Kibano kipya kwa wafanyabiashara

Tuesday June 28 2022
kibanooopic
By Sharon Sauwa

Dodoma/Dar. Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 unaoanza kujadiliwa leo umependekeza faini ya Sh100,000 kwa kampuni itakayoshindwa kuwasilisha taarifa za wamiliki wanufaika au kuwasilisha ritani.

Adhabu hiyo itakayowahusu pia maofisa wa kampuni husika watakaochangia ucheweleshaji huo, itaenda sambamba na Sh10,000 itakayotozwa kila siku itakayozidi kabla ya kulipwa kwa faini husika.

Muswada huo utakaojadiliwa bungeni, unapendekeza marekebisho katika sheria kadhaa ikiwamo ya usajili wa majina ya biashara na sura ya 212 ya Sheria ya Makampuni.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo alisema hii ni mara ya kwanza sheia inaweka adhabu itakayosaidia kuongeza uwazi katika uendeshaji na usimamizi wa biashara nchini hata hivyo akapendekeza adhabu hiyo iongezwe.

“Kuna wanasiasa na watendaji wa Serikali ambao wanamiliki biashara au wanawekeza mtaji kwenye kampuni lakini hawataki wajulikane. Tatizo unakuta wao ndio watendaji katika ofisi zao na kampuni hizi zinaomba zabuni za Serikali hivyo zinashinda kirahisi hata kama hazina uwezo,” alisema Lyimo.

Katika mataifa mengine, Lyimo alisema wameweka adhabu kali kuliko hii ya Tanzania kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji wa hali ya juu na kuiwezesha Serikali kukusanya kodi inayostahili.

Advertisement

Kuhusu uwezekano wa watu kuendelea kuficha taarifa zao na kuwa tayari kulipa faini iliyopendekezwa katika Muswada huo, Lyimo alisema Bunge linaweza kuishauri Serikali kuongeza adhabu kwa watakaojaribu kufanya hivyo.

“Bunge litaujadili Muswada huu. Nadhani sio mbaya kikiongezwa kifungo kwa watu watakaoonekana wapo tayari kulipa faini kuliko kutoa taarifa husika kama inavyotakiwa,” alipendekeza Lyimo.

Katika sehemu ya sita ya Muswada huo inapendekeza kuirekebisha Sura ya 212 ya Sheria ya Makampuni. Marekebisho hayo yana vigusa vifungu vitatu vya 115, 116 na 128 ili kuweka adhabu kwa kampuni zitakazoshindwa kutunza rejesta ya wanachama na wamiliki wanufaika au kutoa taarifa ya mabadiliko kwenye rejesta, kushindwa kuweka fahirisi ya majina ya wanachama na wamiliki wanufaika.

Adhabu itatolewa pia kwa kampuni itakayoshindwa kuwasilisha ritani ya kila mwaka. Vilevile, kifungu cha 393 kinarekebishwa ili kuwawajibisha wafilisi wa kampuni kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka zinazohusiana na ufilisi.

“Iwapo kampuni itashindwa kutekeleza kifungu kidogo cha (1), (2), (4) au cha (6), kampuni hiyo na kila ofisa wake aliyeshindwa kufanya hivyo atalazimika kulipa faini ya Sh100,000 na nyongeza ya Sh10,000 kwa kila siku itakayozidi mpaka atakapoilipa,” unapendeeza Muswada.

Kwa kampuni itakayoshindwa kuwasilisha ritani ndani ya siku 28 tangu tarehe iliyotakiwa, Muswada unapendekeza kampuni hiyo pamoja na maofisa waliohusika kwenye ucheleweshaji huo kutozwa faini ya Sh100,000 na Sh10,000 ya ziada kwa siku zitakazoendelea.

Kwa wafilisi, mapendekezo yanawataka kutunza taarifa za fedha pamoja na nyaraka za kampuni husika za walau kwa miaka mitano tangu tarehe ya ufilisi huo.

Sehemu ya nne ya Muswada huo inapendekeza kuirekebisha Sura ya 213 ya Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara. Maboresho hayo yanakusudia kurekebisha tafsiri ya neno “mmiliki mnufaika” ili kuiwianisha na iliyotolewa katika Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu.

