Kibajaji, Msukuma wataka Dk Bashiru aachie ngazi

Dk Ally Bashiru

Muktasari:

Ikiwa siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) kumkia aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Ally Bashiru, wabunge wa chama hicho pamoja na wakulima wamemtaka kutafakari kauli yake dhidi ya wanaomsifu Rais Samia Suluhu Hassan

Dodoma/ Mtwara. Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Livingstone Lusinde (Mtera) na Joseph Msukuma wa Geita Vijijini wamemtaka aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Ally Bashiru kuachia ubunge kama anakerwa na kusifiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, wamesema Dk Bashiru hakupaswa kukerekwa na uchawa kwasababu yeye ndiye chawa mkuu kwasababu ubunge wake umetokana na Ikulu, “na yeye ndiyo mwanzilishi wa mapambio ya kupongeza utendaji kazi wa Rais.”

Akiwa katika Mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Novemba 17,2022 mkoani Morogoro, Dk Bashiru aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa mbunge aliwataka wakulima kushikamana ili waweze kufikisha ujumbe kwa wanaowaongoza.

Alisema sauti ya wakulima iwatishe aliwowaita wanyonyaji na kama hawajafika kwenye hatua hiyo ya kuwa watu au kundi la kutisha wanyonyaji bado watakuwa hawajafikia malengo.

“Hatutakuwa tofauti na mawakala wao wanaowapambana wakati mwingine kuwadanganya kwamba unaupiga mwingi,”alisema.

Leo Jumapili Novemba 20, 2022, Lusinde akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma amesema katika uongozi wake wote akiwa Katibu mkuu wa chama bajeti ya wizara ya kilimo ilikuwa ni Sh250 bilioni lakini imepanda wakati wa uongozi wa awam ya sita bajeti hiyo imepanda hadi Sh950 bilioni.

Amesema licha ya mfanikio hayo, Dk Bashiru ambaye pia ni mjumbe Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mfugo na Maji hajawahi kuitisha mkutano na waandishi wa habari wala kumpongeza Rais kwa kumteua kuwa mbunge.

Amesema hata kwenye dini, wanafundishwa kushukuru kwa mambo wanayotendewa lakini Dk Bashiru ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, anawaambia wasimshukuru Rais Samia kwa kuwa anakerwa na waosema anaupiga mwingi.

“Kwa Kariba yake yeye jimbo lake ni Ikulu yaani muda wowote anapokuja bungeni jimbo lake ni Ikulu, anatakiwa kuizungumzia vizuri Ikulu kwasababu kwasababu ndio imemteua kuwa mbunge,” amesema.

“Nataka kumshauri Dk Bashiru kwa kuwa yeye anatokana na Ikulu na kwakuwa anajisikia kishefu chefu ikitajwa ikulu, Dk Bashiru anatakiwa ampe mama nafasi achague mbunge mwingine ambaye atamuelewa mama mchezo anaocheza na atakwenda naye sambamba,” amesema

Amesema Bashiru akiwa Katibu Mkuu wa CCM ndiye aliwafundisha kuimba mapambio ya kusifu na mwimbishaji alikuwa ni yeye.

“Mwimbishaji alikuwa ni Dk bashiru kwa hiyo leo hii leo inakuaje mtu alikuwa akiimbisha mapambio ya kusifu chama kile kile ambacho aliyekuwa makamu ndiye Rais sasa anapata kichefu chefu. Tunaposimamna kusifu tunaonyesha na data (takwimu),”amesema Lusinde ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Wakati Lusinde akizungumza akiwa Dodoma, mwenzake wa Msukuma amekutana na waandishi wa habari jijini Mwanza ambapo amesema amesikitishwa na kauli ya Dk Bashiru kwa sababu alikuwa ni katibu wa CCM mstaafu anayejua vitu vingi lakini alidai wa kiongozi huyo wa zamani alizungumza maneno ya kijinga.

“Kama yeye alichomoa fyuzi na sisi tunachomoa, inauma kusikia Rais wako anatukanwa, wakati akiwa akiwa katibu mkuu tulimsifu sana Rais John Magufuli (hayati) na hakuna aliyepinga na Dk Bashiru alikuwa mbele kumsifia ndani ya CCM na majukwaani.”

“Sasa inakuaje tusimsifu Rais Samia Suluhu Hassan kama anaupiga mwingi? Tumseme au tumsifu nani? Nimemuombe Dk Bashiru atoke hadharani aombe radhi, tusilaumiane, Watanzania wengi wanaosema ameupiga mwingi tumeuona.

Musukuma amesema hawakubaliana na kauli ya Dk Bashiru, akisema akiwa Bungeni mbunge huyo anazungumza lakini akiwa mtaani anaponda “anataka tumsifu yeye wakati katoka CCM na matatizo mengi? Serikali inafanya kazi, Rais Samia endelea kufanya watu wa diziani ya kina Bashiru wapo na wataendelea kuwepo.”

Nao, baadhi ya viongozi wa wakulima kutoka mikoa minne ya Ruvuma, Pwani, Lindi na Mtwara wamemuonya Dk Bashiru Ally kuacha kuwatumia kwa manufaa yake.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa mkoa wa Mtwara, Karimu Chipola amesema wakulima wanajitambua na wanaweza kujisemea wenyewe.

Amesema Serikali ya awamu ya tano ilitoa  pembejeo za kilimo cha korosho zenye thamani kubwa bure kwa wakulima wote wakati  Dk Bashiru akiwa kiongozi alishindwa kumshawishi Rais aliyekuwa madarakani kufanya hivyo.


“Unajua Rais Samia Suluhu ameturudishia fedha za export levy katika sekta ya korosho hapa nchini fedha hizo hulipwa na wanunuzi wa korosho ghafi hapa nchini,” amesema

Naye mwakilishi wa wakulima kutoka mkoani Pwani, Musa Mngeresa amesema wakulima wanapaswa kuwa imara na kuwaepuka wanasiasa wanaotuchonganisha na Serikali.

“Tunaomba wakulima wasikatishwe tamaa na maneno ya chuki, tusiyumbishwe tuungane, tushikamane na kuacha maneno ya kichochezi sisi tunazo taasisi zetu hatuwezi kumruhusu mtu kutumia wakulima kama ngazi,” amesema Mngereza

Jitihada za kumpata Dk Bashiru kujibu tuhuma hizo zilizoibuliwa dhidi yake zinaendelea kwani simu yake ya kiganjani inaita pasina kupokelewa.

Jana Jumamosi, baada ya kauli ya Dk Bashuru, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari, mkoani Morogoro alisema Dk Bashiru alizungumzia maneno ambayo si ya kiungwana na yamejaa ukakasi na yamelenga kwenda kuichonganisha Serikali na wananchi hasa wakulima.

Alisema ileweke kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa inayoenda kuacha alaama kwa Watanzania ikiwemo kuweka ruzuku katika mbolea ili kupunguza bei ya pembejeo hiyo nchini.

Alisema pia Serikali imetoa vitendea kazi, pikipiki, vipima udongo na kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo, lengo likiwa ni kusaidia kukuza uchumi hasa katika sekta ya kilimo nchini.

“Sasa inapotokea kiongozi ambaye ana dhamana kubwa anatoa maneno yenye ukakasi na kusema viongozi hawapaswi kupongezwa bali wanapaswa kutolewa matamshi ya kuwashinikiza ili waweze kuwatendea wakulima, hiyo siyo sawa,”alisema Kihongosi.