Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto wabuni mbinu mpya kuhifadhi, kutumia dawa za kulevya

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally (aliyesimama) akizungumza na wajumbe wa kamati ya amani Mkoa wa Mwanza (waliokaa) wakati wa ‘kikao cha tathmini ya mchango viongozi wa dini katika kupambana na ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni’ kilichofanyika leo Ijumaa Desemba 15, 2023, mkoani humo. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Pamoja na kuibuka mbinu mpya za matumizi ya dawa za kulevya zinazosababisha watoto kuwa waathirika wa matukio ya ukatili wa kijinsia, takwimu za utafiti wa afya na idadi ya watu nchini (TDHS) zinaonyesha kupungua kwa visa vya ukatili mkoani Mwanza kutoka asilimia 60 mwaka 2015 hadi 47 mwaka 2022.

Mwanza. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto (Kivulini) umebaini mbinu mpya inayotumiwa na watoto kuhifadhi na kutumia dawa za kulevya ikiwemo kuchanganya vilevi na dawa kwenye juisi ya ndizi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kivulini, Yassin Ally, ameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 15, 2023  wakati wa kikao cha tathmini ya mchango wa viongozi wa dini katika kupambana na ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni mkoani humo.

Ally amesema kutokana na kuongezeka kwa mbinu za udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya na vilevi, watoto wamebuni mbinu ya kuhifadhi pombe na dawa hizo kwenye juisi ya ndizi kwa kile kinachodaiwa si rahisi kwa wazazi na walezi kunusa harufu yake.

“Tukiwa na wataalamu wetu wa saikolojia tulipotembelea shule za msingi jijini Mwanza (bila kuzitaja) baadhi ya watoto walikiri kutumia pombe na dawa kwa kuziweka kwenye juisi hiyo. Walisema wanafanya hivyo, ili kuzuia kubainika kwani inadaiwa juisi ya ndizi hukata harufu,” amesema.

Mbali na juisi hiyo, ametaja mbinu nyingine ni matumizi ya rangi ya mdomo ‘lipstick’, saa na matumizi ya maneno maalumu ikiwemo ‘bahasha’ ambalo humaanisha ‘ugoro’ huku akiwataka wazazi kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa kina kwa watoto wao wanapokuwa na vitu hivyo.

Ametaja athari za watoto kutumia pombe na dawa za kulevya, wengine hujikuta wakitendewa vitendo vya ukatili kwa urahisi, huku wengine wakifanyiana wanapokutana katika taasisi za kielimu na kidini kutokana na kutojitambua wanapotumia dawa hizo.

“Changamoto ni kwamba wazazi wengi siku hizi hatulei watoto, tunawafuga. Hatutengi muda wa kufuatilia mwenendo wa watoto wetu, mwingine unakuta akimaliza kula ama akiwa chumbani anakuwa na chupa yenye kinywaji ukichunguza utakuta kuna pombe humo, shtukeni,” amesema.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amewataka wazazi na walezi kutofumbia macho ukuaji wa teknolojia kwa kile alichotaja kuwa watoto wameanza kuwazidi wazazi kwenye ufahamu wake, hivyo kuitumia kufanya vitendo vya ajabu ikiwemo kufanya ngono na kutumia dawa za kulevya.

Sheikh Kabeke amesema pamoja na kuendesha kampeni ya kupinga ukatili na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu mbinu ambazo ukatili unatendeka, mawaidha yataanza kutolewa kwa wazazi kuhusiana na mbinu hizo.

“Tunaishi katika jamii ambayo watoto wanatuzidi uelewa wa teknolojia, wazazi tuanze kufanya ufuatiliaji wa karibu wa watoto wetu na kuwakagua shughuli wanazofanya kwa sababu kuwa na familia salama ndiyo kunaleta jamii salama,” amesema Sheikh Kabeke.

Naye, Mkazi wa mtaa wa Uhuru jijini Mwanza, Sikitu Mohammed amewaomba viongozi wa dini, Serikali na mashirika kutochoka kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na vitendo hivyo, ili kuvidhibiti na kujenga jamii salama.