Kibano cha Trump, asasi zaendelea kulia na ‘ukame’
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, akikabidhi vyeti kwa watetezi wa Haki za Binadamu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Katika Mkutano wao wa Mwaka, jijini Dar es Salaam, Julai 2026.
Muktasari:
- Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani kumeacha pengo kubwa kwa asasi za kiraia kote duniani, wadau hapa nchini waanza kutafuta mbinu mpya za kujitegemea huku wakionya huduma za haki za binadamu na utawala bora ziko hatarini.
Dar es Salaam. Kusitishwa kwa misaada ya kifedha kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (USAID), Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo na taasisi nyingine za Marekani kunaendelea kuathiri shughuli za asasi za kiraia nchini, huku wadau wakionya kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha utetezi wa haki za binadamu, uwajibikaji na utoaji wa huduma za kijamii.
Hofu hiyo imeelezwa leo Ijumaa, Julai 24, 2026 katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Baadhi ya viongozi wa mashirika ya kiraia wamesema kuna taasisi tayari zimeanza kukabiliwa na upungufu wa fedha za uendeshaji na sasa zinalazimika kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuendelea kutoa huduma.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Programu wa THRDC, Wakili Halima Sonda amesema kusitishwa kwa ufadhili huo kumeathiri uwezo wa asasi za kiraia kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.
"Kupungua huku kwa fedha kunaathiri nafasi yetu kama asasi za kiraia katika jamii na nchini kwa ujumla. Hali hii inaweza kuathiri ustawi wa jamii, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu," amesema.
Watetezi wa Haki za Binadamu kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na washirika wengine wakishiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka, jijini Dar es Salaam, Julai 2026
Ameiomba Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuongeza uwekezaji katika asasi za kiraia, akisema zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utawala bora, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kuwafikia wananchi.
Naye Mratibu wa Jukwaa la Haki za Watoto Tanzania, Ombeni Kimaro amesema athari za upungufu wa fedha hazitaishia katika uendeshaji wa mashirika pekee, bali zinaweza kuongeza hatari ya ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na baadhi ya taasisi kushindwa kuendelea na shughuli zake.
"Hili si tatizo la fedha pekee, bali ni pengo katika utetezi wa haki za binadamu ambalo linaweza kuwaacha wananchi wengi bila msaada wanaouhitaji," amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar (ZCRF), Sophia Leghela, ameiomba Serikali kuongeza bajeti inayotengwa kwa shughuli za utetezi wa haki za binadamu, hususan haki za watoto, ili kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto na kuongeza uwezo wa asasi za kiraia kutekeleza wajibu wake.
"Asasi za kiraia ni wadau muhimu wa maendeleo. Kudhoofika kwake kunaweza kuathiri uwajibikaji wa viongozi na maendeleo ya taifa kwa ujumla," amesema.
Akizungumza kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Wakili Tike Mwambipile, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kupunguza utegemezi wa wafadhili wa nje kwa kuanzisha vyanzo vyao vya mapato na kuimarisha ushirikiano baina yao.
"Lazima tuanze kujenga uchumi wetu wenyewe. Tukishirikiana kama wadau wa asasi za kiraia, tutakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili misukosuko ya kifedha," amesema.
Akichangia mjadala huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewataka viongozi wa asasi za kiraia kuyaona mabadiliko hayo kama fursa ya kujinasua kutoka kwenye utegemezi wa wafadhili wa nje kwa kubuni mifumo endelevu ya kujipatia mapato.
Amesema kujenga misingi imara ya kifedha kutaziwezesha asasi hizo kuendelea kutekeleza majukumu yake hata pale ufadhili wa nje unapopungua au kusitishwa.
Mtazamo huo umeungwa mkono na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye hivi karibuni amewahakikishia watetezi wa haki za binadamu kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Pia ametaja hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kulipatia THRDC kiwanja jijini Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya taifa ya mtandao huo kuwa sehemu ya jitihada za Serikali kuziimarisha asasi za kiraia nchini.
Wito wa wadau hao unakuja wakati ripoti ya kimataifa ya shirika la People in Need (PIN) ya Machi 2025 ikionya kuwa kusitishwa kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kumesababisha mashirika mengi ya kiraia duniani kupoteza kati ya asilimia 40 na 100 ya bajeti zao za uendeshaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali hiyo imeathiri watetezi wa haki za binadamu, vyombo huru vya habari na mashirika yanayopambana na rushwa katika maeneo mbalimbali duniani, huku ikionya kuwa bila vyanzo vipya vya mapato, taasisi nyingi zitashindwa kuendelea na shughuli zake.
Kwa Tanzania, mjadala unaoendelea sasa umejikita katika kutafuta njia za kujenga mifumo ya ndani ya kifedha itakayowezesha asasi za kiraia kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa uendelevu, hata pale misaada kutoka kwa wafadhili wa kimataifa inapositishwa.