Kigogo polisi adaiwa kukimbia na Sh4.8 bilioni za ‘mazishi’

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai akizungumza kwenye moja ya mikutano na waandishi. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Ni za mfuko wa kufa na kuzikana ndani ya Jeshi la Polisi, zilichotwa kwa nyakati tofauti ambapo mmoja wa vigogo wanaodaiwa kuhusu alikatisha mafunzo na kutoweka kusikojulikana.

Dar es Salaam. Nani waliochota mabilioni haya. Hili ndilo swali ambalo wengi wanajiuliza baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini ufisadi wa Sh4.8 bilioni za mfuko wa kufa na kuzikana ndani ya Jeshi la Polisi nchini.

Awali, ufisadi huu uliibuliwa na gazeti la Mwananchi Novemba mwaka jana, ambapo baadhi ya askari walilalamika matumizi mabaya na ufisadi unavyofanywa kupitia mfuko huo wa kufa na kuzikana.

Fedha za mfuko huo hukusanywa kutokana na michango ya askari polisi na watumishi wengine ndani ya jeshi hilo kutoka kwenye mishahara.

Juzi, katika taarifa yake kwa Rais Samia Suluhu Ikulu jijini Dar es Salaam, CAG Charles Kichere alieleza kuwa katika ukaguzi maalumu katika mfuko huo alibaini upotevu wa Sh4.8 bilioni ambazo zilitumika, lakini hazikuwa zimewafikia walengwa.

“Kuna opotevu wa fedha kiasi cha Sh4.8 bilioni ambapo Sh2.4 zilitumika katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na makao makuu na Sh2.4 bilioni zilitumika pia Zanzibar bila kuwafikia walengwa,” alisema CAG Kichere katika taarifa hiyo.

“Tumefanya ukaguzi tumekuta hizo fedha zimetumika lakini hazijawafikia walengwa. Na baadhi ya wahusika walikuwa hawapo na wengine tayari wametoroka,” alimweleza Rais ambaye ndiye aliyeagiza kufanyika uchunguzi huo.

“Nashauri Jeshi la Polisi kuwatafuta wahusika ili waje kujibu hizo tuhuma za ubadhirifu wa fedha hizi ambazo ni maalumu kwa ajili ya askari wakipata shida wanapewa,” alisisitiza CAG Kichere.

Katika hilo, Rais Samia aliagiza wahusika wote watafutwe kwa hatua zaidi pamoja na kurejeshwa kwa fedha hizo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kila askari hukatwa Sh5,000 kuchangia mfuko huo na kila mwezi Jeshi hilo lilikuwa likikusanya zaidi ya Sh300 milioni kwa ajili ya kuwanufaisha polisi wanapofiwa.

Awali, mwanachama akipata msiba wa mama, mama mkwe, baba au baba mkwe mfuko ulikuwa unagharamia chakula msibani, jeneza, usafiri na mfiwa hupewa Sh1 milioni, lakini kiwango hicho kilishushwa na sasa mhusika hupewa Sh500,000.

Hata hivyo, endapo mwanachama atafiwa na mtoto, mke au yeye mwenyewe, pamoja na huduma nyingine za mazishi, ubani wa Sh1 milioni hutolewa.

Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa kama Rais Samia ataamua kuchunguza kwa undani zaidi ufisadi huo, huenda mazito zaidi yakabainika kwa kuwa mtandao huo ulihusisha baadhi ya maofisa wazito ndani ya jeshi hilo.

Kulingana na taarifa hizo, mmoja wa maofisa anayetajwa kuwa ni mshirika wa uchotaji wa fedha hizo mwenye cheo cha Mkaguzi wa Polisi, inadaiwa alitoroka katikati ya mafunzo chuo cha Polisi (Police College) na kutorokea nchini Afrika Kusini.

“Alikuwa hapa Police College kwa kozi ya ASP (Mrakibu wa Polisi) ya miezi sita, lakini fununu za kubumburuka kwa kashfa hiyo zilipoanza alikatisha masomo. Kuna wanaosema ametoroshwa na wengine ametoroka,” kilidai chanzo chetu.

Chanzo hicho kilidokeza kuwa ofisa huyo alikuwa akiishi na familia yake kwenye mjengo wa kifahari jijini Dar es Salaam, lakini polisi walipomtafuta walikuta hayupo na amehamisha familia.

