa jengo la abiria katika uwanja huo lilikuwa ni zoezi la utayari, sio tukio halisi.

Moshi. Menejimenti ya Uendeshaji na Uendelezaji wa kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), imesema tukio la kigaidi lililohusu uvamizi wa jengo la abiria katika uwanja huo wa ndege na kuzua tahuriki kwa abiria waliokuwa uwanjani hapo halikuwa halisi, bali zoezi la utayari.

 Zoezi hilo lililofanyika juzi Februari 26, mwaka huu lilidumu kwa nusu saa na kuleta taharuki kwa abiria na wadau wa usafirishaji waliokuwepo uwanjani hapo.

Akizungumzia tukio hilo, leo Februari 28, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa KADCO, Christine Mwakatobe amesema zoezi hilo hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili, ikiwa ni kupima utayari katika kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza katika viwanja vya ndege yakiwemo matukio ya kigaidi.

"Juzi tulifanya zoezi la utayari na lilikuwa ni la kigaidi linalohusu uvamizi wa jengo la abiria na lilianza saa 5:05 na kumalizika saa 5:35 asubuhi, katika zoezi hili kulizuka hali fulani ya taharuki kwa abiria na wadau mbalimbali ambao ni watumiaji wa uwanja huu.

"Lengo la zoezi hilo ilikuwa ni kukidhi matakwa ya sheria yaliyoaanishwa na Shirika linalosimamia Usafiri wa Anga duniani (ICAO) pamoja na kanuni za Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA)," amesema.

Amesema tukio hilo lililenga kupima utayari wa uwanja cha ndege KIA katika kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo matukio ya kigaidi na utayari unaopimwa ni pamoja na maarifa, uelewa na mbinu za kujiokoa, miundo mbinu, vifaa, mifumo, uratibu, mawasiliano na maokozi.

Hata hivyo, menejimenti ya KIA imeomba radhi kwa taharuki hiyo iliyojitokeza kwa abiria na wadau katika uwanja huo.

"Tunaomba radhi kwa wadau wetu na abiria ambao walipata changamoto za hapa na pale kutokana na zoezi hili," amesema Mwakatobe

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni na ufundi KIA, Martine Kinyamagoha, amesema zoezi hilo lilifanyika kwa usiri mkubwa na risasi zilizotumika si halisi na zilikuwa hazina madhara yoyote.

"Zoezi hili lipo kwa takwa la kisheria kwa ajili ya kujipima namna ya kukabiliana na majanga wakati yanapojitokeza, zoezi la jana lilikuwa ni kama uwanja wa ndege umevamiwa na magaidi ambao waliingia na risasi katika uwanja huo wa ndege,"

"Zoezi hili lilifanyika kwa usiri mkubwa, ndio maana juzi kulikuwa na taharuki kubwa na ndivyo inavyotakiwa ifanyike, risasi zilizotumika si halisi zilikuwa ni za bandia, zilikuwa zinatoa tuu mlio, lakini zilikuwa hazina madhara yoyote," amesema Maghoha.