Kijana aliyesaidia kuokolewa manusura ajali ya ndege apewa Sh1 milioni

Majaliwa Jackson, mvuvi aliyefanikisha kuufungua mlango wa ndege na kufanikisha kuokolewa kwa abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Vickoria.

Muktasari:

  • Majaliwa Jackson, mvuvi aliyefanikisha kuufungua mlango wa ndege na kufanikisha kuokolewa kwa abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Vickoria amekabidhiwa Sh1 milioni kwa kutambua juhudi na moyo wake wa kujitolea.

Bukoba. Majaliwa Jackson, mvuvi aliyefanikisha kuufungua mlango wa ndege na kufanikisha kuokolewa kwa abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Vickoria amekabidhiwa Sh1 milioni kwa kutambua juhudi na moyo wake wa kujitolea.

 Katika juhudi hizo, Majaliwa alijeruhiwa na mlango wa ndege hiyo iliyotumbia jana Jumapili Novemba 6, 2022 karibu na Uwanja wa Ndege Bukoba, Mkoa wa Kagera na kukimbizwa Hoaspitali ya Rufaa Mkoa wa Kagera kwa matibabu akiwa na majeruhi wengine 25 wa ajali hiyo wakiwemo abiria 24 na mtumishi mwingine wa uwanja wa ndege.

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati wa ibada ya kitaifa ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili 19 ya waliofariki katika ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewapongeza na kuwashukuru wote waliojitolea kwa hali na mali kuokoa majeruhi na kuvuta ndege kutoka ndani ya maji ya Ziwa Victoria.

"Kipekee nampongeza kijana mdogo mvuvi ambaye kwa ujasiri mkubwa alitumia kasia kufungua mlango wa ndege na kufanikisha abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege kuokolewa," amesema Chalamila


Mkuu huyo wa mkoa ameuambia umma unaohudhuria ibada hiyo inafanyika uwanja wa Kaitaba leo Jumatatu Novemba 7, 2022 kuwa katika harakati hizo, kijana Majaliwa aliyekuwepo uwanjani hapo naye alijeruhiwa lakini hali yake tayari imeimarika.


Chalamila amekabidhi kiasi hicho cha fedha alichosema ni agizo la waziri mkuu huku akiwaomba watu wengjne kujitokeza kumshika mkono ambapo Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Stephen Byabato aliitikia kwa kumpa kijana huyo Sh300, 000.


Akitoa salaam kwa niaba ya wananchi wa Bukoba, Byabato ambaye pia naibu waziri wa nishati ameahidi kushirikiana na wadau wengine kusaidia kuboresha mazingira na mahitaji ya kikazi kwa wavuvi waliojitolea kushiriki uokozi baada ya ajali.