Kibong’oto yawataka watumishi wake kufanya uchunguzi wa afya zao

Mkurungenzi wa Hospital ya Kibong'oto,  Dk Leornad Subi akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo. Picha na Bahati Chume

Muktasari:

Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong'oto iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, imewataka watumishi wake 300 kufanya uchunguzi wa afya ili kujua hali zao.

  

Siha. Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong'oto iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, imewataka watumishi wake 300 kufanya uchunguzi wa afya ili kujua hali zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Oktoba 20, 2022 na Katibu wa Hospitali hiyo, Rose Shawa imeeleza kuwa uchunguzi huo unahusisha magonjwa ya kifua kikuu, Ukimwi, kisukari, shinikizo la damu, saratani ya shingo ya kizazi, tezi dume na homa ya ini.

"Serikali imeliona hili ili kuwalinda watumishi hawa lazima wapimwe na kupewa chanjo ili wakati wa kumuhudumia mgonjwa asipate maambukizi, tumeona maeneo mengine watumishi hao wamehudumia   wagonjwa na wakapata maambukizi na kufariki hatutaki tufike huko lazima tuwalinde.

"Mwaka huu 2022 tumelenga kuwapima watumishi wetu wanaotoa huduma za afya wapatao 300 lengo ni kuhakikisha usalama wao kwenye maeneo haya ya kazi” amesema

Kwa upande wake Mkurungenzi wa Hospital hiyo, Dk Leornad Subi amesema upimaji huo utafanyika  kwa siku 5 ili kila mtumishi wa hospitali hiyo aweze kupata nafasi ya kufanyiwa vipimo pamoja na kupatiwa chanjo.

Aidha amewataka wananchi kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara na kupatiwa chanjo ya homa ya ini kwa kuwa ugonjwa huo unaenea kwa kasi duniani.

"Ugonjwa huu umeenea kwa kasi duniani na takwimu zilizotolewa na shirika la Afya Duniani (WHO) inasema watu zaidi ya 600,000  wanafariki kwa Ugonjwa huo  kila mwaka,"