Sasa sheria inaweka vifungu vinavyolazimisha uwasilishaji wa taarifa za wamiliki wanufaika wakati wa usajili kwa biashara zinazoendeshwa kwa ubia.

“Kifungu cha 13 kinarekebishwa ili kuweka faini kwa kushindwa kutoa taarifa zinazohusiana na wamiliki wanufaika wa ubia. Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na upatikanaji wa taarifa za wamiliki wanufaika,” alisema Dk Mwigulu.

Atakayeshindwa kutoa taarifa kwa Msajili wa kampuni na majina ya kampuni kuhusu mabadiliko ya wamiliki au atakayeshindwa kutoa taarifa za wamiliki wanufaika wa kampuni inayoendeshwa kwa ubia, Muswada unapendekeza kwamba atakuwa anatenda kosa ambalo likithibitika atalazimika kulipa faini ya isiyopungua Sh1 milioni na isiyozidi Sh5 milioni.

Ukopaji wa Serikali

Muswada pia umependekeza kuifanyia marekebisho Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa lengo la kuongeza kiwango cha ukomo wa Serikali kukopa.

“Lengo la marekebisho haya ni kuiwezesha Serikali kutekeleza bajeti kikamilifu,” alisema Dk Mwigulu.

Mabadiliko hayo, yanalenga kuongeza ukomo huo mpaka asilimia 18 ya mapato ya ndai yaliyoidhinishwa.

“Inapendekezwa, kiasi cha mkopo kitakachotolewa na kisizidi asilimia 18 ya mapato ya ndani yaliyoidhinishwa kwenye bajeti ya Serikali. Mapato hayo ya ndani ni yale yaliyoidhinishwa katika mwaka husika wa fedha,” unasomeka Muswada huo.

Kuhusu mabadiliko hayo, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala alisema umakini zaidi unahitajika ili isije ikatokea Serikali ikakopa kiasi kikubwa kuliko uwezo wa kulipa hivyo kulazimika kuongeza kodi kwa wananchi.

Dk Kamala alitoa tahadhari hiyo kwa kuzingatia ukweli kwamba mara nyingi Serikali haikusanyi kiasi chote kilichopendekezwa kwenye bajeti.

“Serikali ipewe kibali cha kukopa kutoka Benki Kuu hadi asilimia 18 ya makusanyo halisi ya ndani ya mwaka uliotangulia. Isitumie makadirio ya mwaka husika ambayo uzoefu unaonyesha mara nyingi hayafikiwi. Lengo ni kudhibiti mfumuko wa bei,” alisema Dk Kamala.

Katika mwaka huu wa fedha, Serikali ilitarajia kukusanya Sh37.99 trilioni kutoka vyanzo vyote lakini hadi Aprili 2022 ilikuwa imekusanya Sh29.84 trilioni sawa na upungufu wa Sh8.15 trilioni.

“Suala la kujiuliza ni kama kwa miezi miwili iliyobaki Serikali itaweza kukusanya fedha zilizopangwa ili kufikia lengo,” alisema.

Mabadiliko mengine kwenye Muswada huo yanapendekeza kuweka masharti bima iwe lazima kwa majengo yote ya biashara, masoko ya umma, bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, vyombo vya majini na vivuko.

Lengo la marekebisho haya, Serikali imesema ni kuongeza matumizi ya bima nchini na kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika huduma za fedha.

Baada ya mwaka jana Serikali kufuta VAT kwa simu za kisasa zinazoingizwa nchini ili kuongeza matumizi ya intaneti, Muswada unapendekeza kuirudisha kodi hiyo mwaka ujao wa fedha.

Mwaka jana, msamaha wa kodi hiyo ulihusu simu za mkononi, vishikwambi na modemu.

Waajiri nao wamekumbukwa na Muswada unapendekeza wapewe motisha kwa kuirekebisha Sheria ya Mafunzo ya Ufundi Stadi. Motisha hiyo inapendekezwa kutolewa kwa waajiri wote wanaowapa nafasi ya mafunzo kwa vitendo wahitimu wa vyuo vikuu. Lengo la marekebisho hayo, Serikali imesema ni kuwawezesha kupata ujuzi na uzoefu wa kazi kabla ya ajira.

Advertisement