Kiama kwa ‘makanjanja’ katika taaluma ya habari chanukia
Muktasari:
- Kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, unatarajiwa kuziba mianya ya wajanja wanaojifanya wanahabari ilhali hawana taaluma hiyo.
Dar es Salaam. Huenda mwaka huu ukawa mwisho wa ‘makanjanja’ kuivamia taaluma ya habari, baada ya Serikali kutangaza mchakato wa kuunda Bodi ya Ithibati ya Wanahabari utakaokamilika Desemba.
Kuundwa kwa bodi hiyo ni matakwa ya Ibara ya 11 (1) ya Sheria ya Huduma za habari ya mwaka 2016 na kimsingi itajihusisha na ithibati ya wanahabari, kutoa vitambulisho na kusimamia maadili katika utendaji kazi wao.
Mchakato huo, utatanguliwa na marekebisho ya kanuni ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, utakaofanyika kwa vyombo vya habari kutumiwa rasimu yake kisha kutoa mapendekezo kupitia Idara ya Habari Maelezo.
Hata hivyo, bodi hiyo inatarajiwa kufunga milango ya wasio na taaluma ya habari kufanya kazi za habari kama inavyoshuhudiwa sasa, kulingana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), Suleiman Msuya.
Taarifa ya kuundwa kwa bodi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo, Jumapili Oktoba 28, 2023 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari.
Katika hilo, ameeleza sheria hiyo inataka kuundwa kwa bodi ya ithibati ya wanahabari ambayo kisheria inahitaji majina ya waandishi wa habari watakaokuwa sehemu ya wajumbe.
“Tuliomba vyombo vya habari vituletee majina na tunashukuru vyombo vya habari vimetuletea majina, mchakato utakaofanyika litateuliwa jina kulingana na mapendekezo na nadhani kufikia Desemba kama mambo yatakwenda sawa sawa tutakuwa tumeipata bodi hiyo,” amesema.
Akizungumzia hilo, Msuya amesema bodi hiyo itakuwa na tija inayotarajiwa, iwapo Serikali itaiwezesha kwa kuwa na rasilima watu ya kutosha.
Amekiri uwepo wa wanaofanya kazi za habari ilhali hawana taaluma hiyo, akisisitiza baadhi wanamiliki hadi vitambulisho.
“Wapo watu wanamiliki vitambulisho, lakini msingi wa haya yote ni kuwepo kwa utaratibu holela wa uanzishaji wa vyombo vya habari,” amesema.
Hata hivyo, Msuya amesema uamuzi huo wa Serikali ni jambo la kupongeza kwa kuwa kimekuwa kilio cha muda mrefu cha chama hicho na kilishawahi kupeleka hadi mapendekezo ya majina ya wajumbe wa bodi hiyo.
Katika mkutano huo, Matinyi amesema kuundwa kwa bodi hiyo, kutafuatiwa na kuundwa kwa Baraza Huru la Vyombo vya Habari na kisha utaundwa mfuko wa mafunzo ya waandishi wa habari.
“Muda sasa umefika vya kutosha tunakwenda kukamilisha vile vyote ambavyo sheria inavitaka,” amesema.
RC, DED kutoa taarifa
Matinyi amesema ofisi yake inatarajia kuzindua program ya kutembelea Wakuu wa Mikoa ili watoe taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao.
Amesema program hiyo itazinduliwa Novemba 1, mwaka huu mkoani Dodoma, kisha itafuatia Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
“Tutafika katika Mkoa, atakuja na wakuu wake wa Wilaya lakini tunataka tuwape nafasi wakurugenzi wa halmashauri kwa sababu tunataka kusikia habari za utekelezaji na katika muundo wetu fedha zinapelekwa kwenye halmashauri,” amesema.