Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiingereza bado shida matokeo darasa la saba

Muktasari:

Wakati asilimia 67.7 ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka huu wakipata daraja D katika somo la Kiingreza, wadau wamesema shule za sekondari zinakwenda kupata mzigo mkubwa.


Dar es Salaam. Wakati asilimia 67.7 ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka huu wakipata daraja D katika somo la Kiingreza, wadau wamesema shule za sekondari zinakwenda kupata mzigo mkubwa.

Wakati ufaulu wa somo hilo ukiwa chini, lugha hiyo ndiyo itakwenda kutumika kufundishia, jambo ambalo wadau wanaeleza litafanya wanafunzi wapate ujuzi usiostahili kutokana na kusoma kwa kukariri.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Athuman Amasi watahiniwa 912,708 wamepata ufaulu wa daraja hilo huku wengine 39,086 wakipata daraja E (sawa na asilimia 2.90).

“Katika somo la English language (Kiingereza) jumla ya watahiniwa 59,990 wamepata daraja A, 56,569 wamepata daraja B na watahiniwa 279,580 wamepata daraja C.”

Idadi ya wanafunzi waliofaulu kwa daraja A hadi C katika somo hilo ni 396,139 ambayo ni sawa na asilimia 43.4 ya wanafunzi wote waliopata daraja D.

Akizungumzia suala hilo, Dk Luka Mkonongwa ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu kishiriki cha elimu Dar es Salaam (DUCE) alisema ufaulu wa somo la Kiingereza unaonyesha ni kwa kiasi gani shule za sekondari zitakuwa na mzigo mkubwa ambao kwa wakati mwingine unaweza kuchangia kuzalisha wanafunzi wengi waliofeli. “Tusitegemee mtu aliyepata daraja D katika Kiingereza aende sekondari akafanye miujiza, wachache ambao wataangukia katika mikono ya walimu mahiri wanaweza kuwa bora, lakini wengi watakaoangukia katika mikono ya walimu wasiojituma watapata matokeo yasiyoridhisha.

Hali hiyo inaweza kuchangia kuzalisha wimbi la wanafunzi waliopata daraja sifuri katika mitihani yao ya kidato cha nne na sita, huku akitaka kuboreshwa kwa ufundishaji wa lugha hiyo, ili walau mwanafunzi anapomaliza elimu ya msingi awe na uwezo wa kuwasiliana na mwalimu wake kwa Kiingereza.

Mdau wa elimu, Dk Avemaria Semakafu alisema ufaulu katika somo hilo huenda ukawa unachangiwa na kutokuwapo kwa walimu wa kutosha katika somo husika. Pia, alisema hata walimu waliopo, hususan wale waliosoma astashahada ya ualimu waliandaliwa kwa lugha ya Kiswahili walipokuwa vyuoni.

Maoni yao hayatofautiani na ya mwandishi wa vitabu, Richard Mabala aliyesema: “Nadhani umefika wakati wa kubadili lugha ya kujifunzia kuwa Kiswahili na kuwepo na vyuo vya kufundisha lugha za kigeni kama Kiingereza, Kireno, Kifaransa, bila hivyo tutakuwa na wanafunzi wenye shahada ila hawajiamini, hawana ujuzi wa kutosha kwa sababu walisoma kwa kukariri.”