Kiini watoto kujitoa uhai mwaka 2023 hiki hapa, wadau wanena

Wakati kukiwa na matukio ya watoto kujitoa uhai, imeelezwa kuwa visa vingi huwa haviripotiwi kwa kina kuhusu mfumo wa maisha aliyokuwa akiishi mtoto husika.

Wanasaikolojia, wazazi na viongozi wa dini wanasema kuwa, kuna pengo limeachwa katika malezi na makuzi ya watoto hali inayowasababishia kuchukua uamuzi huo wa kujitoa uhai.

Mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Tiba, Teddy John anasema: “kila kitu kinaanzia nyumbani ni namna gani wazazi wamemuandaa huyu mtoto, namna gani mtoto anadhani akikosa kitu fulani basi lazima ajiue.

“Tuanze kuangalia kule nyumbani ni namna gani wazazi wanamuandaa mtoto kukubali kukosa kitu katika maisha yake,”anasema mwanasaikolojia huyo.

Anasema wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto kuambiwa hapana ili watapokuja kuambiwa hapana katika maisha yao wasijisikie vibaya na kuchukua hatua za kujiua.

John anasema wazazi pia, waelewe wana uhuru wa kumpa adhabu mtoto bila kuogopa kuwa nikimpa adhabu basi atajiua.

Pia, anaviomba vyombo vya habari vinapochukua matukio ya kujiua kwa watoto viwe vinatafuta sababu zaidi ili watu waweze kuelewa chanzo.

Mwanasakolojia mwingine, Costastine Michael anasema baada ya kuona dalili za mtu kutaka kujiua ni jukumu la jamii kumsaidia mtu huyo ili kumuepusha na kujiua hata kama yeye mwenyewe haelezi kinachomsibu.

Anasema hatua inayotakiwa kuchukuliwa ni kuelezwa ukweli kuhusu anavyoonekana ili mhusika aweze kujinasua katika changamoto hiyo ikiwamo kusaidiwa kuanza upya kama amekata tamaa kwa kukubali hali halisi iliyopo kwenye maisha yake.
 

Watoto wajengewe hofu ya Mungu

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Alhaj Mustafa Shaban anasema hali ya kujiua inasababishwa kutokuwa na hofu ya Mungu inayoanzia kwenye malezi nyumbani.

“Tuzilee familia zetu katika maadili mema lakini hofu ya Mungu ambayo tunatakiwa kuanza nayo ni sisi wazazi kwa kuwaeleza watoto athari ya mtu anayejitoa uhai wake mwenyewe kuwa atakuwa hana mapokeo mazuri kwa Mungu,”anasema.

Sheikh Rajabu anasema watoto waelezwe kufanya hivyo ni miongoni mwa maasi makubwa kwa kuwa ni sawa na kutoa uhai wa mwenzake.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amon Kinyunyu anasema kinachohitajika ni wazazi kukaa na watoto kwa upendo.

Anasema kinachowafanya watoto kukata tamaa ni kutokana na wazazi au walezi kutowajibu kwa upendo.

“Tunapowajibu watoto kwa hasira, tunawajibu kama sio haki yao kupata hayo mahitaji. Tuwaambie kuwa tunawapenda, tungependa wewe ufanye hivi na vile. Mtoto akiona unajibu kwa upendo anaelewa, lakini kama unajibu kama kwamba amekosea hatochukua uamuzi mzuri,”anasema.

Askofu Kinyunyu anasema ni vyema wazazi wakawashirikisha watoto kujua hali zao za kiuchumi ili hata wanapokosa kitu wanachokitaka, waelewe ni kwasababu gani wameshindwa kukipata.

Anasema iwapo wazazi wanakaa wenyewe na kuambizana hali zao za kiuchumi, wanapokuja kuwaeleza watoto kuwa hawawezi kuwatekelezea hitaji lao wanawaona kuwa ni waongo.

Askofu Kinyunyu anataka watoto waelezwe pia vyanzo vya mapato vya familia ili wafahamu uwezo wa wazazi au walezi wao na wanapokosa mahitaji yao waelewe.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), watu zaidi ya 800,000 hufariki dunia kwa kujinyonga kila mwaka huku vifo kwa vijana wenye miaka 15 hadi 29, vikishika nafasi ya pili.

Asilimia 77 ya wanaofariki dunia kwa kujinyonga ni watu kutoka nchi zenye uchumi wa chini na wa kati.

Kwa mujibu wa wanasaikolojia miongoni mwa dalili na sababu zinazotajwa kusababisha watu kujiua ni msongo wa mawazo, upweke, kukata tamaa, kuahirisha mambo na kukosa ushauri kwa watu waliowahi kubakwa na matatizo ya afya.

