Kigogo Maliasili asema yuko tayari kwenda jela Tanzania ikiaibika UNWTO

  • Katibu mkuu wa wizara ya utalii na mawasiliano, Dkt.Francis Michael

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Francis Michael amesema yuko tayari kwenda jela endapo Taifa litaaibika katika mkutano wa UNWTO.

Arusha. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Francis Michael amesema yuko radhi kwenda jela kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake katika maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika (UNWTO) unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza jijini Arusha katika uzinduzi wa kamati hiyo leo Mei 20, Dk Michael amesema kitendo cha kamati yake kushindwa kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya wageni ni kuliaibisha Taifa la Tanzania.

Amesema hayuPo tayari kuona Taifa likiaibika hivyo ni vyema kamati hiyo ikawajibika ili kuweza kuheshimisha nchi kwa kuwa imeaminiwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

"Mkutano huu usipoandaliwa vizuri tutapigwa mawe mpaka makaburi yetu kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yetu kwenye nchi, sitakubaliana na hilo hivyo nitatoka na kichwa cha mtu," amesema Katibu Mkuu.

Aidha Dk Michael amesema kuwa mkutano huo utakuwa na wageni mbalimbali kutoka nchi za nje hivyo ni lazima wanakamati wazingatie kuboresha mazingira na kuhakikisha kila kitu kinachohusu mkutano huo kinakuwa sawa.

"Sitaki kusikia changamoto yoyote inatokea kwa wageni kwani kwasababu hatukujiandaa vizuri huko ni kuliaibisha taifa na endepo hilo likitokea nipo radhi kwenda jela,"amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Felix John amesema tukio hilo wanalichukulia kimkakati kutokana na kuleta wageni nchini hivyo ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo ambao unalenga kuvutia watalii wanaofika Tanzania.

"Kama mnavyofahamu mkutano huu utakutanisha mawaziri wanaosimamia sekta ya utalii na uhifadhi kutoka katika nchi zote zilizopo barani Afrika ni vyema wadau wa utalii wakajiandaa kupokea wageni mbalimbali,"amesema

Tanzani iliingia makubaliano ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo machi 7, 2022 katika makao makuu ya Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) nchini Uhispania iliyosainiwa na aliyekuwa Waziri mwenye dhamana, Dk Damas Ndumbaro na katibu wa shirika hilo, Zurab Pololikashvil.