Kigogo UVCCM kitanzini kwa madai ya rushwa

Muktasari:

  • Ni mwendo wa kulipuana, ndivyo unavyoweza kueleza baada ya watendaji na wanasiasa, wakiwemo wabunge kuamua kutema nyongo.

Arusha. Ni mwendo wa kulipuana, ndivyo unavyoweza kueleza baada ya watendaji na wanasiasa, wakiwemo wabunge kuamua kutema nyongo.

Hatua hiyo inatokana na kauli za hivi karibuni za wanasiasa ndani na nje ya Bunge kutoleana uvivu baada ya kuona wengine wanakwenda kinyume na maadili.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemlipua Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Kenani Kihongosi, akimtuhumu kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Gambo, ambaye kabla ya kugombea ubunge katika jimbo hilo amewahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha, pia amemtaja Kihongosi kushirikiana na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya jiji hilo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hata hivyo, Kihongosi ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo amejibu kuwa Kamati ya Maadili ya CCM ndiyo yenye uhalali wa kuchunguza tuhuma dhidi yake na kuzitolea ufafanuzi.

Lakini, wakati Kihongosi akitoa kauli hiyo, Majaliwa amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza uchunguzi juu ya tuhuma hizo mara moja.

Katika ziara yake jijini hapa juzi, Majaliwa pamoja na hilo, alitangaza kuwasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, akiwemo mkurugenzi, Dk John Pima kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Ni katika tukio hilo, Gambo alidai kuwa viongozi hao wameingiziwa fedha kwenye akaunti zao kutoka akaunti za halmashauri.

Alisema kuwa Kihongosi kupitia akaunti ya mkewe amewekewa Sh2 milioni na Dk Pima, fedha hizo ikielezwa ni kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya wanawake wakati yeye (Kihongosi) ni Katibu Mkuu wa UVCCM.

“Dk Pima mwenyewe alikwenda benki akaweka Sh2 milioni kupitia akaunti ya mkewe (Kihongosi) iliyopo Benki ya NMB. Na ndio maana utamuona huyu ni katibu wa Taifa lakini kila siku anashinda Arusha kwa sababu pale kuna asali ambayo anailamba kidogo,” alidai Gambo.

Akifafanua, alidai fedha hizo zimepitishwa kwenye akaunti namba (zinahifadhiwa) huku akisisitiza kuwa mtandao huo una vigogo wengi ambao kwa sasa ameamua kuwahifadhi kwa alichosema kulinda heshima ya Serikali.

Gambo akiwa mkuu wa mkoa ilijikuta kwenye migogoro ya mara kwa mara na watendaji wa chini yake, akiwatuhumu kwenda kinyume na maadili na kushindwa kusimamia masilahi mapana ya wananchi wa Arusha.

“Kila siku wanatwambia mbunge mkorofi, mgovi na haelewani na watu. Lakini, sielewani na watu kwenye mambo ambayo hayana masilahi kwa wananchi.

“Tumeenda kuomba kura na wananchi wametuchagua na uchaguzi ulikuwa mgumu, hivyo tuna wajibu wa kulinda masilahi mapana ya wananchi.


Kauli ya Kihongosi

Akizungumza na Mwananchi jana, Kihongosi alisema kuwa Gambo ametoa tuhuma hizo kwenye kikao na yeye ni kiongozi mwenye dhamana ya chama, upo utaratibu wa vikao na kamati za maadili na kwamba kama kuna tuhuma dhidi ya viongozi, kamati hizo huchunguza.

“Chama chetu kina utaratibu wa vikao, hivyo siwezi nikazungumza katika mtandao au chombo cha habari kwa sababu chama kina taratibu za vikao. Vikao vya chama kuna kamati ya maadili,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge alisema licha ya tuhuma zilizotolewa na Gambo, wenyewe watasimamia maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa ya kufanya uchunguzi.

“Zile ni tuhuma zimetolewa na mbunge, lakini sisi tunasimamia maelekezo ya Waziri Mkuu ya kufanya uchunguzi. Naomba niishie hapo kwa sababu tunafanya uchunguzi, vitu vingine naomba ni si-comment (nisizungumzie). Hiki ni chombo cha uchunguzi naomba ieleweke, hatuko very specific (hatuangalii eneo moja), tunamchunguza fulani na fulani,” alisema.

Mbali na Dk Pima, wengine waliosimamishwa na Majaliwa ni mchumi wa jiji hilo Innocent Maduhu, Alex Daniel na Nuru Gana kutoka ofisi ya mchumi, Mweka Hazina wa Halmashauri, Mariam Mshana na ofisa manunuzi Joel Mtango, ambaye alihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zelotte Stephen alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa linamhusu kiongozi wa chama Taifa, hivyo wanalazimika kukaa kimya na wenye jukumu la kuzungumzia ni ngazi ya Taifa.

Katibu wa NEC ya CCM (Itikadi na Uenezi), Shaka Hamdu Shaka alipotafutwa na Mwananchi jana jioni kuzungumzia suala hilo hakupatikana kupitia simu yake.