Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kijana adaiwa kumuua baba yake

Muktasari:

  • Daktari Samwel Tenga alishambuliwa na mwanaye huyo, Honest Samwel Desemba 10, na kipande cha mti, hali iliyompelekea kuvuja damu nyingi, ambapo alipelekwa katika Hospitali ya Mawenzi na kufariki dunia wakati akipata matibabu.

Moshi. Daktari Mstaafu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, Samwel Tenga (68) amefariki dunia baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mtoto wake, Honest Samwel (33) ambaye anadaiwa kuwa mgonjwa wa afya ya akili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 11, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema lilitokea Desemba 10, 2023 katika kijiji cha Lowasi, Wilaya ya Moshi, na kueleza kuwa, daktari huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mawenzi.

Kamanda Maigwa amesema daktari huyo alishambuliwa na mwanaye  saa 7:50 mchana Desemba 10  na kipande cha mti, hali iliyomsababishia kuvuja damu nyingi, ambapo alipelekwa katika Hospitali ya Mawenzi na saa 1:00 usiku alifariki dunia.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia, ambapo inadaiwa kuwa kijana huyo alikuwa akiharibu vitu vya nyumbani na hakutaka kukemewa hivyo alipokemewa na baba yake huyo, alianza kumshambulia kwa kumpiga na kipande cha mti sehemu ya kichwani, hali ambayo ilisababisha kifo chake.

"Daktari mstaafu mkazi wa Lowasi alifariki dunia wakati anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mawenzi, baada ya kushambuliwa na mwanaye kwa kupigwa na kitu butu kichwani maeneo ya kisogoni, na chanzo cha tukio hili ni ugomvi wa kifamilia," amesema Kamanda Maigwa.

Hata hivyo Kamanda Maigwa amesema mtuhumiwa huyo, ambaye anadaiwa kuwa na matatizo ya akili, amekamatwa na amepelekwa katika Hospitali ya Mawenzi ambapo amelazwa katika chumba cha wagonjwa wa afya ya akili.