“Kuna saa tunahisi labda ametoroshwa ili kupoteza ushahidi kwa sababu lazima angetaja mtandao wote unaohusisha na upigaji wa fedha hizi. Nakumbuka kuna ofisa mwingine tuliambiwa alipata mshituko na kupoteza maisha,” kilieleza chanzo hicho.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai amelithibitishia Mwananchi kuwa ni kweli ofisa mmoja anayedaiwa kuhusika ametoroka nchini na juhudi za kumsaka zinaendelea.

Agosti 30, 2022 Rais Samia aliwaambia maofisa wakuu wa Polisi yapo matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa kufa na kuzikana zinazofanywa na kwamba, fedha hizo askari anapofiwa hapewi licha ya michango kufanyika.

Siku hiyo ndiyo alimwagiza CAG Kichere kuchunguza suala hilo na taarifa nyingine za ubadhirifu ndani ya jeshi hilo, ikiwamo matumizi ya mafuta katika magari binafsi ya maofisa.


Mchongo wa upigaji ulivyokuwa

Taarifa kutoka kwa wasiri ndani ya jeshi hilo na mfuko huo, zinadai baadhi ya ‘wakubwa’, walikuwa wanatengeneza mchongo na kufanya malipo na kuyatuma kwa mhasibu katika mkoa unaolengwa, ingawa kunakuwa hakuna msiba wala aliyefiwa.

“Unakuta wanatuma labda Sh40 milioni au Sh50 milioni kwa signatory (mtia saini) au mhasibu halafu anapewa maelekezo atoe hizo fedha halafu Sh30 milioni au Sh45 milioni azitume kwenye akaunti nyingine binafsi,” gazeti limedokezwa.

“Kuna wakati anaambiwa azitoe halafu kuna ofisa anasafiri na ndege kuzifuata anarudi Dar au Dodoma. Kwa hiyo huko mkoa ambako mchezo unafanyika anaachiwa fungu lake kidogo kama bakshishi. Huo ndio mchezo wenyewe.

“Kwa hiyo kama alivyosema CAG kuna ambao walipata misiba na pesa zikatoka lakini hawakuwahi kulipwa na kuna ambazo zilikuwa zinatolewa tu kwa maelekezo na watu wanagawana wanapita hivi,” kilidokeza chanzo kingine.

Lakini mbali na utaratibu huo, inadaiwa baadhi ya vigogo walikuwa wanaandaa orodha halisi ya wanufaika na mtia saini au mhasibu anapewa maelekezo ya kuwalipa wachache na nyingine zinaingia mfukoni.

“Ninachokifahamu kuna maofisa kadhaa sio huko makao makuu tu, bali hata kwenye baadhi ya mikoa walikamatwa na kuhojiwa kuhusu hizi fedha, lakini hatukuona hatua zikichukuliwa,” ilielezwa na mtoa habari wetu.

Baadhi ya askari waliohojiwa kwenye baadhi ya mikoa kuhusu sakata hilo, wamefichua kuwa kumekuwa na urasimu katika kulipwa fedha hizo na wakati mwingine inachukua hadi miezi miwili au mitatu kwa mnufaika kulipwa.

“Mie nilipata msiba hapa ilinichukua miezi miwili kulipwa, mpaka unajiuliza mbona wakati wa kukata wanakata papo hapo kwenye mshahara, lakini kwenye malipo sasa duh, ndio nimejua baada ya ripoti ya CAG,” alieleza askari mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.


Kauli ya DCI Kingai

Akizungumza kuhusu kashfa hiyo mbali na kukiri kigogo mmoja kutoroka nchini, Kingai pia alisema tayari walishaanza kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Alisema tayari kesi zimefunguliwa mahakamani ili kuwawajibisha polisi wote waliohusika na sakata hilo.

“Kwa hiyo tulishaanza kuchukua hatua hata kabla ya ripoti ya CAG kuwekwa hadharani, hivyo Watanzania waelewe kilichofanyika ni uhalifu kama uhalifu mwingine na wahusika wanashughulikiwa kama wahalifu wengine,” alisema DCI Kingai.

Alisema kwa mujibu wa sheria hakuna mtu hata akiwemo ofisa wa Serikali atakayefanya uhalifu kisha akafumbiwa macho, hivyo hatua za kisheria na kinidhamu zimeanza kuchukuliwa, ikiwemo kupelekwa mahakamani.

“Kuna mmoja amekimbilia nje ya nchi na tunaendelea kumtafuta kupitia polisi wa kimataifa kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa wote waliohusika,” alisema DCI Kingai.