Kichwa cha treni chaibua mjadala, Serikali yafafanua

Muktasari:

  • Serikali imesema vichwa vya treni ya umeme vilivyoagizwa bado havijawasili nchini.


Dar es Salaam. Serikali imesema vichwa vya treni ya umeme vilivyoagizwa bado havijawasili nchini.

Imesema vichwa hivyo vipo kiwandani vinatengenezwa, kilichoingia nchini ni cha wakandarasi kwa ajili ya kufanyia majaribio.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa baada ya kuibuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kichwa cha treni kilichoingia nchini.

Katika ukurasa wake wa twitter, Msigwa ameandika: “MSIPOTOSHE. Vichwa vya treni ya umeme vilivyoagizwa na Serikali bado havijawasili nchini, bado vipo kiwandani vinatengenezwa. Kichwa cha treni ya umeme kilichokuja ni cha wakandarasi kwa ajili ya majaribio ya reli ya kisasa ya SGR.”

Februari 21, mwaka huu, katika ukurasa wake wa Twitter, Msigwa aliandika: “Kichwa cha treni cha umeme chawasili nchini. Ni kitakachotumika katika reli mpya ya kisasa (SGR).”

Baada ya kupost uliibuka mjadala kutoka kwa watu mbalimbali wakimuhoji Msigwa kwamba kichwa hicho ni chakavu.

Westernife aliandika: “Sisi hatujui mtuambie kwani nini serikali iko linked na manunuzi ya vichwa vyenye kutu ama muishtaki Wikipedia kwa kusema kuwa TRC imenunua hivo vichwa vibovu, tunataka vitendo sio maneno yaso miguu anzisheni case against Wikipedia mmenunua vichwa rusty mnamzingizia Yapi how.

Naye Sylvia Shikonyi Hansson alisema: “Yaani mkandarasi ansingiza chuma cha kavu nchini na mnathubutu kuleta press kutuonyesha.hivi mnatuonaje. Kwamba hatujasafiri na hatuna idea kuhusu modern stuff. Ni aibu kwa kweli kutuleta hilo likarandinga.”

Bm graphicx aliandika: “Kaka wanacho jiuliza yap markez iweje watumie kichwa Cha zamani ambacho tofauti na kile kinachotarajiwa kuja.. ufafanuzi wako.”

Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk amesema kichwa hicho ni kifaa cha kazi cha mkandarasi kwa ajili ya majaribio.

“Ni kama vile mkandarasi anavyokuja na exleta, ambacho ni kifaa cha ujenzi cha mkandarasi anakitumia kwaajili ya kutifua barabara ili aweze kutengeneza au ni kama vile fundi gari anavyokuja na spana yake kutengeneza, kwa hiyo kile ni kichwa cha mkandarasi cha majaribio kitapita kwenye reli ya kisasa.

“Kwenye hiyo video kuna injinia ambaye ni Mturuki anaelezea uwezo wa kufanya kazi wa hicho kichwa cha treni, watafanya lini majaribio na kama kina uwezo wa kutembea spidi gani na uwezo gani. Kiufupi kile ni kifaa cha kazi cha mkandarasi kimefika kwaajili ya kujaribu kupita katika reli ya SGR kwasababu sasa hivi inajengwa tu haijafanyiwa majaribio na hicho ni kichwa cha umeme,” amesema Jamila.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, vichwa na mabehewa ya TRC bado havijafika vinamaliziwa kutengenezwa viwandani.