Kiapo cha Mkapa chazua mvutano mkubwa mahakamani kesi ya Profesa Mahalu ikisikilizwa

Tuesday May 04 2021
mkapapic
By James Magai

Katika sehemu iliyotangulia ya mapitio ya kesi ya aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Ricky Costa Mahalu jana, tuliona upande wa utetezi ukiwaorodhesha viongozi wakuu wa nchi akiwamo Rais aliyekuwa madarakani, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa Ujenzi wakati huo, John Magufuli ambaye alikuja kuwa Rais wa awamu ya tano kama mashahidi wa utetezi.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 1 ya mwaka 2007, Profesa Mahalu na aliyekuwa ofisa utawala wa ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Grace Martin walishitakiwa kwa mashitaka sita yakiwemo ya kula njama, kutumia nyaraka za ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kumdanganya mwajiri wao (Serikali), wizi wa Euro 2,065,827 (zaidi ya Sh2.5 bilioni) na kuisababishia Serikali hasara.

Walidaiwa kutenda makosa hayo Septemba 23 mwaka 2002 kwa kutumia mikataba miwili tofauti ya ununuzi na kutozingatia baadhi ya taratibu za ununuzi wa Serikali. Kesi dhidi yao ilipata umaarufu wa pekee baada ya Rais Mkapa kupanda kizimbani kumtetea Profesa Mahalu akitofauti na ushahidi uliotolewa na Serikali. Mkapa aapa mahakamani Baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaona Profesa Mahalu na Grace wana kesi ya kujibu.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Ilvin Mugeta hivyo walitakiwa kujitetea kabla mahakama haijatoa hukumu kama wana hatia au la. Katika hatua hii ndipo Rais Mkapa alipolazimika kupanda kizimbani kuwatetea Profesa Mahalu na mwenzake. Ingawa kesi hiyo ilikuwa na mvuto tangu siku wanadiplomaisa hao walipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo, Januari 22 mwaka 2007, uamuzi wa Mkapa kukubali kupanda kizimbani uliongeza mvuto wa kesi hiyo. Kwa uamuzi huo Makapa pia aliweka historia ya kuwa kiongozi wa juu kabisa wa nchi kupanda kizimbani kutoa ushahidi, tena kuwatetea watuhumiwa.

Ni uamuzi ambao ulivuta hisa za watu wengi ndani na nje ya nchi huku wanasheria, viongozi wa kisiasa na wananchi wa kawaida wakilijadili suala hilo kwa nyakati tofauti. Kabla ya kupanda kizimbani, Rais Mkapa aliwasilisha mahakamani hapo kiapo kama kielelezo cha utetezi wake kwa washtakiwa hao.

Hata hivyo kiapo hicho kiliibua malumbano kwa mawakili wa pande zote mbili za kesi hiyo. Malumbano yalitokana na kile kilichodaiwa na upande wa mashtaka kuwa kuvuja kwa taarifa za kiapo hicho kwenye vyombo vya habari, kila upande ukiushutumu mwingine kukivujisha.

Advertisement

 Ilikuwa ni Mei 31 mwaka 2011, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa mara ya kwanza baada ya Mkapa kuwasilisha kiapo chake na washtakiwa kuanza kujitetea. Siku hiyo, mmoja wa mawakili wa Mahalu na mwenzake, Mabere Marando aliiomba mahakama iingize hati ya kiapo kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo. Hata hivyo, Hakimu Mugeta alilikataa ombi hilo akisema ameipokea hati hiyo ya kiapo cha Rais Mkapa lakini wakati wa kuizungumzia bado haujafika.

Hakimu Mugeta alifafanua kuwa hati hiyo itazungumziwa baada ya washtakiwa kueleza namna watakavyojitetea, iwapo watafanya hivyo kwa mdomo au kwa viapo, pamoja na kueleza idadi na kutaja mashahidi wao na vielelezo watakavyoviwasilisha.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Ponsiano Lukosi aliushutumu upande wa utetezi katika kesi hiyo baada ya kiapo cha Mkapa kuanza kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kabla ya kufika mahamani.

Wakili Lukosi alitoa mfano wa gazeti la Mwanahalisi la Aprili 27 mwaka huo lililochapisha kiapo hicho, kuchambua kila kipengele na kukitolea uamuzi kuwa upande wa mashtaka sharti ukunje jamvi kwa kuwa hauna kesi kutokana na kiapo hicho cha Rais.

Pia alizungumzia habari iliyoandikwa na Mwananchi siku moja kabla iliyomkariri Marando akithibitisha kuwa barua waliyomwandikia Rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuomba akubali kuwatetea washtakiwa hao. Katika habari hiyo, wakili Marando alilieleza Mwananchi kuwa Rais Kikwete alikuwa hajajibu barua hiyo na kwamba kutokana na umuhimu wa Rais Kikwete katika kesi hiyo, iwapo wateja wake watamaliza kujitetea pamoja na mashahidi wengine wataiomba mahakama imkumbushe.

Pia wakili Marando alion geza kwamba kama hataridhia wataiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi mwaka 2016 atakapomaliza kipindi chake cha urais ili mahakama imlazimishe kufika mahakamani kutoa ushahidi. Kutokana na habari hizo, wakili Lukosi aliiomba mahakama kutoa mwongozo akidai kuwa mawakili wa utetezi wameanza kusahau matakwa ya taaluma ya sheria kwa kutoa vielelezo vya ushahidi kwe[1]nye vyombo vya habari kabla havijawasilishwa mahakamani.

 Akijibu shutuma hizo, Wakili Marando alisema yeye ndiye aliyeandaa hati hiyo ya kiapo lakini naye akautupia lawama upande wa mashtaka kuwa ndiyo unaopaswa kueleza zilifikaje kwenye vyombo vya habari. “Mimi ndiye niliyeiandaa document (hati) hii kwa mkono wang na nilikuwa nimeifungia mahali ambapo mtu yeyote hafiki. Kutokana na ‘sensivity’ (unyeti) wake niliikabidhi Serikali waraka huo kabla ya Aprili 27,” alidai Marando na kuongeza: “Lakini wiki moja baadaye, nilishtuka kuiona kwenye gazeti kwani hata mteja wangu hakuwa na nyaraka hizo.

Hivyo mimi ndiye niliyestahili kuwalaumu. Hata barua niliyomwandikia Katibu Mkuu Kiongozi nayo nilishtukia iko kwenye magazeti.” Kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti hili alisema: “Mwananchi walinipigia simu wakiuliza utaratibu wa kisheria wa kumwita Rais, nami nikawaeleza kwa mujibu wa Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Mambo ya Rais Aliye Madarakani na hicho ndicho walichokiripoti.” “Mimi naona halijaharibika jambo na tusikubali kuziba midomo magazeti pasipo ulazima,” alisisitiza wakili Marando. Baada ya hoja hizo za kurushiana maneno kati ya pande hizo mbili, Hakimu Mugeta aliiahirisha kesi hiyo na kupanga kuitaja Juni 24 mwaka 2011 ili washtakiwa waanze kujitetea Julai 8 na 11.

Advertisement