Kiama cha wadaiwa sugu Tanesco chaja

Muktasari:


Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia huduma hiyo.

Hatua hiyo inakuja wakati Tanesco inadai jumla ya Sh224 bilioni kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi na waliohama na madeni kutoka mita za zamani kwenda za kisasa hali inayopelekea changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumapili Novemba 26, 2023, wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi  wa ujenzi  wa njia  kuu ya umeme  ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya (KTPIP).

“Hapa Arusha tu, Tanesco inadai wateja wake sh7.7 bilioni na mara nyingi wanaodaiwa si wananchi wadogo bali taasisi za Serikali na wawekezaji wanaojiita wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira, wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira.

“Tanesco inahitahi fedha ili iwekeze na kisha iwapelekee umeme wananchi. Nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki,” amelipa rungu Shirika hilo.

Pia, ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi.

Vilevile ameigeukia Tanesco kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe.

“Huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha huduma kwa wateja tukiimarishe kutoka miito 65 na iongezwe kufika 100 na zaidi,” amesema.