Nyingine ni kuahirisha mambo, kujiona mkosaji, mazungumzo ya kujiua, aibu na kutoangalia usoni, sonona, magonjwa ya akili, kujitenga na wanadamu, unywaji wa pombe kupita kiasi na dawa za kulevya na hofu.

Matukio ya kujinyonga huacha vidonda kwa wazazi, walezi na hata jamii inayowazunguka na sintofahamu pale yanapohusisha na ushirikina.
 

Wanachosema wazazi

“Turudi tukaangalie wapi tulipokosea, tujisahihishe ili turudi katika sehemu sahihi kwenye malezi ya watoto wetu.
“Watoto wengine wanafikia hatua hiyo kwa sababu hawajajengewa uwezo wa kujieleza. Hali hii inawafanya hata wanapokuwa na changamoto kushindwa kuziwasilisha mahali husika,” anasema Stegomena Alex.

Anasema baadhi ya watu wanafikiri watoto hawana misongo ya mawazo, jambo ambalo halina ukweli, watoto wanakabiliwa na changamoto hiyo kama ilivyo kwa watu wazima.

Alex anasema upo umuhimu wa wazazi kujenga urafiki na watoto wao ili waweze kujieleza changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku iwe shuleni na hata katika mazingira ya nyumbani.

Anasema pia, watoto waelezwe kuwa marafiki na ndugu wakati mwingine wanaweza kuwakwaza kwa sababu nao ni binadamu kama walivyo wengine, hivyo wanapaswa kuwasamehe na kuendelea na maisha.

Mariam Msabaha anasema tatizo kubwa, wazazi wa siku hizi wanakwepa kuwajibika kufuatilia mambo ya watoto wao na kuwaeleza ukweli kuhusu hali yao ya kiuchumi inayowakabili kwa wakati huo.

“Epuka kumdanganya mtoto ama kutoa ahadi za uwongo usizoweza kuzitekeleza; na kama ikitokea umechelewa au huwezi kulitekeleza kwa wakati huo, zungumza na mtoto na kumweleza hali halisi, kama ni suala la shuleni mweleze hatua ulizochukua katika kukabiliana nalo,”anasema.

Anasema kwa mfano umeshindwa kulipa ada kwa wakati nenda shuleni waeleze walimu juu ya changamoto hiyo kisha mweleze mtoto asijisikie vibaya kwa kuwa umeshazungumza na mwalimu na umeahidi utalipa wakati gani.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina Mama Othuman anasema malezi ya kumdekeza mtoto ndio yanayochangia baadhi yao kujichukulia sheria mkononi kama kujitoa uhai kwa kuona wameonewa.

“Mtoto anapodekezwa sana, hata akikosea anataka asiambiwe chochote, akisemwa anachukia anahisi hapendwi, mwisho wa siku anachukua uamuzi wa kujiua,” anasema Mama Othuman.

Hata hivyo, anawashauri wazazi na walezi kuwalea watoto katika misingi yote kwa maana ajue katika maisha, kuna kukosea na kupatia kwa kuwa hakuna binadamu ambaye hajawai kukosea.
 

Matukio ya kujitoa uhai

Mitandio, khanga, kamba na chandarua ni miongoni mwa vitu ambavyo vimetajwa kutumiwa na watoto wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi kukatisha uhai wao huku wengine wakiacha ujumbe kwa wazazi na walezi wao.

Moja kati ya matukio hayo yaliyojitokeza mwaka huu ni lile la mwanafunzi wa darasa la sita Ibrahim Edson (12) katika Shule ya Msingi Lyoto, Kata ya Ilemi jijini Mbeya.

Mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani chumbani kwake, chanzo kikidaiwa ni hasira baada ya kukaripiwa na ndugu zake.

Mbali na tukio hilo, lingine ni la mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kambarage katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, lililotokea Februari 20 mwaka 2023.

Mwanafunzi huyo, Tatu John (10) alidaiwa kujinyonga kwa kutumia chandarua kwenye chumba cha kulala wageni nyumbani kwao.

Juni 27, 2023, mwanafunzi wa Kijiji cha Ikengwa Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma, Zamada Jafari (13) alifariki dunia kwa kile kilichoelezwa alinyonga kwa kutumia mtandio wa mama yake chanzo kikiwa ni kukosa nguo za sikukuu.

Septemba 30, 2023, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi ya Majengo, Wilaya ya Same Brian Elisha (12) alijiua kwa kujinyonga na shuka akiigiza kama filamu ya kujinyonga aliyopenda kuiangalia.

Desemba 6, 2023, mwanafunzi wa darasa la kwanza, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Fahad Juma (6) alijinyonga kwa kutumia chandarua katika chumba alichokuwa akilala yeye na ndugu zake.