Kichanga anusurika kifo, akutwa hai kando ya mto 

Kichaka ambacho kilipatikana kichanga cha wiki tatu kilichotupwa na mama yake Evina Kivega. Picha na Mary Sanyiwa, Mufindi

Muktasari:

  • Mama na Mtoto mdogo mwingine mwenye umri wa miaka minne wauwawa na watu wasiojulikana.

Mufindi. Mtoto mchanga wa wiki tatu amenusurika kifo baada ya kutupwa kando ya mto huku mama yake Evina Kivega (33) Mkazi wa Mtaa wa Mgodi Mafinga Mjini yeye na Mtoto wake mwingine Daudi Kigulu (4) wakiuawa Shambani kwake na watu wasiojulikana.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa 12, 2023 Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgodi, Nausy Kalinga amesema alipokea taarifa za tukio hilo jana majira 12: 30 asubuhi baada ya kupigiwa simu na balozi wa Mtaa huo kwamba katika eneo la Shamba la Serikali  Lumwago ambalo wananchi wamepewa kwa ajili ya kulima kuna mauaji limefanyika kwenye misitu huo huku mtoto mchanga wa wiki tatu akikutwa bado yupo hai.

"Baada ya kupigiwa simu waliongoza yeye pamoja na  Mtendaji wa Kata ya Upendo kwenda eneo la tukio na kukuta mama huyo na mwanaye wamefariki huku mtoto mchanga wa wiki 3 akiwa bado yupo hai ndipo waliwapigia polisi kuhusu mauaji hayo," amesema Kalinga.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema mama huyo alikuwa amelima mahindi  katika shamba hilo ambalo walipewa na Sao Hill kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo  hivyo alikwenda kwenye eneo hilo kwa lengo la kuangalia mazao yake ndipo hakurudi tena nyumbani kwake hadi  taarifa za mauaji hayo ziliporipolipotiwa.

Kwa upande wake shemeji wa marejemu Damas Kigulu amesema baada ya kupokea taarifa kwa mdogo wake kuwa mke wake hajarudi nyumbani walienda kutoa taarifa katika uongozi wa Serikali kisha wakaenda shambani huko usiku wa manane ndipo walipokutana na tukio hilo ambapo mtoto mchanga alikutwa ametupwa kando ya mto akiwa bado hai.

" Baada ya kufika shambani tulikuta mke wa mdogo wangu ameuwawa pembeni akiwa na mtoto wake mdogo wa kiume naye akiwa amefariki tukaangaza kumtafuta mtoto mchanga ndipo tukasikia sauti ya mtoto analia tukaifuatilia hiyo sauti ndipo tukamkuta mtoto huyo yupo kando ya mto lakini akiwa bado yupo hai," amesema Kigulu.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dk Amatha Haule amethibitisha kupokea miili ya marehemu wa wawili na tayari imehifadhiwa katika chumba maalumu huku akieleza hali ya mtoto kuwa ni salama na hana changamoto yoyote.

" Tumepokea miwili ya marehemu wawili mama na Mtoto mwingine mdogo tumewahifadhi katika chumba maalum pamoja na mtoto mchanga wa wiki tatu tumempima lakini hana changamoto yoyote anaendelea vizuri chini ya uangalizi wa wauguzi wetu hapa hospitalini," amesema Dk Haule.